BEI YA RAMANI YA UJENZI SIO KUBWA, BALI INAENDENA NA THAMANI YA MRADI.

Baadhi ya watu wamekuwa wakiuliza gharama za ramani za ujenzi na kushangaa pale wanapotajiwa bei na kuona kwamba ni bei kubwa huku hoja yao kubwa ikiwa ni kwa sababu mtu anatumia tu akili yake na hakuna gharama kubwa anayotumia kutengeneza ramani husika zaidi ya akili yake. Hapa kwanza jambo muhimu la kujua ni kwamba gharama ya kazi haipo kwenye faida au hasara peke yake, bali gharama ipo kwenye muda unaoutumika na kiwango cha ubora kinachopatikana kutokana na thamani na ubora wa huduma husika. Tukianza na suala la muda, kazi ya kutengeneza ramani inahusisha vitu vingi sana na hata matokeo yake ya mwisho ni kutengeneza seti 7 mbalimbali za michoro katika nakala ngumu(hardcopies) angalau tatu. Muda ambao mtu anaweka katika kazi husika na mwingi na unaotumia sana nguvu ya akili kutokana na umakini unaotakiwa kwenye kufanya kazi bora na yenye usahihi. Pia ubora wa huduma unahusisha muda na nguvu kubwa ya akili kufanikisha kazi yenye thamani kubwa na iliyofanyika kwa usahihi.

MUDA UNAOWEKWA NA UBORA WA HUDUMA UNAOKUJA KAMA MATOKEA NDIO THAMANI YENYEWE MRADI HUSIKA

Suala la pili ni ukubwa na thamani ya mradi husika na dhamana ambayo mtu anachukua kwa kujihusisha na mradi husika. Wote tunajua kwamba gharama za ujenzi ni kubwa sana, kwa mfano utakuta nyumba inayogharimu kiasi cha shilingi milioni 130 za kitanzania ramani yake inagharimu kiasi cha shilingi 650,000 ukijaribu kuangalia uwiano wa gharama utakuta gharama ya ramani haifiki hata asilimia 1% ya gharama yote ya ujenzi, yaani ni kama asilimia 0.5% ya gharama yote ya ujenzi, japo ramani ndio inayotoa miongozo yote ya kitaalamu katika jengo. Hiyo 0.5% ni kiasi kidogo sana ukilinganisha na gharama nyingine za ufundi wakati wa kutekeleza mradi husika. Jambo lingine muhimu la kuzingatia ni dhamana ya mradi husika, ambapo pale inapotokea jambo lolote katika mradi husika labda maafa fulani yametokea au watu wa mamlaka husika wanahitaji kumwajibisha mtu kwa jambo lolote hapo mtu atakayekamatwa ni mtaalamu husika wa jengo hilo, hivyo anabeba dhamana kubwa sana ya mradi wa mamilioni ya pesa kwa hiyo kutokana na dhamana na wajibu alionao katika mradi husika sio mtu anayetakiwa kuwa kwenye dhamana kubwa kwa kufanya kazi kama mtu wa nyongeza.

DHAMANA NA WAJIBU NI VITU VYENYE GHARAMA KUBWA SANA KWA MIRADI MIKUBWA KAMA YA UJENZI

Hivyo muda, utaalamu, dhamana na wajibu kwa mradi husika ni vitu vinavyomgharimu sana mtu kiasi kwamba hata malipo yake kwa uwiano hata wa huduma nyingine za ufundi bado na madogo. Hivyo badala ya kuangalia gharama moja ambayo mara nyingi hata haifikiriwi kwa usahihi inatakiwa kuangalia mradi mzima kuweza kuona mambo katika uhalisia.

Architect Sebastian Moshi.

Whatsapp/Call +255717452790.

0 replies

Leave a Reply

Want to join the discussion?
Feel free to contribute!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *