KWA NINI NI MUHIMU KULIPIA GHARAMA YA RAMANI KABLA YA KAZI KUANZA.

Baadhi ya watu kwa sababu mbalimbali wanapohitaji kufanyiwa kazi za ushauri wa kitaalamu katika eneo la michoro ya ramani kabla ya ujenzi hupenda mtaalamu wa usanifu majengo aanze kazi ya kufanya ubunifu wa michoro na kutoa pendekezo la kwanza baada ya kuelewana bei lakini bila wao kufanya malipo ya awali. Watu hao huona hilo ni sahihi kabisa kufanyika hivyo kwa sababu huamini mwisho wa siku watalipia gharama hizo kwa hiyo hawaona sababu ya kwani mtu asiendelee na kazi wakati wameshasema kazi iendelee watafanya hayo malipo.

Katika hili baadhi ya wataalamu huendelea na kazi bila malipo lakini wengine husitisha kazi kwanza mpaka mteja husika amefanya malipo ndio nao huendelea na kazi. Jambo hili limekuwa likileta mivutano na wakati mwingine hata kupotezeana imani kwani mteja huona pengine mtaalamu haonyeshi kumheshimu wala kumwamini huku na mtaalamu naye akiona kwamba mteja hamheshimu pia na kwa nini asifanye malipo kama kweli ana uhitaji wa kazi hiyo kwa kiasi hicho na kuchukulia kwamba pengine ana agenda ya siri ndio maana anagoma kufanya malipo.

Kwenye hili japo kila mtu ana msimamo wake na ana kanuni zake anazosimamia lakini uhalisia ni kwamba sio kwamba wanaokataa kufanya kazi hiyo hawataki au wana viburi bali mara nyingi utakuta tayari hapo ni mhanga wa kukubali kufanya kazi bila malipo na kutapeliwa tena pengine sio mara moja na ndio maana anakuwa mgumu kuendelea na kazi. Kiuhalisia angekuwa ana uhakika kabisa kwamba atalipwa kwenye kazi hiyo akishamaliza kazi nina uhakika hakuna hata mmoja ambaye angekuwa mgumu kuendelea na kazi lakini kwa kuwa anajua anabahatisha ndio maana anaamua ni bora akose ajue amekosa kulipa ajaribu kufanya na kujikuta kwenye maumivu mengine ya majuto kwa nini alikubali kufanya kazi hiyo. Hata hivyo mteja anaweza kusema atatafuta mtu mwingine ambaye yuko tayari kwa masharti hayo.

Kwa nini sasa nasema ni vyema kulipia wakati unaweza kupata mtu ambaye yuko tayari kuanza kazi bila malipo. Moja kati ya faida kubwa sana za mteja kufanya malipo ya awali kabla ya kazi husika kuanza ni kazi kufanyika kwa ubora na kwa muda. Kama nilivyoeleza kwamba kazi inapokuwa haijalipiwa mtaalamu anakuwa hana uhakika kama kweli atalipwa pesa yake kitu ambacho kinapelekea kutoifanya kazi hiyo kwa moyo wala kwa ubora na ubunifu mkubwa kwa sababu anaiona tu kama kazi isiyo na thamani. Lakini pia huenda akaichelewesha sana kwa sababu kwanza hana motisha wa kuifanya na pia huenda ana kazi nyingine au majukumu mengine ambayo atayapa kipaumbele kuliko kazi yako.

Kinachokuja kutokea ni kwamba wewe mwisho wa siku unakuja kulipa pesa yote mliokubaliana lakini yeye alishaifanya kazi hiyo bila kuipa uzito mkubwa kwa hiyo kutoipa muda mwingi wala kuifanya kwa viwango vya juu. Lakini pia huenda akaichelewesha sana tofauti na muda ulioupanga wewe kwa sababu anajua kazi haina haraka wala umuhimu sana na kama ingekuwa navyo basi mteja angekuwa amelipia. Hili linasababisha kwamba kazi inaweza isiwe na ubora wa juu kwa sababu tayari haikupewa umuhimu wa kufanyika kwa viwango bora tangu mwanzoni. Lakini unapokuwa umelipia moja kwa moja mtaalamu kwanza anajihisi ana deni kwako na anaweka muda wake wote akiwa na imani 100% kwamba anafanya kazi ambayo ni bora na yenye manufaa makubwa sana.

Hivyo ni muhimu sana mnapokuwa mmekamilisha makubaliano ya bei ni vyema ukalipia na kisha kumwambia akupe tarehe ambayo atakuwa amekamilisha pendekezo la kwanza kwa ajili ya mjadala ambapo utahakikisha unamfuatilia kuhakikisha amekamilisha ndani ya tarehe hiyo. Hilo litasaidia sana kuleta utulivu kwa pande zote mbili na kupelekea kazi kufanyika kwa viwango bora.

Karibu sana.

Architect Sebastian Moshi.

Whatsapp/Call +255 717 452 790.

0 replies

Leave a Reply

Want to join the discussion?
Feel free to contribute!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *