HAWA WATU WANAKUHARIBIA KAZI NA KUKUINGIZA HASARA BILA WEWE KUJUA.
Na Architect Sebastian Moshi
Whatsapp/Call +255717452790
Ndugu Mdau wa Ujenzi
1. Siku zote sehemu inapotolewa fedha huwa kuna matata, kama kuna sehemu ya kuwa nayo makini sana ni sehemu yenye maslahi ya kifedha. Sehemu inapotoka fedha sio sehemu unayotakiwa kumuamini mtu kiurahisi kwa sababu tu ni mtu wako wa karibu, hisia za tamaa au chuki zinapomwingia mtu huacha kufikiria kwa usahihi badala yake huongozwa na tamaa, chuki au visasi.
2. Katika miradi mingi na hasa ya ujenzi kuna aina ya watu huweza kutokea ambao kwa jina la mtaani hufahamika kama “wapambe”. Hawa watu hujionyesha kama ni watu wako wa karibu na wako ili kulinda maslahi yako na kwa kawaida huwa unawaamini sana. Kwa kuwa huwa wanaonyesha kukuheshimu na kukujali sana hivyo nawe bila mashaka yoyote huwa unawaamini, na kusikiliza kila wanachokwambia, lakini wacha nikwambie kama kuna watu wa kuwa nao makini basi ni hawa watu wanaoitwa “wapambe” au watu unaowapa majukumu ya kusimamia maslahi yako katika ujenzi wakati wewe umebanwa na majukumu mengine.
3. Mara nyingi hawa watu huwa hawako kwa maslahi yako kama unavyofikiri bali kwa maslahi yao wenyewe na huongozwa na hisia za chuki, tamaa au visasi na hasa tamaa. Mara nyingi watu hawa hugeuka wachonganishi kama wanaona hawanufaiki kama walivyotegemea au kama wameshindwa kuendana au kuelewana na watu uliowapa kazi hivyo ni lazima walete mpasuko na kuvuruga maelewano ili uweke watu wengine ambao wakati mwingine wamewapendekeza wao watakaoweza kukubaliana nao kwa maslahi yao, wakati wewe ukiwa umeshaingia gharama na kupoteza muda.
4. Japo wanaweza kuwa watu wako wa karibu na saa nyingine hata ndugu zako lakini mara nyingi utakuta wana agenda zao wanazozisukuma ambazo sio agenda zako, wana malengo yao ambayo sio malengo yako na ambayo hata wewe mwenyewe huyajui ila wamekuteka kihisia na kisaikolojia bila wewe kujua. Mara nyingi utakuta wao ndio wanaolazimisha uchakachuaji au wizi wa vifaa na saa nyingine hata kuwatishia watu uliowapa kazi kama wanaenda kinyume na maslahi yao. Ila shida ni kwamba wewe unawaamini na unataka kuwafurahisha ukifikiri wako kwa ajili yako.
5. Ikitokea hawa watu wanakuja kukupa ripoti mbaya kuhusu watu uliowapa kazi ni vyema kuwaita pamoja wote na kuwahoji ili kupata ukweli. Japo ni mara chache watu hufanya hivyo, wengi hutekwa kisaikolojia na kihisia na “wapambe” na huwaamini moja kwa moja hivyo huingia kwenye mafarakano na watu waliopatana nao kazi bila kujua hilo limefanyika sio kwa maslahi yake bali kwa maslahi ya “mpambe” kutokana na wewe kumwamini sana “mpambe” na kusikiliza upande mmoja.
N:B Sio “wapambe” wote huwa wachonganishi, wapo wachache ambao hufanya kazi kwa maslahi yako, lakini ni muhimu kuwa makini kwa sababu mara nyingi hawa watu huwa na agenda zao binafsi.
*Jambo hili hutokea kwa zaidi ya 90% ya miradi ya ujenzi inayohusisha watu wa aina hiyo.
Leave a Reply
Want to join the discussion?Feel free to contribute!