UWIANO NI MUHIMU KATIKA KULETA MATOKEO BORA KWENYE UJENZI.

Uwiano kwenye ujenzi ni ule uhusiano wa gharama unaokuwepo baina ya bei za huduma zinazotolewa na gharama za ujenzi kwa ujumla. Moja kati ya sababu inayopelekea matokea mabaya, hasara na majuto ni kutokuzingatia uwiano wa kimahusiano kati ya vitu hivi.

UWIANO WA GHARAMA UNA NAFASI KUBWA KWENYE KULETA MATOKEO SAHIHI NA YANAYOTARAJIWA

Katika kupatana na watoa huduma kwenye mradi wa ujenzi hasa kwa upande wa michoro ya ramani na kandarasi yenyewe ya kujenga ni muhimu kuzingatia haya na tofauti na kama hakuna uwiano basi kuna nafasi kubwa zaidi ya kazi kuharibika. Kwa mfano unakuta mtu anajaribu kujenga jengo linalogharimu kiasi cha shilingi milioni 300 lakini huku akijaribu kulazimisha kandarasi nzima ya ujenzi wa jengo zima kugharimu kiasi cha shilingi milioni 25, hapa unaona wazi kwamba hakuna uhusiano na kazi hii inaweza kuwa mbovu na kuleta hasara kubwa. Hii ni sawa na uambiwe unauziwa gari aina ya prado kwa shilingi milioni 7, hapo lazima ujiulize hii ni prado ya aina gani, na kwamba kuna uwezekano mkubwa aidha kuna utapeli unafanyiwa au labda hiyo Prado yenyewe imeibiwa na itakuingiza kwenye matatizo siku za karibuni.

UWIANO WA GHARAMA UNAPOKOSEKANA UNAPASWA KUPATA WASIWASI JUU YA UWEZO WA WATOA HUDUMA

Kama nilivyoeleza katika makala zilizopita ni kwamba kiwango cha gharama za michoro ya ramani yenye ubora inatakiwa kuwa katika wastani asilimia 1.5% ya gharama zote za ujenzi, huku kandarasi nzima ya kujenga jengo husika mpaka kukamilika na kuhamiwa ikiwa katika wastani wa asilimia 30% ya gharama zote za ujenzi kwa viwango vilivyowekwa na mamlaka zinazoshughulika na ujenzi ambavyo ndivyo pia hutumika katika kulipia vibali na gharama nyingine zinazotolewa na mamlaka zinazohusika na ujenzi.

Architect Sebastian Moshi

Whatsapp/Call +255717452790

0 replies

Leave a Reply

Want to join the discussion?
Feel free to contribute!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *