KUPATA KIBALI CHA UJENZI KWENYE ENEO LISILOPIMWA

Mambo mengi yanaendelea kubadilika kwa kasi katika sekta ya ujenzi kupitia mamlaka za udhibiti ambazo zinaendelea kuongeza masharti mbalimbali katika kufanikisha malengo yao mbalimbali ikiwa ni pamoja na kukusanya mapato zaidi. Zamani ilikuwa kujenga kwenye eneo ambalo bado halijapimwa haikuhitaji kupata kibali cha ujenzi kutoka halmashauri husika hata kama ni eneo lililopo kwenye mji mkubwa kwa sababu utaratibu wake ulikuwa bado haujafanyiwa kazi. Hata hivyo siku hizi mambo yamebadilika sana na ufuatiliaji wa vibali vya ujenzi unaenda mpaka maeneo yasiyopimwa na tayari utaratibu wa kupata kibali cha ujenzi katika halmashauri nyingi umeidhinishwa. Lakini hata hivyo bado kuna watu wengi hasa ambao wako kwenye maeneo ya mbali kidogo na katikati ya miji ambao hawafuati utaratibu wa kuchukua vibali vya ujenzi aidha kwa kutokujua kabisa au kwa kutofahamu utaratibu sahihi wa kufuata.

UNAWEZA KUFUATILIA UJENZI KWENYE ENEO AMBALO HALIJAPIMWA WALA KUWA NA HATI

Swali moja kubwa ni unapataje kibali cha ujenzi kwa eneo lisilopimwa, kwa eneo lililopimwa utaratibu ni kupeleka michoro ya ramani ya ujenzi husika ikiambatana na hati ya kiwanja cha eneo hilo kinachoonyesha taarifa zote za kiwanja na umiliki wa mhusika anayetaka kujenga, na baada ya kufuatilia eneo hilo katika kanzidata zao kwenye mifumo wataona kama mradi husika unakidhi vigezo vya kiwanja husika na kisha kukupatia kibali cha ujenzi au kama mradi haukidhi vigezo watakujulisha ukafanya mabadiliko sahihi kwa kuzingatia vigezo na masharti husika ili wakupatie kibali. Kwa kiwanja kisichopimwa maana yake hawana taarifa za kiwanja husika katika kanzidata zao kuweza kujua hadhi ya kiwanja na kama mradi husika wa ujenzi unakidhi vigezo vinavyohitajika ili kujengwa kwenye eneo husika, hivyo watakachohitaji ni wewe upeleke taarifa za kiwanja chako mwenyewe zikiambatana na mkataba wa mauziano ya kiwanja hicho pamoja na barua ya serikali ya kijiji husika kuthibitisha kwamba wewe ndio mmiliki halali wa kiwanja hicho na taarifa unazotoa kuhusu kiwanja hicho ni sahihi. Baada ya mamlaka husika za ujenzi kutoka halmashauri ya jiji, manispaa au mji husika kujiridhisha na hilo kwa kutembelea pia eneo husika na kulikagua na kujiridhisha kwamba umetimiza vigezo na masharti ya kwa eneo husika watakupatia kibali cha ujenzi na ikiwa hujatimiza watukujulisha mambo ya kufanyia kazi ili kutimiza vigezo husika na kupatiwa kibali cha ujenzi.

KUFUATILIA KIBALI KWENYE ENEO AMBALO HALIJAPIMWA KUNAWEZA KUWA NA MANUFAA BAADAYE

Manufaa unayoweza kupata kwa kufuatilia kibali cha ujenzi kwenye eneo lako hata kama halijapimwa ni kwamba utaweza kujiepusha au kushinda kesi ya mgogoro wowote utakaoweza kujitokeza mbeleni kwa kuhusu uhalali wa wewe kujenga eneo hilo kwa sababu utakuwa na nyaraka maalum ya ruhusa ya serikali ya kujenga eneo hilo. Manufaa mengine ni kwamba utaweza kuaminiwa kwa jambo lolote unalotaka kufanya kwenye eneo hilo na taasisi nyingine binafsi na za kiserikali kwa sababu una nyaraka halali ya kibali cha serikali cha kujenga kwenye eneo hilo.

Architect Sebastian Moshi.

Whatsapp/Call +255717452790.

0 replies

Leave a Reply

Want to join the discussion?
Feel free to contribute!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *