VIBALI VYA KUJENGA JENGO LA GHOROFA NA GHARAMA ZAKE.
Jengo la ghorofa linahitaji vibali vya ujenzi vya aina nyingi, kwanza linahitaji kibali cha ujenzi kutoka halmashauri. Kibali hiki kinachotokea kwenye halmashauri ya jiji, manispaa au mji husika ndio kibali chenye mambo mengi na ndicho huweza kupata vizuizi na kuchukua muda pia. Hata hivyo hiki ndio huwa kibali cha kwanza kupatikana kabla ya vyote. Kibali hiki kinachotolewa na halmashauri ya jiji, manispaa au mji husika hupitishwa kwenye idara zote za halmashauri kupitia michoro ya ujenzi wa mradi husika wa ujenzi.
Unachotakiwa kupeleka kule halmashauri ili upatiwe kibali cha ujenzi cha kutoka halmashauri ni michoro kamili ya ramani za jengo la mradi wako inayokidhi vigezo vilivyowekwa na halmashauri. Michoro hiyo ya ramani iliyopigwa mihuri na kampuni iliyosajiliwa utaipa kwa wataalamu wa majengo kama vile wasanifu majengo na wahandisi. Baada ya kupeleka michoro katika halmashauri ya jiji, manispaa au mji husika itakaguliwa kwenye idara ya ujenzi kama imekidhi vigezo husika nak ama inaendana na matumizi ya kiwanja yaliyoamuliwa na wizara ya ardhi kisha kupitisha kwenye kila idara ya halmashauri kwa ajili ya ukaguzi kama imetimiza vigezo vilivyowekwa na kila idara kadiri ya mipango na maamuzi yao.
Idara za halmashauri ambazo michoro hii inapitishwa ni pamoja na idara za ujenzi, idara ya mipango miji, idara ya mazingira, idara ya afya n.k., kisha itaangaliwa kama itakuwa haijakidhi vigezo utarudishiwa ili ufanye marekebisho ya michoro au kubadili matumizi ya ardhi ili kukidhi vigezo. Lakini sasa ikiwa michoro hiyo imekidhi vigezo vyote na kupitishwa itasubiri kuingizwa kwenye kikao cha timu ya wataalamu wa halmashauri ya jiji, manispaa au mji husika ambayo ndio itafanya maamuzi ya kupitisha michoro hiyo na hivyo kupatiwa kibali hicho. Kibali kitaandikwa na kuitiwa.
Baada ya kupatiwa kibali kutoka halmashauri kwa Tanzania kama jengo lako ni la kawaida nyumba ya chini isiyo ya ghorofa unaweza moja kwa moja Kwenda kuanza kujenga. Lakini kama jengo lako ni kubwa au ni ghorofa ya aina yoyote ile utapaswa kutumia kibali hicho cha ujenzi ulichopewa na halmashauri ya jiji, manispaa au mji wa eneo hilo Kwenda kuomba vibali vya kwenye bodi za ujenzi ambazo ndizo zinazosimamia taaluma husika. Bodi zako nyingi lakini kuna bodi tatu kubwa ambazo ndio muhimu zaidi kuanza nazo ambazo ni bodi ya wasanifu majengo na wakadiriaji majenzi(Architects and Quantity Surveyors Registration Board(AQRB)), kisha kuna bodi ya wahandisi (Engineers Registration Board(ERB)) na kuna bodi ya wakandarasi (Contractors Registration Board(CRB)).
Kwenye hizi bodi za ujenzi kwa miradi mikubwa ya ghorofa utatakiwa kupeleka michoro ya ramani sambamba na kibali cha ujenzi ulichopata kutoka kwenye halmashauri ya jiji, manispaa au mji husika na baada ya kukaguliwa utapewa gharama za kufanya malipo kisha utapewa stika maalum utakazokwenda kubandika kwenye kibao cha ujenzi kilichopo katika eneo ambapo mradi wa ujenzi unaendelea. Bodi hizo sambamba na stika hizo zitakupa vitabu vya kujaza maendeleo ya miradi site (logbook) kazi ambayo itafanywa na kampuni ulizoamua kufanya nazo mradi wako wa ujenzi. Kimsingi kampuni hizi ndizo zitakazochukua vibali hivyo au hizo stika kutoka bodi na kuziweka katika eneo la ujenzi zikijitambuisha kwamba zenyewe ndizo zinasimamia mradi wako kama wataalamu kwa gharama mlizokubaliana.
Sasa ukiachana na kibali cha manispaa na vibali vya kutoka kwenye bodi za ujenzi kuna vibali kutoka kwenye taasisi nyingine kama vile taasisi inayohusika na suala la usalama mahali pa kazi maarufu kama OSHA kwa kirefu (Occupational Safety and Healthy Authority). Pia kuna taasisi inayojihusisha katika kulinda mazingira, kuna taasisi inayojihusisha na masuala ya zimamoto maarufu kama “fire and safety” n.k., Kampuni zote hizi zina kazi moja ya kuhakikisha vigezo vyake vinazingatia mahali pa ujenzi.
Gharama za kupata kibali vya ujenzi kutoka halmashauri ya jiji, manispaa au mji licha ya kwamba ndio ngumu na yenye mkwamo mara nyingi lakini sio kubwa ukilinganisha na gharama za stika za bodi za taaluma hizi za ujenzi. Gharama za kulipia stika za bodi mara nyingi ni kubwa japo hakuna usumbufu mkubwa wala haichukui muda mrefu kupata. Sasa ili mtu uweze kufanikiwa kuvuka eneo hili la vibali vya ujenzi bila usumbufu mkubwa wala mivutano sana na taasisi hizi ni muhimu kutumia wataalamu wabobezi kwenye kazi hizi wakusaidie kwenye kila hatua ili uokoe muda na wakati mwingine hata gharama pia.
Karibu sana.
Architect Sebastian Moshi.
Whatsapp/Call +255 717 452 790.
Nina ndoto ya kujenga ghorofa hata tatu niandae nondo gani na tani ngapi? Nipo mwanza
Tuwasiliane whatsapp +255 717 452 790