HATUA YA KWANZA MUHIMU KWENYE UJENZI
Mara kwa mara nimekuwa ninaeleza hapa umuhimu wa kuwepo kwa mtaalamu kwenye usimamizi wa ujenzi kuhakikisha kwamba utaalamu unazingatiwa na kile kilichokusudiwa kinapatikana kwa uhakika. Kweli haya yanawezekana ikiwa kuna aidha mpango au mchakato unaofuatwa katika kufanyia kazi mradi husika au kuna mtaalamu ambaye anafahamu na anafanya maamuzi sahihi kwenye kila hatua ya ujenzi mara zote. Lakini katika hatua zote za ujenzi moja kati ya hatua muhimu sana na ya kwanza ambayo isipozingatiwa katika kufanyika kwa usahihi itapelekea matatizo makubwa mbeleni ni hatua ya kuseti jengo kwa usahihi kuanzia eneo, uelekeo sahihi(orientation), vipimo sahihi vya wima na ulalo pamoja na ukubwa sahihi uliokusudiwa kwenye ramani.
Hatua hii ni maarufu zaidi kwa lugha ya kitaalamu kama (setting out) au kulipangilia jengo katika sehemu yake kwa usahihi unaotakiwa kitaalamu. Kuna majengo mengi kwa sababu ya kukosekana kwa utaalamu au mchakato sahihi unaofuatwa katika utekelezaji wa shughuli za ujenzi yamekuwa yakifeli sana kwenye hatua hii aidha kwa kutowekwa katika uelekeo sahihi(building orientation) au kwa kukosea vipimo na mraba wa nyumba na hivyo kusababisha changamoto kubwa sana mbeleni. Lakini hata hivyo sio kila fundi au mjenzi ana uwezo wa kufanya “setting out” ya jengo kwa usahihi na hasa katika kuona uelekeo sahihi unaofaa kwenye mazingira ambayo kiwanja kinachojengwa hakijakaa katika mpangilio ambao tayari umeshakubalika.
Hivyo ni muhimu sana kwa mtu yeyote mwenye mradi wake wa kujenga kuzingatia sana hatua hii ya kwanza kabisa hata kama atapuuza ushauri wa kitaalamu kwenye hatua nyingine. Hatua hii ni muhimu na kutofanyika kwa usahihi ni mwanzo wa uharibifu mkubwa wa jengo/nyumba hiyo mbeleni.
Karibu sana.
Architect Sebastian Moshi.
Whatsapp/Call +255 717 452 790.
Leave a Reply
Want to join the discussion?Feel free to contribute!