JE UNA UHAKIKA UTARIDHIKA NA RAMANI YA NYUMBA/JENGO LAKO? FANYA HIVI.

Licha ya kwamba watu wengi huwa wana vipaumbele vyao mbalimbali linapokuja suala la nyumba zao za kuishi au hata majengo yao mengine kama vile majengo ya biashara, taasisi za kijamii n.k., lakini mara kwa mara wamekuwa hawafanikishi kile hasa wanachohitaji kwa kushindwa kujipanga vizuri wanapokuwa kwenye mchakato wa kukamilisha hatua ya michoro ya ramani. Hili huweza kusababishwa na kujisahau, kusahau au kushindwa kuwasilisha vipaumbele vyao kwa mtaalamu au hata uzembe tu upande wa mtaalamu ambao unashindwa kuzingatia mambo muhimu au yaliyojadiliwa na kujisahau kwa pande zote kunakopelekea nyumba/jengo kukosa vile vitu muhimu vilivyoazimiwa, kupendekezwa au kupendwa mwanzoni.

Sasa ili kuhakikisha kwamba huji kujikuta unajutia baadaye wakati pengine jengo limeshajengwa n ani vigumu kuvunja ni vyema sana kuzingatia mambo haya. Kwanza kabisa jiridhishe na mahitaji yako yote na vipaumbele vyako vingine vyote unavyohitaji viwepo kwenye jengo lako kisha viandike chini. Orodhesha mahitaji yako yote kuanzia yale muhimu mpaka yale unayopendelea hata kama sio hitaji la msingi. Namna ya kujua kuhusu mahitaji yako na matamanio mengine ni kuanza kwa kuangalia pale ulipo sasa ni vitu gani unahisi unavikosa ambavyo ungetamani viwepo. Kisha angalau utamaduni wako na watu wako wa karibu kwa maana ya familia na wale unaishi nao kwa ujumla kisha unaweza kuona wazi kwamba unahitaji nini.

Baada ya kuandika yote unayohitaji sasa zungumza na watu wako wa karibu kwa maana ya familia na wale unaoishi nao ukihitaji maoni yao pamoja na mahitaji yao kama watumia wa jengo hilo unalokwenda kulijenga sasa. Kisha unaweza kuingia mtandaoni pia na kuendelea kuboresha yote uliyoandika kwa kuongezea kila unachoona unahitaji au kitakachoongeza thamani ya jengo lako kwa namna unayoona wewe inafaa. Baada ya kuwa na orodha ya mahitaji na vipaumbele vya kwenye jengo lako ndio sasa unaweza kumwita mtaalamu ukamshirikisha mkajadiliana naye akaongeza au kupunguza mahitaji hayo kadiri ya ushauri wa kitaalamu atakaotoa na kufikia hitimisho la pamoja.

Kitakachofuata sasa baada ya kukubaliana upande wa mahitaji na mtaalamu kabla hajaenda kuanza kazi unapitia yote mliyojadili na kuazimia na kuyaweka kwenye maandishi tena inakuwa ndio mwongozo wa mtaalamu kwenye utekelezaji wa ramani ya kazi husika ambapo pia inakuwa ndio rejea yenu na mtaalamu pale atakapoleta pendekeza la kwanza la michoro ya ramani ya jengo lako ambalo mtajadili kwa mwongozo ambao mliuandika siku ya makubaliano. Kutokea kwenye mwongozo mliouweka kwenye maandishi mnahakikisha kila mlichokubaliana kimezingatiwa kama vile makubaliano yenu yalivyokuwa yanataka. Mtaalamu anaweza tena kwenda kufanya maboresho baada ya kuongezea tena kwenye yale makubaliano kuendana na vile mlivyoamua kwenye mkutano wa pili wa utekelezaji wa kazi ya ramani.

Kwa vyovyote hapo kupitia kutafakari, kujadili, kushirikisha utaalamu na kujadili tena kisha kuandika mwongozo ni wazi kwamba sehemu kubwa ya mahitaji yako na vipaumbele vyako vitakuwa vimezingatiwa kuelekea kufanikisha nyumba ya ndoto yako. Hivyo ukifuata mwongozo huu utaweza kuwa na nyumba utakayoifurahia sana na itakayopa furaha na amani huku ikikuepushia usumbufu na mivutano na mamlaka zinazosimamia ujenzi. Ikiwa unahitaji ushauri wowote juu ya hili karibu sana tukusikilize.

Karibu sana.

Architect Sebastian Moshi.

Whatsapp/Call +255 717 452 790.

0 replies

Leave a Reply

Want to join the discussion?
Feel free to contribute!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *