NAMNA UTARATIBU WA MALIPO UNAVYOATHIRI UBORA WA RAMANI YA JENGO.

Wote tunajua kwamba kazi yoyote ya kitaalamu au inayoongeza thamani kubwa kwenye kitu huwa ina gharama na ile gharama inayolipiwa ndio inaweka nia kwa mtaalamu kuweka muda wake na umakini wake mkubwa sambamba na utaalamu wake kuweza kutengeneza thamani inayokusudiwa. Hivyo msukumo wa ndani wa mtu kufanya kazi na hasa kufanya kazi nzuri kunasababishwa na yale manufaa ambayo mtu huyo anayapata ambapo anaongeza thamani kubwa ya kwenye eneo husika. Kwenye kutengeneza ramani ya ujenzi pia eneo hili ni muhimu sana kuzingatiwa ili kupata matokeo bora sana ya thamani iliyoongezwa katika mradi husika.

Sasa leo tunakwenda kuona namna utaratibu wa malipo unaweza kusaidia kuongeza au kuchangia kushuka kwa thamani ya ramani ya jengo na hatimaye jengo lenyewe.

Kwanza kabisa anza na kutafuta mtaalamu mwenye uwezo mkubwa katika taaluma ya usanifu majengo katika eneo la ramani kuanzia ubunifu wa majengo mpaka sanaa ya uchoraji. Hakikisha mtu huyo sio tu kwamba ana uwezo lakini pia awe ni mtu rahisi kudili naye na muungwana mwenye kujali zaidi na kufikiria maslahi yako kuliko tamaa zake binafsi. Sasa baada ya kuwa mmeshajadili vizuri na kwa kina kuhusu mahitaji yako na yeye kwenda kufanya kazi hiyo inapaswa alipwe malipo ya awali ya kazi ya usanifu wa jengo. Malipo hayo yatamfanya aone kwamba mradi huo ni mradi uliodhamiriwa kweli kujengwa na kwamba juhudi zake haziendi bure hivyo ataweka kazi kubwa ambayo atakuwa anategemea kuiona ikiwa imejengwa. Malipo hayo yanaweza kuwa theluthi moja ya gharama malipo yote ya michoro ya ramani au yakafika hata nusu yake.

Baada ya hapo hakikisha mtaalamu huyo amepewa muda na tarehe ya kukamilisha kazi hiyo ambapo tarehe hiyo haipaswi kuwa mbali sana bali ya karibuni ili aweke mud ana umakini wake kwa wakati huo huo mliojadili ili asije kujisahau sana na kusahau uzito mliouweka kwenye baadhi ya mambo. Kwa maana hiyo kazi hiyo itafanyika katika ari kubwa huku mtaalamu mwenyewe akiwa anazingatia mengi mliojadili. Kitakachofuata baada ya hapo ni uwasilishaji wa kazi husika kwako mteja ambapo ikiwa utaipitisha atakwenda kukamalisha hatua ya muonekano. Mtajadili hatua hiyo na kisha utalipa tena hatua ya pili ya malipo huku kazi ikiwa imeshafanyika kwa angalau 70% na wakati huo huo maazimio mengi yakiwa yamefanyika kama ilivyopangwa.

Namna hii ya malipo inamfanya mtu afanye kazi kwa ubora na usahihi kwa sababu anajua kwamba kutakuwa na mjadala ambao endapo hatutapitisha kazi yake basi malipo hayatafanyika lakini pia na kwa upande wa mteja ni kwamba mtaalamu akiona malipo hayafanyiki au yanasuasua anahisi kwamba mradi hauna uzito na labda hautajengwa hivyo anakuwa haweki bidii kubwa na ubunifu kwenye kitu ambacho hana uhakika kama kuna dhamira kweli ya kwamba kinajengwa. Kisha mwishoni baada ya kukamilisha michoro ya mwisho na kutoa nakala ndipo malipo ya mwisho yanafanyika.

Kwa utaratibu huo pande zote mbili zinakuwa zimenufaika na kila uzembe wa upande wowote unakuwa unawajibika kwa namna ambayo itaweka uzito na msukumo wa kufanikisha yale yanayokusudiwa kwa ubora na usahihi uliopangwa. Ikiwa utahitaji ushauri zaidi au huduma yoyote inayohusiana na haya tunayosema usisite kuwasiliana na sisi muda wowote utakaokuwa tayari.

Karibu sana.

Architect Sebastian Moshi.

Whatsapp/Call +255 717 452 790.  

0 replies

Leave a Reply

Want to join the discussion?
Feel free to contribute!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *