KUJUA BEI YA RAMANI YA NYUMBA/JENGO KWENYE UJENZI.
Katika dunia ya sasa ambapo soko huria limeendelea kushika kasi sana baada ya mifumo karibu yote ya kiuchumi duniani ikijikuta inaangukia kwenye mfumo wa kibepari au uchumi wa soko huria, gharama ya vitu vingi tumeona ikiendelea kuamuliwa na soko badala ya kupangwa kama ilivyokuwa inafanywa na baadhi ya serikali hapo zamani. Hili limepelekea pia watu wengi kujikuta kwenye utata wa bei sahihi ya vitu mbalimbali ambavyo hawajavizoea na hawana mazoea ya kuvinunua au kusikia vikinunuliwa mara kwa mara hususan bei za huduma mbalimbali, hasa zile huduma kubwa kubwa ambazo hufanyika mara chache katika maisha ya mtu binafsi.
Moja kati ya huduma hizo ambazo bei zake huwa ni utata ni pamoja na huduma za ujenzi kwa ujumla kuanzia ushauri wa kitaalamu na michoro ya ramani mpaka huduma za ufundi na ukandarasi kwa ujumla. Mara nyingi kwenye eneo hili bei kuamuliwa na nguvu ya soko sio kitu kinachoonekana moja kwa moja kiurahisi kwa sababu kwanza ni huduma na pili ni huduma ambayo bado ni ngeni sana kwenye mazingira yetu. Kwa watu wengi wanapoambiwa bei ambayo ni wastani huona kwamba ni bei kubwa sana kwa sababu ya uelewa mdogo sana walionao juu ya namna kazi hiyo inavyofanyika, umuhimu wake, thamani yake na manufaa yanayotokana na utaalamu husika.
Hivyo sasa watu wamekuwa wakibaki njia panda kuhusu ni ipi sasa bei sahihi au ni namna gani mtu unaweza kujua kwamba umelipia bei sahihi kwa michoro husika ya ramani. Ukweli ni kwamba kama jinsi lilivyo hili ni soko huria hakuna bei sahihi ya moja kwa moja kati huduma hizi za ujenzi iliyopangwa au ambayo inakubalika japo mamlaka zinazohusika kupanga viwango vya gharama za ujenzi huwa vinaweka wastani wa bei hizo. Gharama hizo zinazopangwa na bodi mbalimbali za taaluma mbalimbali za ujenzi huwa zinasaidia zaidi au kuwarahisishia wao namna za malipo na namna za kutoza gharama za ada mbalimbali na malipo mengine ya kitaalamu lakini huwa hazitumiki sana mtaani kwani kwa kawaida huwa ni gharama kubwa sana.
Hivyo kwa mtaani bei huishia kuwa ni maelewano tu na mara nyingi hutegemea pia na ubora wa mtaalamu mwenyewe ambapo uwiano wa bei hiyo huendana zaidi na ukubwa wa mradi husika. Kwa maana hiyo sasa mpaka hapo unaweza kuona bei ni maelewano zaidi kuliko mipango mingine yoyote. Lakini sasa ikiwa unataka kupata wastani mzuri ili ufanye maamuzi ambayo hutajutia au maamuzi ambayo hayajakuumiza wewe wala hayajamuumiza mtaalamu wako basi ni vyema kupimisha bei za gharama nyingine za huduma za ujenzi wa jengo lako na gharama za michoro ya ramani anazokwambia mtaalamu huyo. Hiyo inafanyikaje sasa.
Kwa mfano mtu unapatana bei ya michoro ya ramani ya nyumba/jengo lako kwanza unaangalia umuhimu wa huduma hiyo ya kitaalamu kwenye mradi wako, ni muhimu kiasi gani na huyo anayeitoa ana utaalamu mkubwa kiasi gani na kwa viwango gani. Baada ya hapo sasa unaangalia huduma nyingine za ujenzi kwenye hilo jengo ni kiasi gani? Kwa mfano nyumba yako ni nyumba ya vyumba vinne unaweza kuchukua simu ukampigia fundi ujenzi na kumwambia unataka kumpa kazi ya kujenga nyumba ya vyumba vinne akupe gharama zake za ufundi wa kazi ya kujenga msingi wa jengo au kazi ya kupiga jengo ripu/plasta kisha uchukue gharama hizo ulinganishe na bei anayokwambia mtaalamu wa kufanya michoro ya ramani ya jengo hilo.
Unaweza kuangalia kwamba kama hao mafundi ni watu wenye elimu fulani na wanafanya kazi ya kujenga kwa muda fulani na wanalipwa kiasi fulani cha pesa na umuhimu wa kazi yao ni mkubwa kiasi fulani basi unaweza kuona kwamba huyo mtu ambaye labda naye ana elimu fulani na uwezo na uzoefu wake kwenye kazi yake ni mkubwa kiasi fulani na kazi yake itachukua muda fulani na anadai kiasi fulani cha pesa basi yuko sawa au hayuko sawa. Ukienda na staili hiyo ya kulinganisha bei na huduma unaweza kuwa katika usahihi kiasi huku ukiwa hujamuumiza sana wala kumpendelea sana mtu yeyote. Japo kwa miradi ya taasisi za kiserikali na hata taasisi nyingine binafsi na za kimataifa huenda gharama za kitaalamu zikawa kubwa zaidi japo uwiano bado hauwezi kucheza mbali sana. Ikiwa unahitaji ushauri zaidi au huduma za ujenzi usisite kuwasiliana na sisi.
Architect Sebastian Moshi.
Whatsapp/Call +255 717 452 790.
Leave a Reply
Want to join the discussion?Feel free to contribute!