HII NDIO SABABU KUU YA GHOROFA KUANGUKA KARIAKOO.

Kabla sijaingia ndani kuanza kuchambua sababu ambazo hupelekea maghorofa kuanguka niende moja kwa moja kueleza sababu kuu ili hata wale ambao hawatasoma zaidi basi wawe wametoka na kitu kimoja kikubwa. Sababu kuu ya ghorofa kuanguka ni kukosekana kwa usimamizi makini wa wataalamu au maelekezo yao kupuuzwa bila ya wao wenyewe kujua kama yalipuuzwa endapo hakusubiri kuthibitisha utekelezwaji wake.

Katika hali ya kawaida huwa ni vigumu sana kwa jengo lolote lile la ghorofa kuanguka ikiwa kulikuwa na michoro ya uhandisi mihimili ambayo imefanyika na kupitishwa na mamlaka husika na utekelezwaji wake ukazingatiwa, ni vigumu sana. Kazi ya mamlaka za ujenzi katika ngazi zote kuanzia katika ngazi ya idara ya ujenzi kwenye halmashauri ya mji/manispaa/jiji husika mpaka kwenye ngazi ya bodi za kitaaluma ambazo ziko chini ya wizara ya ujenzi ni kuhakikisha kwamba miradi yote ya ujenzi inayopitishwa na kupewa kibali cha ujenzi imekidhi vigezo vyote vya ubora na vya kitaaluma vinavyohitajika.

Katika ngazi ya kitaaluma vigezo hivi ni vigezo rahisi sana kwani hata wanaofanya kazi hizi za kitaalamu ni watu wabobezi kabisa wanaofanya kazi hizi kila siku na wanakutana na changamoto nyingi wanazozitatua kiasi kwamba sio jambo gumu kwa kiasi ambacho wengi wanaweza kudhani mpaka kufikia kusababisha ghorofa kuanguka na kuua watu. Sababu pekee huwa ni aidha kutokuhusishwa wataalamu au mapendekezo yao kupuuzwa au kutokutekelezwa kwa sababu aidha ya uzembe, kuchakachua au wizi uliofanywa na wale waliokuwa kwenye jukumu la utekelezaji wa kazi husika.

Japo sababu ya jengo kuanguka zinaweza kuwa nyingi sana lakini kwa kesi ya majengo ambayo yana muundo rahisi wa uhandisi mihimili kama ya Kariakoo ni sababu kuu huwa ni kupuuzwa kwa wataalamu kwa sababu mbalimbali ikiwemo kukosekana kwa uelewa kwa upande wa mteja na wale waliomzunguka. Hata hivyo kwa kesi ya Kariakoo hasa ukizingatia kwamba wamiliki wengi wa majengo ya Kariakoo ni wafanyabiashara wa kawaida ambao wengi hata ule uelewa wa umuhimu wa masuala ya kitaaluma ni mdogo ni rahisi kushawishiwa kwamba wakiweza kukwepa wataalamu wataokoa fedha, bila hata kufikiria kwamba hizo fedha wanazookoa ni kiasi gani.

Hili linapekea mradi ambao ulipaswa kufanyika kwa kuhusisha wataalamu wenye weledi mkubwa wa kitaaluma na ambao maelekezo yao ndio yalipaswa kutekelezwa unafanywa na mafundi wa kawaida wasio na uwezo wala uelewa wowote wa kitaalamu hasa katika fani ya uhandisi mihimili ambao kazi yao huwa ni kutekeleza maagizo waliyopewa na wahandisi. Kwa sababu ya tamaa kwa upande wa mafundi na kukwepa gharama kwa upande wa mmiliki wa jengo basi kazi inafanyika kwa kubahatisha ambayo wakati mwingine mafundi ambao hawana msimamizi sahihi wanaongezea na wizi na ubadhirifu wa vifaa vya ujenzi unaopelekea matokeo duni yanayokuja kusababisha kuanguka kwa jengo na kusababisha hasara, maafa na kesi kwa watu wengi.

Changamoto ambayo bado ni kubwa hata kwa majengo ambayo yapo hata sasa hasa kwa maeneo yenye uholela wa ujenzi na wamiliki bahili kama Kariakoo bado kuna uwezekano majengo zaidi yasiyokidhi viwango kuanguka au kudhoofika. Hivyo kwa wamiliki wa majengo ikiwa jengo lako lilijengwa kiholela sana ni muhimu kujaribu kutafuta wataalamu wa kulichunguza na kuja na mapendekezo ya nini kufanyike ili kuliimarisha kabla halijaanguka na kuleta hasara na maafa kwa watumiaji wake.

Kwa wale ambao bado hawajajenga ni muhimu sana kuzingatia kwamba unapaswa mara zote kusikiliza na kuzingatia maelekezo ya wataalamu, na sio tu wataalamu bali wataalamu husika na sahihi. Watu wengi wa kawaida hawajui utofauti kati ya wahandisi mbalimbali na wataalamu wengine waliopo katika tasnia ya ujenzi. Kuna wahandisi wa aina tofauti tofuati na pia kuna wasimamizi wa ujenzi maarufu kama “foremen” ambao watu hudhani nao ni wahandisi na kusikiliza ushauri wao na kuutilia maanani hata kwa maeneo ambayo hawana uwezo wa kushauri.

Karibu sana kwa ushauri zaidi na usimamizi thabiti wa ujenzi unaozingatia vigezo vyote vya kitaaluma na uliopitishwa na mamlaka zote za usimamizi.

Architect Sebastian Moshi.

Whatsapp/Call +255 717 452 790.

0 replies

Leave a Reply

Want to join the discussion?
Feel free to contribute!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *