KWENYE UJENZI HUWEZI KUKWEPA GHARAMA, UTAILIPA KWA NAMNA TOFAUTI.

Hivi umewahi kununua kitu fulani kama simu au bidhaa nyingine kwa gharama nafuu kidogo kisha ukaitumia kwa kipindi fulani halafu ikaanza kuleta matatizo na kisha kuharibika moja kwa moja baada ya hapo ukaanza kufikiria kwamba kama ungenunua simu ya bei ya juu kidogo ingedumu kwa muda mrefu hata mara tano zaidi ambapo unakuwa hujapata hasara kama hela uliyotumia kwenye simu iliyoharibika haraka sana? Au umewahi kutafuta njia ya mkato ya kufanya kitu halafu kitu chenyewe kikakusumbua kiasi kwamba ukaja tu kuona kwa nini usingetumia njia ya kawaida kwani umepoteza muda fedha halafu usumbufu umekuwa ni mkubwa mpaka ukaishia kwenye kukuletea hasara?

Sasa kwenye ujenzi siku zote mambo huwa yako hivyo, yaani karibu kila gharama unayoikimbia utakuja kuilipa, tena wakati mwingine utalipa gharama kubwa zaidi kuliko hiyo au kupata hasara moja kwa moja na kulazimika kupoteza kabisa fedha yote na kuanza upya kutegemea na tatizo lenyewe ni kubwa kiasi. Siku moja ofisini tuliitiwa mradi mmoja ambao ulikuwa umejengwa na watu ambao wanaonekana walikuwa hawajui kitu chochote kuhusu ujenzi, yaani inaonekana ni mtu ambao sio tu kwamba walikosa umakini bali hajui kabisa kile anachofanya. Mradi husiku ulikuwa umeshagharimu pesa nyingi kiasi na walikuwa wanataka sasa tuurekebishe na kuendelea nao. Lakini kwa kiasi ambacho ulikuwa umeharibiwa na umefanyika vibaya ulikuwa ni mradi wa kubomoa tu na kuanza upya kabisa, wenyewe walionekana kutokuwa tayari kwa hilo lakini hakuna mtaalamu makini anayeweza kuendelea na kazi ya namna ile kwani sio tu itamsumbua na kumpoteza muda bali inaweza kumwingiza pia kwenye matatizo makubwa.

Lakini sasa ukichunguza kwa makini unagundua kwamba sababu kuu ya mradi huo wa ujenzi wa jengo hilo la ghorofa kuharibika kiasi hicho ilitokana na kujaribu kukwepa gharama kwa wahusika wa jengo kwani inaonekana hawakuhusisha kabisa wataalamu waliochora wakati wa kujenga na pengine hata ramani yenyewe waliokoteza au mchora ramani hakufika kabisa katika eneo husika kabla hajachora licha ya kwamba ni eneo lenye mwinuko. Lakini haikuishia hapo tu bali hata fundi aliyepewa kazi ya kujenga inaonekana pengine sio fundi kabisa bali ni mtu tu aliyewahadaa kwamba anaweza kuwajengea jengo hilo kwa gharama ndogo sana ili apewe kazi apate pesa ya haraka lakini hajui chochote au aliweka watu wasiojua chochote na pengine hata aliiba sana vifaa vya ujenzi kwenye mradi husika.

Sasa fikiria mtu umeshafanya kazi kubwa kiasi hicho na kuweka pesa namna hiyo ukifikiri unakwepa gharama lakini mwisho unakuja kutakiwa kubomoa kabisa jengo lenyewe. Lakini tukiachana na mfano huo hai kabisa wa uzembe uliopindukia bado kuna hasara nyingi aidha za ujenzi kuwa chini ya kiwango, au umaliziaji mbovu, wizi uzembe na mengine mengi ambayo ni gharama inayolipwa kuwa kutotaka kuzingatia ubora katika kazi zako.

Kukwepa gharama siku zote ni kuilipa kwa njia tofauti, unapaswa kuwa mtu makini sana na mwenye uelewa mkubwa sana kwenye ujenzi kuweza kukwepa gharama kwa usalama, lakini ni nadra sana kufanikisha hilo katika hali yenye usalama na sahihi kabisa. Ni muhimu kuzingatia kwamba ili kazi yako ifanyike kwa viwango ambavyo vitakupa kuridhika na kufurahi lazima pia uingie gharama fulani ambazo ni muhimu kufanikisha kile haswa ambacho unakihitaji lakini huna uhakika utakipata kwa njia gani.

Karibu sana kwa huduma bora.

Architect Sebastian Moshi.

Whatsapp/Call +255717452790.

0 replies

Leave a Reply

Want to join the discussion?
Feel free to contribute!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *