KWENYE UJENZI UADILIFU BINAFSI NA MAADILI YA KAZI YA MJENZI/MKANDARASI MWENYEWE NDIO MUHIMU ZAIDI.
Changamoto zinazotokana na miradi ya ujenzi ni nyingi sana hususan miradi ambayo inafanyika bila kufuata taratibu zote za kitaalamu ambazo zimewekwa kwa lengo la kuhakikisha kwamba mradi unafanyika kwa mafanikio na kupunguza sana hatari ya kupata hasara, mradi kushindwa kumalizika kwa wakati, kazi kuwa ya viwango duni au uzembe unaoweza kupelekea uharibifu na usumbufu. Uhalisia huu umekuwa ukisababisha watu kuchukua tahadhari mbalimbali za kukabiliana nao kwa namna tofauti tofauti na mbinu tofauti tofauti ambazo zinalenga kuhakikisha mambo yanafanyika kwa namna sahihi zaidi kwa manufaa ya mmiliki.
Hata hivyo kwenye miradi ya ujenzi kuna mambo mengi sana ambayo mengine yamekaa kimitego na kitaalamu sana kuweza kugundua kama yanaweza kutumika katika kuhujumu mradi kwa namna moja au nyingine. Wamiliki wengi wanaojenga majengo yao mara nyingi sana huwa wanaibiwa kwa namna ambazo hawagundui kabisa na hata mara nyingi kuendelea kumwamini kabisa yule aliyewaibia kwa sababu wanaamini amewafanyia kazi nzuri ambayo imemalizika vizuri. Lakini katika uhalisia kuna michezo mingi sana wamechezewa hapo katikati bila kugundua chochote lakini hawajui na kwa sababu hawapo kwenye fani hii ya ujenzi wanaweza wasigundua kabisa. Hata wale ambao wanafikiri wanafahamu bado kuna namna nyingi sana ambazo huwa zinatumika kuwahadaa bila wao kugundua chochote.
Hivyo mbinu pekee ya kukabiliana na changamoto karibu zote za kwenye ujenzi ni kujihusisha na wataaamu waadilifu na wanaozingatia na kusimamia maadili ya kazi. Ikiwa mtu unayejihusisha naye ni mtu makini, mwenye kujali na anayesimama kwenye viwango sahihi vya uadilifu wa kazi yake na anayejali kuhusu kazi yake na kesho yake basi kuna nafasi kubwa sana ya kazi kufanyika kwa namna ambayo ungetamani ifanyike ikiwa nawe ni mtu mwelewa na unayethamini kazi bora na iliyofanyika kwa uadilifu wa hali ya juu. Hili suala la uadilifu linaambatana pia na roho ya ubinadamu na utamaduni binafsi wa mtu husika.
Hivyo ni muhimu sana mtu unapoangalia namna sahihi na kwenda na mradi wako wa ujenzi kwanza kabisa ni kuwahusisha watu ambao wana kiwango kikubwa cha uadilifu na maadili thabiti sana ya kazi kwani hivyo ndivyo namna ambavyo utajiepusha na matatizo mengi makubwa na yakakayokuumiza na kukuvunja sana moyo ikiwa utakutana na watu wasio waadilifu. Hii ni kwa sababu kazi yako nzima unayotaka kuifanya tayari ni kazi ambayo watu wengine wenye uzoefu ipo kichwani kwao na wao kama washauri wako wataamua kukupeleka njia sahihi au njia isiyo sahihi kwa maslahi yako, ya kwao au ya wote kutegemea na machaguo watakayofanya. Watu wasio waadilifu ni lazima watakupoteza na kupotezwa huko utakuja kugundua ukiwa umeshachelewa sana kitu ambacho kitakuletea maumivu na majuto makuu.
Ni muhimu sana kuzingatia hili suala la uadilifu wa wale unaokwenda kuwapa kazi au kuwategemea kitaalamu kabla ya vigezo vingine vyote kwani ndipo ambapo hapo watu wengi huwa wanafeli halafu wanaishia kuumia na kuona kama wana mikosi au kupoteza kabisa imani na watu wote. Ukijihusisha na watu waadilifu mwisho wa siku utakuja kuishia kuwa mwenye furaha zaidi japo mwanzoni wanaweza wasionekane kama ni watu wenye kuvutia sana kufanya nao kazi pengine kwa sababu ya misimamo yao.
Karibu sana kwetu.
Architect Sebastian Moshi.
Whatsapp/Call +255717452790.
Leave a Reply
Want to join the discussion?Feel free to contribute!