Mambo Ya Kuzingatia Kufanikisha Mradi wa Ujenzi kwa Usahihi Tanzania.
Katika kuongeza thamani ya kiuchumi Tanzania tunahitaji ujenzi bora kuhakikisha kwamba watu wanapata kitu kinachoendana na thamani ya fedha wanayolipa. Katika mazingira ya Kitanzania, kuhakikisha hili kunahitaji mbinu sahihi, uhamasishaji wa mali ghafi kwa kuzingatia unafuu wa gharama na ubora halisi unaendana na utamaduni wetu kwa kuzingatia pia kuzingatia hali ya hewa ya eneo husika.

1. Kufanya Utafiti na uchunguzi wa mambo kadhaa.
Kabla ya kuanza ujenzi, ni muhimu kufanya utafiti Pamoja na uchunguzi juu ya mambo kadhaa yanayohusika na kuathirika kwa ujenzi, hususan kwa mradi husika. Utafiti huu unahusisha mambo kama:
- Aina ya udongo: Udongo wa eneo husika unaweza kuathiri uimara wa msingi wa jengo. Kwa mfano, udongo wa mfinyanzi unaopatikana maeneo mbalimbali ikiwemo hasa maeneo ya mkoa wa Pwani, msingi imara wa jengo unahitajika ili kuepuka kupasuka kwa kuta baada ya muda kunaotakana na kuchanwa na udongo huu unaolowa kipindi cha mvua na kukakamaa kipindi cha kiangazi au jua kali.
- Uwepo wa maji na Barabara inayofikika kwa uhakika katika eneo husika: Ni muhimu kujua chanzo cha maji safi na njia bora za usambazaji wa maji kwenye mradi huo wa ujenzi.
2. Kuchagua vifaa sahihi vya ujenzi.
- Kudumu kwa muda mrefu: Kuna vifaa vingi vya ujenzi ambavyo havina ubora na vingine ni feki kabisa hasa malighafi yanayotumika katika boma au katika hatua ya fremu ya jengo kama vile yanayohusisha saruji au mchanganyiko wa malighafi ambao unakosa uwiano sahihi. Ubora wa vifaa kwa ujumla huwa ni changamoto sana kwenye mradi wa ujenzi kwa ujumla wake.
- Kuzingatia hali ya hewa: Kuna maeneo yenye joto sana au baridi sana ambapo kunahitajika umakini wa machaguo mbalimbali, kwa mfano kwa maeneo yenye yenye joto sana au baridi sana malighafi za upauaji zinapaswa kuwa ambazo hazisababishi joto kali au baridi kali ndani ya nyumba kama vile kutumia vigae badala ya mabati kwenye upauaji n.k.,.
- Upatikanaji wa baadhi ya vifaa vya eneo husika kwa gharama nafuu: Kupata malighafi kama vile udongo sahihi, mawe au kokoto kwa gharama nafuu kwa sababu vinapatikana katika mazingira husika au usafirishaji wake sio wa kutokea mbali.

3. Kufuata Kanuni na Taratibu Zinazozingatia Viwango vya Ujenzi Zilizowekwa na Mamlaka Zinazosimamia Ujenzi Tanzania.
Ujenzi sahihi unapaswa kufuata miongozo na sheria zilizowekwa na mamlaka za ujenzi Tanzania, kama vile bodi za taaluma mbalimbali za ujenzi na halmashauri za miji/manispaa au majiji.
- Sheria za Mipango Miji na Makazi ambazo zinaeleza kanuni za ujenzi wa nyumba za makazi na biashara na vigezo na masharti yote yanayotakiwa kutumizwa ili kustahili kupata kibali halali cha ujenzi.
- Bodi za Kitaaluma kwa maana ya Wahandisi, Wasanifu, Wakadiriaji majenzi, wakandarasi, watalaamu wa mazingira Pamoja na watu wa usalama mahali pa kazi n.k.,.
- Viwango vya ujenzi (Building standards) vinavyoainisha ujenzi wa jengo kuanzia mwanzo mpaka kukamilika hatua zote kuanzia msingi, kuta, paa, mifereji ya maji, na mifumo mingine ya jengo n.k.,.
4. Misingi Imara wa jengo.
- Kuchimba msingi wenye kina sahihi kulingana na aina ya udongo wa eneo husika na asili ya eneo hilo.
- Kutumia zege bora kwenye msingi kwa kuchanganya simenti, mchanga, kokoto, na maji kwa uwiano sahihi kulingana na kiwango cha zege kilichokusudiwa katika hatua husika ya ujenzi wa msingi.
- Kuimarisha msingi kwa nondo za chuma (reinforcement bars) ili kuongeza nguvu ya jengo. Hili linafanyika na kuzingatiwa zaidi kwenye zege la maeneo ya nguzo zinazosimama wima na boriti zinazoambaa kwa mlalo na kubeba mizigo yote ya jengo kwa juu.

5. Kujenga Kuta na Paa Kwa Ubora Bila Kuchakachua.
- Kuchagua matofali bora: Matofali ya saruji au mawe ni bora zaidi kwa uimara wa muda mrefu. Lakini haya yanapaswa kuwa yametengenezwa kwa ubora pia uliohusisha mchanganyo wa uwiano sahihi wa saruji na mchanga bila kuchakachua.
- Kutumia zege yenye uwiano sahihi wa simenti na mchanga: Hii husaidia kuhakikisha kuta haziwezi kupasuka kwa urahisi kwa ndani mpaka kwenye mwonekano wa nje.
- Kuezeka kwa kutumia vifaa imara na kuepuka vifaa feki: Kama vile vigae au mabati ya kisasa yanayopunguza joto na yanayoweza kudumu kwa miaka mingi.
Mfano mzuri ni katika ujenzi wa nyumba za kisasa za makazi maeneo ya Mbweni, ambapo matumizi ya vigae vya mfinyanzi na vigae vya Harvey tiles yameongeza ufanisi wa kudhibiti joto ndani ya nyumba.
6. Mfumo Bora wa Maji na Umeme
Ili kuhakikisha nyumba inakuwa na huduma bora, ni muhimu kuwa na mifumo sahihi ya maji na umeme. Hatua muhimu ni:
- Kusakinisha mabomba ya maji kwa usahihi ili kuepuka uvujaji na upotevu wa maji Pamoja na uharibifu wa maeneo mengine ya nyumba utakaoletwa na uvujaji wa maji.
- Kuhakikisha mfumo wa umeme unafuata viwango vya kitaifa ili kuepuka hatari ya moto au hitilafu za umeme. Hili litahakikishwa kwa kutumia wataalamu waliobobea kwenye ujenzi badala ya Kwenda na mazoea ya kutumia mafundi wa kawaida wasio na uelewa mkubwa kuhusiana na mambo ya umeme.

7. Utunzaji na ukarabati wa mara kwa mara wa Jengo Baada ya Ujenzi.
Baada ya ujenzi kukamilika unapaswa kuepuka kujisahau kama baadhi ya watu waliokosa umakini, kwani matengenezo ya mara kwa mara ni muhimu ili kuhakikisha jengo linadumu kwa muda mrefu. Hatua za matengenezo ni pamoja na:
- Kupaka rangi upya mara kwa mara ili kulinda kuta dhidi ya unyevu na kupendezesha muonekano. Hili linapaswa kuzingatiwa hata kama ulipaka rangi inayoweza kuhimili hali ya hew ana kuchafuka.
- Kuziba uharibifu na nyufa ndogondogo zinazoweza kuleta uharibifu mkubwa endapo hazitatatuliwa mapema. Hili linapaswa kufanyika kila mara inapotokea kuna nyufa zimejitokeza kwa sababu yoyote ile ndani ya jengo.
- Kuhakikisha mifumo ya mitaro na mifereji ya maji iko katika hali sahihi ili kuzuia mafuriko na mmomonyoko wa udongo unaoweza kuathiri uimara wa jengo kwa ujumla. Hili linakwenda mpaka kwenye mifereji iliyopo juu ya paa inayokusanya maji ya mvua.

Hitimisho
Kufanikisha ujenzi sahihi wenye viwango kwa mazingira ya Kitanzania kunahitaji mikakati sahihi, matumizi ya malighafi na vifaa bora vya ujenzi, na kufuata viwango vya ujenzi. Kutumia teknolojia sahihi, maarifa sahihi na vifaa vinavyopatikana kwa urahisi husaidia kupunguza gharama na kuongeza uimara wa majengo.
Architect Sebastian Moshi.
Whatsapp +255717452790
Leave a Reply
Want to join the discussion?Feel free to contribute!