NAMNA SAHIHI ZA KUPUNGUZA GHARAMA ZA UJENZI
Na Architect N. Moshi
+255717452790
Habari Boss
Karibu Sana Tuelimishana Namna Sahihi Zaidi Kadhaa Za Kukusaidia Kupunguza Gharama Za Ujenzi Wa Mradi Wako
Unaweza Ku-Share(Kushirikisha) Ujumbe Huu Kwa Watu Wako Wa Karibu, Unaweza Kuwasaidia Sasa Au Wakati Mwingine Kwa Namna Moja Au Nyingine
Ahsante
Kwanza kabisa kabla hujafikiria kupunguza gharama za ujenzi unatakiwa kufahamu gharama halisi za ujenzi, tatizo ni kwamba watu wengi huwa wanataka kupunguza gharama za ujenzi wakati hawana uelewa mzuri wa gharama halisi za ujenzi zilivyo. Ni vyema ukajua kwanza nyumba/jengo fulani la ukubwa fulani na ubora fulani katika mazingira fulani linagharimu kiasi gani cha fedha mpaka kukamilika ndio ufikirie uwezekano wa kupunguza hizo gharama ili ujue umeokoa kiasi gani cha fedha katika mradi huo.
Sasa twende tuangalie mbinu mbalimbali za kupunguza gharama hizi za ujenzi;
- Namna ya kwanza na pengine sahihi zaidi ya kupunguza gharama za ujenzi ni kuwa makini na ukubwa wa jengo husika, kwa sababu ukubwa wa jengo unachangia kwa kiasi kikubwa sana ukubwa wa gharama za ujenzi wake, kwa hiyo kupunguza vile visivyo na umuhimu na kupunguza ukubwa wa functions za ndani ya jengo kama sio muhimu sana kwako ni njia ya kwanza sahihi sana. Huwa inashangaza mtu anaweza kukwambia nataka unitengenezee nyumba ndogo ya gharama nafuu ya vyumba vitano viwe vikubwa, mtu anataka nyumba ndogo ya bei nafuu lakini yenye vyumba vingi halafu viwe vikubwa. Weka vyumba ambavyo ni standard, kama ni nyumba ya kuishi unaweza kuchagua baadhi ya vyumba kama vile sebule na masterbedroom viwe vikubwa kiasi labda na jiko liwe na nafasi ya kutosha kupangilia vinavyohitajika na vyumba vingine viwe vya kawaida.
Kama ni majengo ya biashara au ofisi unaweza kupunguza “dead spaces”(maeneo yasiyotumika) kuondoa visivyo na ulazima na vingine vya namna hiyo. - Namna ya pili sahihi kupunguza gharama za ujenzi ni kutengeneza ramani halisi ya jengo lako. Ukiwa na michoro iliyofanywa kwa kuzingatia gharama unaweza kuepuka kutumia gharama zaidi kwa sababu utakuwa tayari umefanya makadirio ya ujenzi ambapo utaondoa uwezekano wa kuongezewa gharama zitakazoweza kuongezeka aidha kwa kuongeza jengo kiholela au kupunguza chochote kutokana na kukosa mwongozo au kwa wasimamizi wasiowaaminifu kudanganya kwa kuongezea chochote usichokifahamu.
- Namna ya tatu sahihi ya kupunguza gharama za ujenzi ni wataalamu wa ujenzi kufanya kazi kwa pamoja kwa ushirikiano huku wakiweka kipaumbele katika kupunguza gharama. Kwa mfano structural engineer(mhandisi mihimili) anaweza kushauriana na architect(msanifu/mbunifu majengo) namna ya kupunguza idadi ya nguzo au upana wake kwenye baadhi ya maeneo ili kuepuka kutengeneza dead spaces zitakazolazimu kutengeneza spaces zaidi kufidia hizo spaces zilizochukuliwa na nguzo, bila kuleta madhara
- Namna ya nne sahihi ya kupunguza gharama za ujenzi ni kufanya kazi na watu waaminifu. Hii itakusaidia kuepuka uwezekano wa kuibiwa au kuongezewa gharama (variations) ya kitu chochote kutokana na loopholes zinazoweza kuwepo kwenye makubaliano.
- Namna ya tano sahihi ya kupunguza gharama za ujenzi ni kuufuatilia mradi kwa makini na kuuelewa vizuri, hii itakusaidia kujua ni kitu gani cha muhimu au kisicho cha muhimu kinachoweza kuondolewa ambacho kinasababisha gharama bila sababu za msingi baada ya kuzungumza na wataalam wako na kuelewana.
- Namna ya sita sahihi ya kupunguza gharama za ujenzi ni kama una pesa yote ya mradi husika unaweza kukaa chini na wataalam wako mkapanga namna ya kusimamia ununuzi wa vifaa mkatafuta maeneo wanakouza vifaa vya ujenzi kwa bei nzuri ya jumla mkafanya manunuzi ya jumla. Jambo hili linahitaji umakini mkubwa sana kwa sababu unaweza kufika mbele ya safari katika huo ujenzi ukakuta ulichonunua hakifai au pengine kimeharibika na hakifai tena kwa sehemu iliyokusudiwa au ukawa umeamua kubadilisha baadhi ya vitu au mpangilio wa jengo lenyewe, ndio maana nasisitiza ni vyema kwanza kukaa chini na wataalam mkajadili kwa makini sana usije kujikuta unajiingiza kwenye hasara badala ya kupunguza gharama.
NOTE; Kutaka kuepuka gharama kwa kufanya ujenzi kienyeji hasa kwa miradi mikubwa kunaweza kukusababishia aidha kujikuta kwenye gharama zaidi ya zile ulizokuwa unaepuka mwanzo au kusababisha maafa kwa watu kutokana na kuchakachuliwa kupita kiasi, au jengo kudumu kwa muda mfupi na kupelekea ukarabati wa mara kwa mara unaohusisha gharama nyingi ambazo zingeweza kuepukwa mwanzoni kwa kufanya maandalizi makini
Kwa leo tuishie hapo
Ahsante na karibu sana
Please share
Leave a Reply
Want to join the discussion?Feel free to contribute!