UJENZI WA GHARAMA NAFUU KWA KUPUNGUZA UKUBWA WA JENGO

Baada ya kujua kutengeneza michoro ya ramani kisha kufanya makadirio ya ujenzi na kuona kwamba gharama za ujenzi wa mradi wako ni kubwa sana na ungependa zipungue kufikia kiwango fulani ambacho unafikiri ndicho nafuu kwako au kinachoendana na bajeti uliyopanga unaweza sasa kuanza kufikiria kupunguza ukubwa wa gharama hizo kwa kupunguza ukubwa wa ramani yako ya jengo lenyewe. Muhimu cha kukumbuka ni kwamba ukubwa gharama za mradi wa nyumba unatokana na ukubwa nyumba yenyewe.

UKUBWA WA JENGO NDIO UKUBWA WA GHARAMA ZA JENGO LENYEWE

Sasa muhimu cha kuanza nacho hapa ni kuangalia idadi ya vyumba vilivyoko ndani ya nyumba husika, hapa ndio sehemu ya kwanza ambayo unaweza kupunguza gharama za ujenzi huu kwa kiasi kikubwa ambapo unaangalia chumba kisicho na ulazima na kukipunguza. Kwa mfano katika nyumba yako ya kuishi umeweka kwamba kila mtoto atakuwa na chumba chake, sasa badala yake unapunguza idadi ya vyumba na kuweka kila jinsi kutumia chumba kimoja yaani watoto wa kiume wote watakuwa na chumba kimoja kisha watoto wa kike nao watatumia chumba kingine. Halafu labda chumba cha wageni unakiondoa ndani ya nyumba kwa sababu wageni sio watu wa kila siku basi utaondoa chumba hicho na baada ya kumaliza ujenzi wako huu unaweza kuanza ujenzi mwingine wa nyumba ya msaidizi pembeni ya nyumba kubwa maarufu kama “servant quarter” ambayo ndio mgeni akija atatumia chumba cha huko kwenye “servant quarter”. Hiyo itakusaidia kukamilisha nyumba yako muhimu kwa gharama nafuu na baadaye utaijenga nyumba ya pembeni taratibu wakati umeshahamia kwenye nyumba hii. Unaweza pia labda kuondoa nafasi nyingine zote zisizo na umuhimu mkubwa ndani ya jengo. Njia ya kupunguza vyumba na nafasi ndani ya jengo ndio njia inayosaidia kupunguza ukubwa wa jengo kwa kiasi kikubwa zaidi na kupunguza gharama za ujenzi kwa kiasi kikubwa kuliko njia nyingine yoyote.

PUNGUZA UKUBWA WA VYUMBA NDANI YA JENGO KUPUNGUZA UKUBWA WA JENGO

Njia nyingine muhimu na ya uhakika ya kupunguza gharama za ujenzi kwa kupunguza ukubwa wa jengo ni kupitia kupunguza ukubwa wa vyumba ndani ya jengo. Watu wengi hawajui kwamba ukubwa wa vyumba ndani ya jengo ndio ukubwa wa jengo lenyewe. Kadiri nyumba inavyokuwa na vyumba vikubwa ndani ya jengo ndipo kadiri inavyokuwa kubwa zaidi, huwa inashangaza kusikia mtu anasema “nataka unitengenezee ramani ya nyumba ndogo ndogo lakini nataka iwe na vyumba vikubwa”, hii ni kauli amabyo inajipinga yenyewe, ukubwa wa vyumba ndio ukubwa wa nyumba yenyewe na udogo wa vyumba ndio udogo wa nyumba yenyewe. Kwa maana hiyo sasa nashauri kwamba kukagua ukubwa wa vyumba na kuangalia namna ya kupunguza na kuvifanya vidogo zaidi lakini visiwe vidogo tena kupita kiasi, kiasi cha kuwa kero kwa watumiaji. Chumba cha kawaida cha kulala hata kiwe kidogo kiasi gani kisipungua chini ya urefu na upana wa mita tatu kwa tatu, yaani 3m x 3m hiyo ndio iwe saizi ya chini kabisa ya ukubwa wa chumba kwa sababu chini ya hapo unaenda kuwa na chumba ambacho ni kero kwa mtumiaji na ambacho ni acha ajabu. Pia sebule, jiko, dining n.k., vyote kuna viwango havitakiwi kupungua zaidi. Hivyo mtu unaweza kufanya marekebisho ya namna hiyo katika kupunguza ukubwa wa nyumba na matokeo yake kupunguza gharama za ujenzi.

VYUMBA VISIPUNGUE NA KUWA VIDOGO KIASI CHA KUGEUKA KUWA KERO KWA MTUMIAJI

Architect Sebastian Moshi.

Whatsapp/Call +255717452790.

5 replies

Leave a Reply

Want to join the discussion?
Feel free to contribute!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *