KUVUJA KWA NYUMBA ZA “CONTEMPORARY” NI KUKOSEKANA KWA UFUNDI SAHIHI.

Kumekuwa na malalamiko mengi sana juu ya kuvuja kwa nyumba za kisasa aina ya “contemporary” ambazo bati za nyumba lenyewe zinakuwa hazijatokeza kwa nje kwa sababu linafichwa na kuta za “parapet” hivyo kutegemea “gutter” ya zege katika kukusanya na kuondoa maji ya mvua juu ya paa.

Ni kweli malalamiko haya ni mengi sana na kweli nyumba nyingi zinazojengwa kwa mtindo huu zimekuwa na changamoto kubwa ya maji kuvuja kupitia “gutter” ya zege inayoyakusanya ili kuyashusha chini kupitia mabomba wima “vertical ducts”.

Suala hili la changamoto ya nyumba za aina hii kuvuja limeendelea kuonekana sana kiasi kwamba baadhi ya watu wameanza kuwa na mtazamo hasi sana juu ya aina hizi za nyumba na wengine licha ya kuzipenda sana kwa muonekano lakini wameanza kusita kuzijenga na wengine kutozihitaji kabisa.

NYUMBA YA “CONTEMPORARY” INATEGEMEA “GUTTER” YA NDANI KWA NDANI KUSHUSHA MAJI YA MVUA CHINI AMBAYO MARA NYINGI HUTENGENEZWA KWA ZEGE.

Ukweli ni kwamba kuvuja kwa nyumba hizi za “contemporary” kunasababishwa na kukosekana kwa ufundi sahihi uliobobea kwenye suala zima la kushughulika na maji yanayopita juu ya eneo lenye zege na hivyo kupelekea kutoka kwenye njia yake na kupenya kuingia ndani ya nyumba.

Kwa kawaida maji yana nguvu kubwa sana na ubishi wa hali ya juu, na siku zote yanahitaji umakini mkubwa sana kwenye kushughulika nayo hasa pale yanapokuwa yanahitajika kukwepeshwa kwenye maeneo yanayopita karibu, jambo ambalo mafundi wengi hawalifikirii katika uzito unaostahili.

“GUTTER” YA NDANI KWA NDANI AMBAYO HUSHUSHA MAJI YA MVUA CHINI NDIO MARA NYINGI HUWA CHANZO CHA MAJI HAYO KUVUJIA NDANI YA NYUMBA

Hii “gutter” ya zege ambay ndio eneo lenye udhaifu linalopelekea nyumba nyingi za “contemporary” kuonekana hazifai lina njia nyingi sana sahihi za kushughulika katika kuhakikisha maji haya yanadhibitiwa hata kwa kutumia akili ya kawaida tu, yaani hata kwa kuongezea tabaka moja tu la plastiki lililowekwa kwa usahihi na kumalizia na uso laini wa juu.

Hivyo changamoto hii ya nyumba za “contemporary” inayozifanya zionekane kuwa ni tatizo kubwa ni changamoto ndogo za kiufundi ambazo zinatatulika bila shida ikiwa utatumia mtaalamu mwenye uzoefu na ufundi sahihi. Ikiwa utahitaji wataalamu wazoefu katika hili unaweza kututafuta.

Architect Sebastian Moshi.

Whatsapp/Call +255717452790.

0 replies

Leave a Reply

Want to join the discussion?
Feel free to contribute!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *