KWENYE UJENZI USIPOJUA SEHEMU SAHIHI YA KUCHUKUA USHAURI UTAINGIA KWENYE MAJUTO.

Ikiwa mtu unahitaji kupata ushauri wa uhakika ambao utakuwa na majuto kidogo katika masuala yote yanayohusiana na ujenzi ni muhimu sana kuwa na mtaalamu mshauri wa masuala ya ujenzi ili kuepuka kuchukua ushauri kwa watu wasio sahihi ambao utakufanya ufanye maamuzi yatakayokuja kukugharimu sana baadaye. Kila mtu anajua umuhimu wa utaalamu katika fani yoyote ile ndio maana mtu ukiumwa unaambiwa uende ukamuone daktari, ukiwa na masuala yanayokusumbua kuhusiana na watu au taasisi utaambiwa utafute mwanasheria, ukiwa unasumbuliwa na mamlaka za kodi au taarifa nyingine za kifedha utaambiwa utafute mhasibu na hivyo hivyo kwenye ujenzi ndivyo unavyopaswa kufanya.

Katika shughuli zetu za ujenzi na ukaguzi wa miradi ya ujenzi kila tunapotembelea maeneo ya ujenzi ambayo hakuna mwongozo kitaalamu huwa tunakutana na changamoto nyingi na kubwa na haswa ikiwa mradi haukuwa na mtaalamu kabisa kuanzia kwenye hatua ya michoro. Uharibifu ambao huwa unakuta unakuta umefanyika kwa sababu ya maamuzi yasiyo sahihi yaliyofanyika kienyeji bila kufuata kanuni za kitaalamu huwa ni mkubwa sana na mara nyingi aidha huhusisha gharama kubwa sana kufanya marekebisho au hupunguza sana thamani ya jengo pale marekebisho yanapokosa kufanyika.

Hivyo kwa mtu yeyote mwenye mipango yoyote ya kuja kufanya ujenzi katika maisha yake anapaswa kuwa na mtaalamu wa karibu ambaye ndiye atakuwa anamsaidia kumshauri na kumwelekeza mambo mengi muhimu kwenye jambo lolote linalohusiana na ujenzi. Hilo litasaidia kumwepusha na maamuzi mabovu katika kila hatua ya ujenzi anayotaka kuiendea tangu mwanzoni kabisa mpaka mwisho wa maisha ya jengo lenyewe. Hata hivyo mshauri huyo anapaswa kuwa ni mtu mwenye uelewa mpana kuhusu ujenzi, mwenye uzoefu na mwenye rekodi ya uaminifu na uadilifu wa hali ya juu sana.

Uadilifu na uaminifu ni sifa muhimu sana kwa mtu mshauri kwani anapaswa kuwa anasimamia maslahi ya anayemshauri kwa viwango vya juu sana badala ya kumpotosha na kumpoteza kwa maslahi yake binafsi. Mwisho wa siku mtaalamu huyo atakuwa ametoa msaada mkubwa sana kwa mjenzi huyo mtarajiwa kuliko vile ambavyo angefanya kwa kukutana tu wakati wa uhitaji na kuachana muda mfupi baada ya kukamilisha ile huduma aliyokuwa anaitoa.

Karibu sana

Architect Sebastian Moshi.

Whatsapp/Call +255 717 452 790.

0 replies

Leave a Reply

Want to join the discussion?
Feel free to contribute!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *