KUEPUKA USUMBUFU NA KUPOTEZA MUDA PELEKA MICHORO NA HATI VIKAKAGULIWE KABLA YA KUOMBA KIBALI.
Japo siku hizi kwenye halmashauri nyingi za miji, manispaa, majiji na hata wilaya mchakato wa kupata kibali cha ujenzi umekuwa rahisi zaidi na hata wa muda mfupi zaidi kuliko zamani lakini bado kuna usumbufu mwingi hujitokeza katika zoezi hilo la kuchakata kibali cha ujenzi ikiwa kuna mambo hayajazingatiwa. Makosa yanaweza kuwepo kuanzia kwenye matumizi ya kiwanja ambayo yanaweza kupelekea kulazimisha kubadili matumizi au hata kwenye mpangilio wa michoro ambao ndio unaamua hayo ni matumizi ya aina gani.
Sasa ili kufanya maamuzi sahihi kwenye jambo hili na hasa ikiwa una haraka na una wasiwasi kwamba mchakato wa kupata kibali cha ujenzi unaweza kukutana na changamoto ni vyema na muhimu ukachukua hati ya eneo lako sambamba na skechi ya michoro au wazo tu la kile unachotaka kujenga na kwenda navyo halmashauri husika ya manispaa, mji, jiji au wilaya. Ukifika pale halmashauri na kwenda kwenye idara ya ujenzi watakwambia kama kwa matumizi yaliyopo kwenye hati na aina ya jengo unalotaka kujenga utaweza kufanikisha kupata kibali cha ujenzi na kama kutakuwa na changamoto basi ni nini cha kufanya kuweza kufanikisha.
Mara nyingi watu wamekuwa wanaenda kuomba kibali moja kwa moja na kukutana na mkwamo ambao unawapotezea muda mwingi na hata gharama zaidi kwa sababu tu hawakutafuta kwanza kujua mambo ambayo yanaweza kuwaletea usumbufu. Habari njema ni kwamba ikiwa utaenda kufahamu kwanza kama unaweza kupata kibali cha ujenzi hata kama umebeba hati ya kiwanja peke yake unaweza kupewa ushauri wa namna rahisi ya kupata kibali cha ujenzi kisichohusisha mlolongo mrefu wa mabadiliko ya matumizi kwa kuwa na michoro iliyopangiliwa vizuri na kwa usahihi kuendana na matumizi ya eneo ambayo yameelezwa kwenye hati ya kiwanja.
Kwa maana hiyo ni muhimu sana aidha wewe au mtaalamu wako wa usanifu majengo akapeleka nyaraka hizo kwenye halmashauri ya mji husika kwanza kisha ndio mkaendelea na zoezi la kutengeneza michoro ya ramani ambayo mna uhakika itakubalika kwenye halmashauri pale mtakapoenda kuomba rasmi kibali cha ujenzi baada ya kukamilisha michoro yote. Hii itakusaidia pia hata kuepuka kuingia gharama mara mbili kufanya michoro ya ramani mbili tofauti ili kuendana na kile ambacho matumizi ya kiwanja yanahitaji. Ikiwa unahitaji ushauri zaidi katika eneo hili karibu tuwasiliane.
Karibu sana.
Architect Sebastian Moshi.
Whatsapp/Call +255 717 452 790.
Leave a Reply
Want to join the discussion?Feel free to contribute!