WAMILIKI WA MAJENGO KARIAKOO WACHUNGUZE MAJENGO YAO.
Wataalamu wengi wa hapa Tanzania hasa wale wataalamu makini na wanaojali kuhusu sifa zao na sifa za makampuni yao kwa maana ya wasanifu majengo, wahandisi mihimili wa majengo, wakadiriaji majenzi wa majengo pamoja na baadhi ya wataalamu wengine, wanapoitiwa mradi unaoenda kujengwa Kariakoo huwa wanaikataa au kuiagizia kwa watu wengine wasiojua au kujali sana kuhusu hali halisi ya Kariakoo. Sababu kuu ya wataalamu hawa wa majengo kufanya hivi ni aina ya wamiliki au wateja wa majengo haya yanayojengwa Kariakoo au tunaweza kusema ni asili, tabia au haiba ya wafanyabiashara wa Kariakoo kwa ujumla.
Sehemu kubwa ya wafanyabiashara wa Kariakoo namna wanavyofikiri, kuamini na kufanya mambo yao ni namna ya kienyeji sana ambayo mara nyingi inawaletea faida kwa namna wanavyofanya. Mitazamo na imani hizo ndizo zimewaletea mafanikio katika maeneo mengine ya biashara na hivyo ni vigumu kuwashawishi kufanya kazi zao nyingine kwa namna ya tofauti na hivyo. Katika hali ya kawaida ni vigumu sana kumshawishi mtu aliyefanikiwa kwa kupitia njia fulani eti aiache atumie njia nyingine ambayo anaona inampunguzia faida na wakati huo huo anaona haina madhara yoyote ambayo anaaminishwa kwamba yanaweza kutokea, ni vigumu sana.
Sasa hali hii ndio inayoendelea Kariakoo, kinachotokea baada ya hapo sasa ni kwamba wale wataalamu bora na ambao huwa wanasimamia kanuni sahihi za kitaalamu na baadhi wengine hata gharama zao ni kubwa kidogo huwa wanaikataa miradi ya Kariakoo kwa sababu wanajua ni miradi ambayo kwanza mara nyingi ina usumbufu kwenye malipo lakini hofu zaidi ni kazi kulazimishwa kufanyika chini ya viwango ili kuokoa gharama lakini yanapokuja kutokea matatizo wao ndio wataingia matatani. Jengo linapoanguka mtu wa kwanza kukamatwa huwa ni mmiliki kisha mmiliki anarudisha mpira kwa wale wataalamu waliohusika hata kama yeye mwenyewe mmiliki kuna mambo aliyalazimisha kinyume na ushauri au mapendekezo ya mtaalamu bado mtaalamu ndiye atakayewajibika.
Sasa jengo lililoanguka ni hilo moja lakini kuna majengo mengi dhaifu katika ukanda huo wa Kariakoo ambayo yanafanyika bila kuzingatia utaalamu pamoja na uzembe na kukosekana kwa ufuatiliaji makini wakati wa ujenzi. Ni kweli kwamba wakati mwingine mtu unashirikisha wataalamu vizuri kabisa wakati wa kutengeneza michoro ya ramani lakini wakati sasa ujenzi unapoanza mtu anachukua watu ambao ameaminishwa kwamba ni wasimamizi sahihi wa mradi wa ujenzi lakini kiuhalisia sio wataalamu na mbaya zaidi unakuta watu wenyewe ni wezi au wanafanya udanganyifu na kuchakachua kiasi kwamba jengo husika linakuwa dhaifu kimihimili na linakuwa linasubiri tu wakati ufike kabla uhalisia wake haujawaumbua.
Changamoto zaidi ni kwamba hakuna anayejua kama jengo husika limefanyika kwa uimara sahihi unaotakiwa au halikufanyika kwa sababu hakukuwa na mtaalamu anayefuatilia au kusimamia michoro ifuatwe kama ilivyofanyika. Hivyo natoa rai kwa wamiliki wa majengo Kariakoo hasa wale ambao hawana uhakika na namna ujenzi ulivyofanyika au wanajua kabisa walitumia watu wa kawaida na kukwepa wataalamu, ni muda muafaka sasa watafute wataalamu wa kuchunguza majengo yao kama yalifanyika kwa kiwango kinachotakiwa na kama kwa matumizi ya sasa jengo hilo litakuwa na uimara sahihi wa kuendelea kumudu mzigo unaobebwa na jengo kuanzia mzigo unahamishika mpaka ule usiohamishika.
Hili ni muhimu sana kwa sababu jengo litakapoanguka sio tu kwamba utapata hasara kubwa ya kukosa mapato na kupoteza mali yako bali pia itapelekea watu wengi kuingia matatani ikiwemo wewe mwenyewe huku ukiwa pia umesababisha watu kupoteza maisha na wengine kupoteza ndugu zao. Jambo hili litakupotezea utulivu wako na kukuyumbisha sana pengine kwa muda mrefu na pengine hata ukafungwa kabisa na kupoteza muda wako ikiwa kwamba uzembe ulikuwa upande wako. Tahadhari kabla ya hatari ni muhimu na kuishi kwa amani na utulivu baada ya kuweka jengo lako sawa na kuendelea kulitumia kwa usahihi ni muhimu sana.
Ikiwa utahitaji huduma ya uchunguzi wa jengo lako na hata marekebisho au maboresho yatakayoendana na matumizi yaliyopo kwa sasa unaweza kuwasiliana nasi.
Karibu sana.
Architect Sebastian Moshi.
Whatsapp/Call +255 717 452 790.
Leave a Reply
Want to join the discussion?Feel free to contribute!