WAMILIKI WA MAJENGO KARIAKOO MNAMSIKILIZA NANI?
Imekuwa ni hali ya kawaida pale mtu anapotaka kujenga kwanza huwa anaanza na kujaribu kushirikisha wale watu wa karibu wanaomzunguka kupata mawazo na maoni yao juu ya kile anachokwenda kufanya. Mara nyingi huwa ni marafiki wa karibu na hasa wale ambao tayari wana uzoefu binafsi katika miradi ya ujenzi kama huo anaoenda kufanya. Lakini pia watu wengine ambao huwa anawashirikisha ni wale wadau wa kwenye ujenzi kama vile mafundi au watu wengine wowote ambao anawafahamu wanaojishughulisha na masuala ya ujenzi.
Sasa hawa moja kwa moja ndio huwa wanampa ushauri wa masuala ya ujenzi na kumsisitiza sana juu ya kile ambacho ni sahihi kwake kufanya na kwa kuwa ni watu wa karibu ambao anawaamini basi moja kwa moja anazingatia ushauri wao. Changamoto iliyopo ni kwamba yeye mwenyewe hajui ni kwa kiasi gani watu hawa wana uelewa wa maeneo yote ya ujenzi na ujenzi wenyewe umegawanyika kiasi gani. Ni jambo linaloweza kukushangaza kwamba hata mafundi unaowaona wakijenga katika maeneo mbalimbali ya ujenzi wengi hawaelewi undani wa taaluma za ujenzi na namna zilivyogawanyika katika vitengo mbalimbali kwenye jengo.
Ukweli ni kwamba kuna watu wengi sana ambao wanajishughulisha na ujenzi katika ngazi ya ufundi au hata usimamizi wa kazi maarufu kama “foremen” lakini hawaelewi hata undani wa taaluma hizi zinazohusika kwenye ujenzi hususan uhandisi na usanifu wa jengo na badala yake wao wanapokea tu maagizo na kuyatekeleza kadiri walivyoagizwa. Wewe ukiangalia kwa nje unaweza usielewe kabisa na hata wao kuna vingi hawaelewi badala yake wanaoelewa sasa kwa undani na kujua nani ni nani na anafanya nini na chenye madhara kiasi gani ni wale wataalamu wenyewe ambao ni wasanifu wa jengo, wahandisi mihimili na wakadiriaji majenzi pamoja na wengine wadogo wadogo kama vile wahandisi wa umeme n.k.,.
Kwa maana hiyo ushauri wowote unaopokea kutoka kwa watu waliokuzunguka isipokuwa tu kama wapo katika fani hizo kuu za ujenzi basi ni rahisi kuwa ushauri unaokupotosha zaidi kuliko kukusaidia au ni ushauri ambao haujakamilika. Watu wengi hupenda kumwambia mtu kile kitu anachopenda kukisikia zaidi kuliko kumweleza uhalisia wa jambo aidha kwa kutaka kumfurahisha au kwa kuingiza maslahi yake hivyo pengine sio busara sana kutegemea watu wa karibu pekee.
Rai yangu sasa katika hili ni kwamba sio mbaya kuwasikiliza watu wa karibu wanachoweza kukuambia au kukushauri kwa sababu hao pia ndio watu wanaokufahamu vizuri zaidi na kile unachokwenda kufanya. Lakini usichukue ushauri wao moja kwa moja bali wasikilize kwa makini kisha tafuta mtaalamu kamili ambaye ni aidha msanifu majengo au hata mhandisi mihimili na kufanya naye mazungumzo ya kina na kuuliza maswali mengi iwezekanavyo ambapo unaweza pia kulinganisha na kile ulichoelezwa au kushauriwa na watu wako wa karibu kabla hujaingia kufanya maamuzi. Ni vyema na muhimu sana mtalaamu huyo awe na uzoefu wa miaka angalau mitano katika kazi au awe tayari ameshajishughulisha na miradi kadhaa.
Kwa kufanya hivi na kuzingatia vizuri ushauri wa wataalamu unaweza kupunguza makosa mengi sana kwenye ujenzi wako na mwisho ukafanya kazi bora sana yenye ufanisi na itakayokuongezea hata faida kibiashara kuliko kufanya mambo kienyeji ambapo unaweza kuishia kwenye maafa makubwa kama hayo yaliyotokea. Watu wa Kariakoo tunawasisitiza sana kwa sababu tunajua wengi sio watu wanaopenda sana kufuata taratibu za ujenzi wakidhani kwa kufanya hivyo wanaokoa gharama lakini mwishoni huishia kwenye hasara na majuto kwani matatizo ambayo huambatana na kufanya kazi kiholela huwa ni mengi sana na sio tu haya ya jengo kuanguka pekee.
Karibu kwa ushauri na huduma.
Architect Sebastian Moshi.
Whatsapp/Call +255717452790.
Leave a Reply
Want to join the discussion?Feel free to contribute!