WAMILIKI WA MAJENGO KARIAKOO MSISUBIRI SERIKALI KAGUENI MAJENGO YENU WENYEWE.
Wakati tunaendelea na maombolezo ya maafa ya kuanguka kwa jengo la ghorofa nne katika mtaa wa mchikichini Kariakoo na kupelekea vifo vya watu ambao idadi yao inasemekana kufikia 13 mpaka sasa huku majeruhi wengi wakiendelea kutibiwa katika hospitali ya taifa ya Muhimbili serikali imeshaunda kamati ya kufanya uchunguzi wa majengo yote ya Kariakoo. Katika hali ya kawaida ni hatua nzuri ambayo serikali imechukua na hata inapaswa kupongezwa angalau kwa kuonyesha kujali juu ya hili lililotokea sambamba na kuhitaji matokeo ya utafiti kuweza kujua ni kwa kiasi gani hali ni mbaya na hivyo kufanya maamuzi sahihi ya nini kifanyike.
Hata hivyo sambamba na hatua hiyo nzuri ya serikali bado naendelea kusisitiza kwamba kila mmiliki wa jengo Kariakoo anapaswa kufanya uchunguzi wa jengo lake ili kujua lipo katika hali gani na afanye nini sasa ili kujinusuru na hatari pamoja na hasara zinazoweza kuletwa na maafa ya jengo hilo. Hatutegemei kwamba kuna mmiliki wa jengo Kariakoo anayesubiria ripoti ya serikali ndio imwambie kama jengo lake liko katika ubora sahihi au linahitaji maboresho ili kulirudisha katika viwango sahihi vya ubora vinavyohitajika.
Katika hali ya kawaida tunaona wazi kwamba hata kamati yenyewe iliyoteuliwa ni ndogo sana kulinganisha na kazi kubwa ya kukagua majengo mengi sana yanayotakiwa kukaguliwa. Japo wanaweza kuongoza timu kubwa za kuyakagua majengo yote kutegemea na bajeti watakayopewa lakini bado wewe huna uhakika kama wakimaliza ukaguzi huo watakupa taarifa za usalama wa jengo lako. Na hata ikitokea kweli wamekagua yote kwa kina na kukupa taarifa bado hutakuwa na uhuru wa kuwapangia wapi hawajakagua wakague. Haya yote yatategemeana na ukubwa wa kazi yao wanayoenda kuifanya ambayo hata hivyo bado haijawa wazi wanaifanya kwa namna gani kwa sababu timu yao pekee mpaka sasa ni ndogo sana ikiwa hawatakuwa na timu mbalimbali chini yao.
Hivyo bado msisitizo uko pale pale, kwa manufaa yako binafsi na uhakika wa taarifa zako binafsi kwa matumizi yako binafsi ni muhimu sana kufanya ukaguzi huo wa jengo lako binafsi ili kupata taarifa na kuendelea na maboresho yako binafsi kwani changamoto itakapojitokeza itakuwa yote juu yako. Lakini pia uchunguzi wa uimara wa jengo ni jambo moja kuna changamoto nyingine nyingi ndani ya jengo kama vile kuvuja kwa jengo, mpangilio usio sahihi wa vyumba na maeneo mengine ya matumizi pamoja, mwanga , hewa n.k., ambavyo vinaweza kuboreshwa baada ya uchunguzi na kufanya jengo lako kuwa bora zaidi na linalopendwa na watu.
Ni vyema kuchukua hatua mapema zaidi kabla ya kuja tena kuuthibitisha msemo wa siku nyingi wa majuto ni mjukuu.
Karibu sana.
Architect Sebastian Moshi.
Whatsapp/Call +255717452790.
Leave a Reply
Want to join the discussion?Feel free to contribute!