KUJUA UNACHOTAKA KWENYE NYUMBA YAKO ANZA KUANGALIA UTAMADUNI WAKO WA SASA.
Imekuwa ni changamoto kwa baadhi ya watu kujua ni nini hasa wanataka linapokuja suala la nyumba yao ya kuishi kitu kinachopelekea wanakuja tena baadaye kubomoa na kuongeza baadhi ya vitu ambavyo wanafikiri wanavihitaji lakini mwanzoni hawakuvijua vizuri, ni baada ya kuanza kutumia nyumba ndio wanahisi kuna kitu muhimu kinakosekana.
Pamoja na kwamba mtu huwa na matamanio ya vitu mbalimbali ambavyo anahitaji nyumba yake iwe navyo hasa vile vitu vinavyoonekana kuvutia au kuwa na starehe lakini kabla ya kuzungumzia hayo mtu anatakiwa kwanza kuangalia utamaduni wake wa kila siku wa namna anavyoishi katika sehemu anayoishi. Anatakiwa kujua anapenda nini, huwa anafanya nini muda mwingi na ni vitu gani anahisi kuvikosa.
Kwa kuangalia pale unapoishi sasa na vitu unavyojishughulisha navyo kila siku utaanza kuona ni vitu gani na gani unahitaji ndani ya nyumba yako, kwa mfano kama huwa una kazi nyingi za kiofisi unazofanya ukiwa nyumbani ni wazi kwamba utahitaji ofisi ndogo ndani ya nyumba yako, au kama unapenda sana kusoma vitabu, kujifunza au unataka kujenga utamaduni wa watoto kusoma vitabu ni wazi kwamba utahitaji kuwa na maktaba ndogo ndani ya nyumba yako.
Kama ni mtu unapenda sana kwenda kuangalia filamu au mpira wakati nyumbani kwako watu wengi hawapendi vitu pengine utahitaji “cinema room/movie theatre”, ndani ya nyumba yako, chumba ambacho hakipitisha sauti “soundproof”, ili kuwa huru na starehe zako hizo.
Kama ni mtu wa kwenda sana kwenye ibada na kufanya mambo sana wakati watu wako sio muda wote wanahitaji vitu hivyo hali kadhalika utahitaji chumba maalum cha maombi kisichopitisha sauti “soundproof” pia. Kama wewe ni mtu ambaye huwa unatembelewa mara kwa mara na wageni wengi wengi kwa sababu zozote zile pengine utahitaji sebule kubwa kadiri utakavyoona inafaa. Kama wewe ni mtu wa kunywa sana pombe pengine utahitaji baa sebuleni au nje ya nyumba yako, na kama wewe ni mtu unayependa ukimya na utulivu utahitaji chumba chako kikao eneo ambalo ni mbali na kelele katika mpangilio wa vyumba ndani ya nyumba.
Baada ya kuweka kipaumbele kwenye utamaduni wako wa sasa na vile maisha yako yanaenda kuwa hapo mbeleni ndio sasa utahitaji kuangalia yale matamanio yako mengine ya ziada kama vile namna ungependa muonekano wa nyumba yako uwe, vitu vingine vya ziada kama vile vitu vya starehe ndani ya nyumba n.k.,
Architect Sebastian Moshi
Whatsapp/Call +255717452790
Leave a Reply
Want to join the discussion?Feel free to contribute!