KUPUNGUZA GHARAMA ZA NISHATI KAMA UMEME NA NYINGINEZO KWENYE JENGO.

Kitaalamu jengo linatakiwa kutumia gharama kidogo ya nishati kadiri itakavyowezekana kutokana na ubora na usahihi wa ramani ya jengo husika ilivyofanywa na mtaalamu kwa kuzingatia suala hilo la kupunguza gharama za matumizi ya nishati, hasa nishati ya umeme ambayo ndio imekuwa inatumika kwa kiasi kikubwa zaidi kwa nyakati tulizopo.

JENGO LINATAKIWA KUTUMIWA NISHATI KIDOGO YA UMEME KWA KADIRI ITAKAVYOWEZEKANA

Mambo muhimu ya kuzingatia kwenye utaalamu wa ramani ya jengo ambayo hupelekea kupunguza gharama za nishati katika jengo hasa nishati ya umeme.

-Kuhakikisha nyumba/jengo ina sehemu za wazi(openings) kama madirisha, vent, kuta za vioo(transparent glasses), na hata milango ya aina ya vioo yote au nusu ambavyo vinaingiza mwanga ndani kadiri ya aina ya jengo lenyewe litakavyoruhusu ambapo angalau siku nzima kabla ya giza kusiwe na eneo linalolazimu kuwasha taa ili kupata mwanga wa kutosha. Uwazi mwingi unategemea na aina, malengo na matumizi ya jengo lenyewe lakini angalau uzingatiwe kama inabidi kupunguza kutumia nishati ya umeme katika kuleta mwanga.

UWAZI ZAIDI UNAONGEZA MWANGA NA HEWA NDANI YA JENGO HIVYO KUPUNGUZA MATUMIZI MAKUBWA YA NISHATI, HASA UMEME

-Kuhakikisha jengo linakuwa na mzunguko sahihi wa hewa ndani ya jengo (cross ventilation), ambayo itasaidia kupatikana kwa hewa safii muda wote ili kuepusha matumizi makubwa ya viyoyozi na feni ndani ya jengo ambavyo vinagharimu matumizi makubwa ya umeme. Hili litawezeshwa zaidi na kuwepo kwa uwazi(openings) zaidi ya mmoja ndani ya chumba au eneo moja la jengo ambavyo vitawezesha mzunguko wa hewa unaosaidia hewa kuwa safi muda wote hivyo kutolazimika kutumia kiyoyozi(AC).

MZUNGUKO SAHIHI WA HEWA NDANI YA JENGO UNAWEZESHWA NA KUWEPO KWA UWAZI ZAIDI YA MMOJA NDANI YA CHUMBA

-Aina ya rangi inayopakwa baadhi ya maeneo huchangia pia kuongeza au kupunguza mwanga ndani ya jengo au ndani ya eneo fulani la jengo na hivyo kuongeza au kupunguza matumizi ya nishati. Kwa mfano tunajua kwamba kisanyansi rangi nyeupe huakisi mwanga (light reflection) hivyo kama kuna kuna ndani ya nyumba ambayo haijaweza kuwa na eneo la uwazi lakini inaweza kumulikwa na ukuta unaopata mwanga wa kutosha kutoka kwenye upande mwingine wa jengo wenye uwazi basi ni vyema ikapakwa rangi nyeupe. Hii itasaidia eneo hilo la kiambaza(corridor) kuwa na mwanga wa kutosha wakati wa mchana bila kulazimika kuwasha taa inayotegemea nishati ya umeme ili kuongeza mwanga ebeo husika.

RANGI NYEUPE HUAKISI MWANGA(LIGHT REFLECTION) HIVYO KUSAIDIA KUPELEKA ZAIDI MWANGA MAENEO KWENYE VIAMBAZA(CORRIDORS & LOBBIES)

-Uelekeo sahihi wa jengo katika eneo au mazingira husika huchangia kuongeza au kupunguza matumizi ya nishati kadiri ya uchaguzi sahihi wa uelekeo wa jengo ulivyofanyika (building orientation). Jengo linapaswa kuelekezwa eneo ambalo kuna uelekeo sahihi wa upepo na sehemu ambayo haina msongamano wa vitu vinavyozuia jengo husika kupata hewa na mwanga asili wa kutosha.

UELEKEO SAHIHI WA JENGO HUSAIDIA UPATIKANAJI ZAIDI WA MWANGA NA HEWA NDANI YA JENGI HIVYO KUPUNGUZA GHARAMA ZA UMEME

-Kuwepo kwa uwazi kutokea juu ni moja ya mbinu unayoweza kuitumia kuongeza mwanga na hewa ndani ya jengo hivyo kupunguza gharama za matumizi makubwa ya nishati hasa nishati ya umeme. Uwazi huu unaweza kuwa ni uwazi ambao uko kati ya ghorofa ya chini na ghorofa ya juu ambapo unaruhusu mzunguko mkubwa zaidi wa hewa kwa ghorofa ya juu na ya chini kwa wakati mmoja pamoja na mwanga mwingi zaidi kutoka ghorofa ya juu na ghorofa chini au unaweza kuwa ni uwazi uliopo kwenye jengo kutokea angani moja kwa moja ambapo mwanga na hewa vinaingi kwenye jengo kutoka angani hivyo kupunguza sana gharama za matumizi ya nishati hasa nishati ya umeme. Uwazi wa kutokea moja kwa moja angani moja kwa moja (open to the sky) mara nyingi huwekwa eneo la katikati ya jengo ambalo kwa chini yake sio eneo la matumizi na ambapo hata mvua ikinyesha bado haiathiri shughuli nyingine ndani ya jengo au kuwekwa kioo kwa juu kitakachowezesha eneo hili kutumika japo itakuwa ni kikwazo kwa kiasi kwenye mzunguko wa hewa.

UWAZI WA JUU KATIKATI YA JENGO HUONGEZA MWANGA NA HEWA YA ASILI NDANI YA JENGO
UWAZI KATI YA GHOROFA YA CHINI NA YA JUU YAKE HUSAIDIA KUONGEZA MWANGA NA KUHIMIZA MZUNGUKO SAHIHI WA HEWA NDANI YA JENGO

Architect Sebastian Moshi

Whatsapp/Call +255717452790

0 replies

Leave a Reply

Want to join the discussion?
Feel free to contribute!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *