KERO ZA NYUMBA ZA KUPANGA ZINACHANGIWA SANA NA KUTOJENGA KITAALAMU.

Katika eneo la nyumba za kupanga kumekuwa na kero mbalimbali tofauti na usumbufu unaotokea kati ya mwenye nyumba na wapangaji wake, nyingi kati ya hizi zikiwa zinasababishwa na misuguano kati ya wapangaji kutokana na kushindwa kuelewana au kuwa kero kati ya mmoja na mwingine kutokana na sababu mbalimbali.

Hili kwa sehemu kubwa likiwa linasabishwa na muingiliano mkubwa kati ya mpangaji mmoja na mwingine kutokana na udhaifu wa kitaalamu wa ujenzi husika ambao umeshindwa kulipa kipaumbele suala la faragha kati ya mpangaji mmoja na mwingine wakati wa kutengeneza ramani ya jengo husika.

KUWEKA KIPAUMBELE KWENYE FARAGHA NI MUHIMU SANA KATIKA KUPUNGUZA KERO ZA NYUMBA ZA KUPANGA.

Hili eneo la nyumba za kupanga ndio eneo ambalo suala la faragha na kupunguza muingiliano wa aina yoyote kati ya mpangaji mmoja na mwingine linapaswa kupewa kipaumbele cha hali ya juu wakati wa kutengeneza ramani ya jengo husika kwa sababu ndio eneo linachangia sana hadhi ya jengo. Katika utafiti mdogo niliofanya kuzungumza na wapangaji kadhaa wengi hili suala la faragha limekuwa ni moja ya kero kubwa inayowasumbua zaidi na pale wanapobahatika kupata nyumba ya kupanga yenye faragha ya kutosha wanaichukulia kama nyumba yenye hadhi ya juu na yenye ubora.

WAPANGAJI WAMEKUWA WAKIIONA NYUMBAYA KUPANGA YENYE FARAGHA KAMA NI NYUMBA YENYE HADHI YA JUU.

Eneo lingine muhimu ambalo nyumba za kupanga zinashindwa kulitendea haki ni kwenye kujitegemea kwa huduma kati ya mpangaji mmoja na mwingine, kwa mfano suala kama mpangaji kujitegemea katika suala la umeme, maji, maliwato n ahata ikiwezekana kama ni nyumba kubwa yenye pande mbili peke yake basi hata geti la kuingilia kila mtu awe na lake kadiri nafasi itakavyoruhusu.

KILA MPANGAJI ANAHITAJI KULIPIA HUDUMA MUHIMU KAMA MAJI, UMEME, N.K., KIPEKEE.

Eneo jingine la kulipa kipaumbele ni kwenye parking za magari ambapo ikiwa jengo linajengwa kiholela na wahusika hawana uzoefu hata wa ukubwa sahihi unaotosha kuruhusu gari kuingia na kutoka bila kuleta matata na kuanza kufikiria hata kabla ya kufikiria ramani yenyewe, basi changamoto ya “parking” ya gari nayo huwa ni kero na jengo husika kuchukuliwa kama halina hadhi ya kutosha au wapangaji kujikuta wakigombania “parking”, kitu ambacho huwa kero kubwa kwao.

KUPANGILIA NAFASI KWA USAHIHI ILI KUFANIKISHA KUPATA “PARKING” ZA GARI.

Hivyo kabla ya kuanza kufikiria kuhusu kujenga nyumba za kupanga za namna yoyote ile na ukubwa wowote ile, ni muhimu sana kukutana na mtaalamu na kukaa chini kujadili kwa kina juu ya ramani na mahusiano yatakayokuwepo baina ya wapangaji na namna ramani yenyewe ya jengo inaweza kusaidia kutatua changamoto hizi za migogoro baina ya wapangaji. Hapo utaweza kupata ramani nzuri na ambayo italeta thamani kubwa kwa nyumba inayoenda kujenga ambayo matokeo yake itapendwa zaidi na wapangaji.

Architect Sebastian Moshi

Whatsapp/Call +255717452790

0 replies

Leave a Reply

Want to join the discussion?
Feel free to contribute!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *