MASHARTI NA VIGEZO VINAVYOHITAJIKA ILI KUPATA KIBALI CHA UJENZI HALMASHAURI

Japo kila halmashauri ya manispaa au halmashauri ya mji ina masharti yanayotofautiana kwa kiasi katika kutimiza vigezo vya kuweza kupewa kibali cha ujenzi wa jengo ndani ya manispaa au mji husika lakini msingi wa mahitaji yake hufanana.

KILA HALMASHAURI YA JIJI, MANISPAA AU MJI HUWEZA KUTOFAUTIANA KWA KIASI JUU YA VIGEZO NA MASHARTI YA KUPEWA KIBALI CHA UJENZI

Kwanza inatakiwa ukamilisha angalau seti saba za michoro ya usanifu majengo katika nakala ngumu angalau tatu. Michoro hiyo saba inajumuisha ramani ya sakafu ya/za chini(floor plan(s)), muonekano wa pande zote nne za jengo(elevations), ramani ya wima iliyotokana na jengo kukatwa katikati(cross section), ramani ya paa(roof plan), ramani ya kiwanja na mpangilio wake wa namna jengo lilivyokaa katika kiwanja na vitu vingine(site layout plan) pamoja na ramani na mpangilio wa mfumo wa maji taka(septic details). Michoro yote hii inapaswa kuwa imezingatia masharti na mahitaji ya halmashauri ya manispaa na mji husika kwa kila kitengo kinachohusika ambapo masharti na mahitaji wakati mwingine huweza kutofautiana kidogo kati ya halmashauri ya manispaa moja na nyingine. Michoro hii itapitishwa katika idara zote za halmashauri husika na kukaguliwa kama imetimiza vigezo na ndipo huruhusiwa kupita mpaka itakapomaliza na kuandikiwa kibali.

MICHORO YA RAMANI INAPITA IDARA ZOTE ZA HALMASHAURI HUSIKA KUKAGULIWA KAMA IMETIMIZA VIGEZO ILI KUANDIKIWA KIBALI CHA UJENZI

Kama jengo ni la ghorofa itatakiwa pia michoro mingine ya uhandisi mihimili ambayo nayo huwa na seti saba za michoro katika nakala ngumu angalau mbili pamoja na mahesabu ya kiuhandisi ambayo yamepelekea kufikia hitimisho hilo la michoro iliyofikiwa na mhandisi mihimili. Michoro hii ya uhandisi hujumuisha ramani ya msingi(foundation plan), taarifa za ndani za kuta(wall details), ramani za nguzo(columns plans and sections), ramani ya ngazi na taarifa zake za ndani(stair plans details and sections), ramani za boriti na taarifa zake za ndani(beam plans details and sections), taarifa za sakafu za sakafu za chini(slabs plans, details and sections), taarifa za paa(roof plans details and sections).

Michoro yote inapokuwa inaendana na vigezo na masharti ya halmashauri husika huwa ni rahisi kukamilisha taratibu nyingine na kupatiwa kibali cha halmashauri.

Architect Sebastian Moshi.

Whatsapp/Call +255717452790.

0 replies

Leave a Reply

Want to join the discussion?
Feel free to contribute!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *