FAIDA ZA KUANZA MAANDILIZI YA UJENZI WA KISASA MAPEMA, KABLA HATA YA KUWA NA PESA.

Kama kuna kitu kimoja kinachohitaji maandalizi na mipango muhimu basi ni mradi wowote ujenzi hasa wa nyumba ya kuishi au jengo la aina yoyote. Ujenzi ni kitu kinachohusisha mambo mengi sana kuanzia utaalamu, uchaguzi wa watu sahihi wa kufanya nao kazi, uamuzi wa eneo sahihi la kujenga, kudili na mamlaka zinazoshughulika na mambo yanayohusiana na ujenzi, pamoja na fedha nyingi kwa ajili ya kufanikisha mradi husika wa ujenzi.

KUJIANDAA MAPEMA NA UJENZI HATA KAMA HUNA PESA NI FURSA YA KUFAHAMU MAMBO MENGI NA KUFANYA MAAMUZI SAHIHI.

Tatizo kubwa ni kwamba watu wengi huwa hawajui uzito wa michakato hii pamoja na uhalisia wa gharama za ujenzi mpaka pale wanapofikia kuamua kutaka kujenga ndipo hukutana na uhalisia wakiwa na mawazo tofauti kabisa katika akili zao na hilo wakati mwingine kupelekea kuahirisha kujenga au kubadilisha aina ya jengo walilokuwa wamepanga kujenga kwa sababu wanakutana na mambo ambayo hawakutarajia na hawakuwa wamejipanga nayo.

KUJIANDAA MAPEMA UTAWEZA KUJUA UKUBWA WA GHARAMA KWA USAHIHI NA KUFANYA MAANDILIZI SAHIHI.

Kwa hiyo mtu anapojiandaa akiwa bado hana kitu ana huru sana kusikiliza nini kinachotakiwa na kufanya maandilizi sahihi, na kwa upande wa gharama mtu huweza kuwa huru zaidi kuchagua aina ya nyumba sahihi anayoihitaji huku akijua kwamba anaenda kujipanga na hivyo hahitaji sana kulazimisha namna anayotaka yeye kwa kuangalia kiasi alichonacho. Mtu anapokwenda kujipanga nguvu na akili zake hupelekwa kwenye maandilizi sahihi na hasa kiasi sahihi cha pesa anachohitaji ili kukamilisha mradi wake hivyo ataweka malengo sahihi zaidi ya kufikia ili akamilishe lengo husika. Mwenendo wa mradi wake utaenda vizuri na kwa mipango sahihi kwani atafanyia kazi kwa uhalisia na kwa namna ambayo imepangwa kwa usahihi.

KUJIANDAA MAPEMA KUTAKUEPUSHA NA CHANGAMOTO NYINGI ZA UJENZI WA KISASA

NB: Suala la kujiandaa na ujenzi sasa hivi kabla hata ya kuwa na fedha ni muhimu sana kwa sababu licha ya kufanya maandilizi sahihi yatakayokupa picha halisi ya unachoenda kufanya lakini pia litakuepusha na changamoto nyingi ambazo utakutana nazo endapo utakuwa hukujipanga.

Architect Sebastian Moshi.

Whatsapp/Call +255717452790.

1 reply

Leave a Reply

Want to join the discussion?
Feel free to contribute!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *