KUJENGA NYUMBA YA GHARAMA NAFUU.

Nyumba ya gharama nafuu ni dhana ambayo watu wengi sana wamekuwa wakiifikiria na kwa kutumia hisia watu wamekuwa wakiamini kwamba inawezekana kuna muujiza fulani wa kujenga nyumba kwa gharama nafuu kwa kutumia mbinu fulani fulani ambazo pengine zipo. Japo dhana hii ya “gharama nafuu” ipo jumla jumla sana na kila mtu ana mtazamo wake mwenyewe kichwani juu ya maana ya huu “unafuu” unaozungumzwa. Mtu mwingine unafuu kwake ni milioni 5, mwingine unafuu ni milioni 20, mwingine unafuu ni milioni 50 na mwingine unafuu ni milioni 100. Kila mtu ana mtazamo wake kulingana na upana wa fikra zake na uzoefu binafsi juu ya fedha na kile anachokiongelea.

KILA MTU ANA UZOEFU BINAFSI JUU YA FEDHA NA HILO LINASABABISHWA DHANA YA “UNAFUU” KUWA TATA ZAIDI

Je kuna unafuu wowote katika ujenzi?

Jibu ni ndio unafuu upo lakini sio kwa namna ambayo wengi wanafikiria, kwa sababu kikubwa nilichogundua ni kwamb kila mtu anafikiria unafuu kwa kuangalia uwezo wake binafsi na uzoefu wa kifedha bila kufikiria uhalisia wa gharama husika. Pia unafuu wa gharama za ujenzi sio mkubwa sana kwa sababu unafuu unapokuwa mkubwa hata ubora wa vifaa na huduma za ujenzi unakuwa chini na mradi mzima badala ya kuwa nafuu unaweza kurudi kuwa ghali kwa sababu ya hasara inayotokana na marekebisho mengi yaliyosababishwa na vifaa na huduma za viwango duni ambavyo vilikuwa nafuu sana. Hivyo unafuu huu inatakiwa mtu uufahamu kwanza ili ujue ni unafuu mkubwa kiasi gani. Kwanza kabisa unapaswa kujua uhalisia wa gharama ndipo ujue unafuu uko wapi na ni mkubwa kiasi gani.

NI MUHIMU KUFAHAMU UHALISIA WA GHARAMA HUSIKA NDIPO UWEZE KUJUA UNAFUU NI KIASI GANI NA UNATOKANA NA NINI

Lakini hapo juu tunazungumzia mradi ambao tayari unao na michoro ya ramani umeshachora sasa unawaza kuhusu unafuu, lakini kuna aina nyingine ya unafuu ambayo ni halisia zaidi. Aina hii ya unafuu wa ujenzi ni kupunguza ukubwa wa jengo, yaani badala ya jengo kuwa la vyumba vinne unapunguza liwe la vyumba vitatu au badala ya vyumba vitatu unapunguza liwe la vyumba viwili au unaondoa baadhi ya vyumba vingine visivyo vya lazima hivyo jengo linapungua ukubwa, au unapunguza sana ukubwa wa vyumba ili jengo lipungue sana na hivyo gharama kwa ujumla zinapungua kwa kadiri ya jengo lenyewe linavyopungua. Jambo la muhimu la kufahamu hapa ni kwamba ukubwa wa jengo ndio ukubwa wa gharama zenyewe za ujenzi hivyo kupunguza gharama unajaribu kulenga zaidi kupunguza gharama za ukubwa wa jengo husika.

KUPUNGUZA UKUBWA WA JENGO HUSIKA NI KATI YA NJIA ZENYE UHALISA ZAIDI ZA KULETA UNAFUU

Lakini njia hiyo ya kupunguza ukubwa wa jengo bado kuna watu wengi wanaweza kuona haiwafai kwa sababu wanahitaji nyumba yenye ukubwa huo huo kwa sababu ndio inakuwa imetimiza mahitaji yao muhimu na chini ya hapo inakuwa bado haiwatoshi. Sasa njia nyingine ambayo inaweza kuwa ni sahihi zaidi ni kutopunguza ukubwa wa nyumba lakini kujenga nyumba kwa awamu na kuihamia kabla hajakamilika huku ukiendelea kuikamilisha taratibu. Kwa mtu ambaye anahitaji nyumba ya kumtosha lakini anaona gharama ya kuikamilisha yote kwa pamoja ni kubwa anaweza kutengeneza ramani kwa namna ambayo ataanza ujenzi na kuikamilisha kwa sehemu ambayo anaweza kuihamia na kuishi huku akiendelea kuikamilisha taratibu maeneo mengine bila kupata usumbufu mkubwa. Kwa mfano mtu anaweza kujenga nyumba ya ghorofa akakamilisha vipengele vyote vya mihimili ya jengo kisha akamalizia vyumba viwili vya juu na kuanza kuvitumia huku akiendelea kumalizia vingine taratibu, hivyo kwa kuwa itamchukua muda mrefu kukamilisha itampa urahisi wa kuimalizia taratibu bila presha kubwa kitu ambacho ni unafuu mkubwa kwa watu wengi.

KUPUNGUZA IDADI YA VYUMBA NI KATI YA NJIA HALISIA PIA ZA KUPATA UNAFUU WA GHARAMA

Architect Sebastian Moshi.

Whatsapp/Call +255717452790.

0 replies

Leave a Reply

Want to join the discussion?
Feel free to contribute!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *