KUJENGA KWA HATUA NI BORA KULIKO KUCHAKACHUA GHARAMA.

Watu wengi wanapofikia hatua ya kuamua kuanza ujenzi wakiwa tayari wameweka kiasi cha fedha ambacho walitegemea kingefanikisha kukamilisha mradi mzima wa ujenzi mara nyingi wanakuta fedha hiyo haitoshi na wanahitajika fedha zaidi pengine nyingi sana ukilinganisha na iliyopo. Sasa inapotokea watu wanapojikuta katika hali hii baadhi huamua kufikiria namna ya kupunguza gharama za ujenzi ziendana na ukubwa wa bajeti iliyopo. Hii hupelekea watu kupanga na kutumia vifaa vya ujenzi vya bei rahisi, kutafuta mafundi wa bei rahisi na kutumia wataalamu wa ramani wa kuungaunga sana ambapo matokeo yake huishia kuwa na nyumba ya hovyo, dhaifu na isiyodumu muda mrefu na kuishia kupata nyufa na uharibifu mwingine ndani ya muda mfupi sana tena wakati mwingine kabla hata haijahamiwa na wakati mwingine bado inaweza hata isikamilike pia.

UNAWEZA KULAZIMISHA BAJETI ULIYONAYO KUMALIZA UJENZI WA MRADI WAKO NA BADO IKASHINDWA KUKAMILISHA

Ni muhimu sana badala ya kukimbilia kukamilisha nyumba kwa haraka haraka kiholela kwa sababu ya ufinyu wa bajeti ni bora sana kujenga kwa hatua ambapo utaanza kwa kujenga mpaka pale bajeti itakapoishia kisha kujipanga upya na kufikiria njia mbadala za kutafuta kiasi kingine cha fedha kuendelea mpaka kukamilisha. Kujenga kwa haraka haraka ili kulazimisha bajeti iliyopo kutosha nji kujiandaa na hasara kubwa pamoja na majuto mbeleni kwani kwa kawaida ujenzi unatumia pesa nyingi sana hivyo utajikuta katika majuto makubwa ya kutumia fedha nyingi kujenga jengo bovu. Hili ni muhimu sana kulifikiria kwa sababu mara nyingi mtu anapokuwa na shauku ya kukamilisha mradi wake huwa hisia zinakuwa juu na anafikiria matokeo peke yake bila kuwaza uhalisia wa mchakato mzima utakaomfikisha kwenye matokeo hayo, na kwa kuwa hisia zinakuwa juu basi mtu hukimbilia kufanya maamuzi hata kama sio maamuzi sahihi kwa sababu muda huo akili yake ipo kwenye kufikiria matokeo na kupuuzia uhalisia wa mchakato mzima utakaomfikisha kwenye matokeo. Hivyo uhalisia wa mchakato unapokuwa dhaifu matokeo yanayotarajiwa yanashindwa kufikiwa.

NI HATARI KUJARIBU KULAZIMISHA BAJETI ULIYONAYO KUMALIZA MRADI WAKO WA UJENZI UNAPOKUWA UMESHAONA WAZI KWA HATA HAITOSHI

Ni muhimu sana kuhakikisha kwamba kila kitu kinapangwa kwa usahihi na kwa uhakika kabla ya kuanza mradi unaogharimu pesa nyingi kama mradi wa ujenzi ambao ukifeli utaishia kukuingiza kwenye hasara kubwa na majuto.

Architect Sebastian Moshi.

Whatsapp/Call +255717452790.

0 replies

Leave a Reply

Want to join the discussion?
Feel free to contribute!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *