NYUMBA YA NDOTO ZAKO.
Karibu kila mtu kwenye maisha huwa na nyumba ya ndoto zake, hasa watu wanapokuwa katika umri mdogo kila mmoja huota kwamba atakuja kuishi kwenye nyumba fulani na mara nyingi nyumba hiyo huwa ni kubwa na ya kifahari sana. Kwa uzoefu wangu ni watu wachache ambao hufikia ndoto hii mapema kadiri ya ndoto zao. Watu wengi hufanikiwa kufikia ndoto hii wakiwa kwenye umri wa miaka ya 50 kuendelea na wachache huweza kufikia wakiwa kwenye miaka ya 40 na mmoja mmoja sana hufanikiwa kufikia akiwa kwenye miaka ya 30 kama atakuwa ameanzia chini kabisa kutafuta mafanikio. Lakini hata hivyo haijalishi umefikia nyumba ya ndoto yako ukiwa umri gani jambo la muhimu ni kuishi kwenye nyumba ya ndoto zako.
Lakini kutokana na ukweli kwamba nyumba nyingi za ndoto zetu ni za gharama kubwa sana na vipato vya wengi huchelewa kukua kufikia kumudu nyumba za gharama kubwa kiasi hicho mapema mtu unaweza kuanza kwa kujenga nyumba inayoendana na kipato ulichonacho kwa sasa kisha baadaye ndio ukaja kujenga nyumba ya ndoto yako baada ya kipato chako kuwa kimekuwa kiasi cha kuweza kumudu nyumba ya gharama hizo. Lakini hata hivyo ikiwa una mpango wa kujenga mara moja peke yake na huhitaji kurudi kujenga nyumba ya kuishi mara mbili mbili au ikiwa kuna eneo maalumu ambapo ndipo unapotaka kujenga nyumba ya kuishi na unahitaji eneo hilo hilo ndio ujenge nyumba ya ndoto yako kwa sababu zozote zile, basi hilo bado ni jambo linalowezekana kabisa. Kinachotakiwa ni kwamba unaweza kujenga nyumba ya kawaida kwa sasa lakini hiyo hiyo ikiwa na maandalizi ya kuja kujenga nyumba ya ndoto yako, yaani nyumba husika iwe imejengwa kwa matarajio ya kuja kujenga nyumba ya ndoto yako ambapo muda ukifika kitakachofanyika ni kuiendeleza iliyopo kuwa nyumba ya ndoto zako. Nyumba hiyo itafanyiwa mabadiliko kutokea hapo ilipo kuelekea kuwa nyumba ya ndoto zako na kwa sababu ilishaandaliwa hivyo tangu mwanzoni basi ni kazi ambayo inaweza kuja kuendelezwa. Kufanya hivi haimaanishi kwamba hii nyumba ya kawaida haitajengwa kukamilika, hii nyumba utakayojenga mwanzoni itakuwa nyumba iliyokamilika kwa kila kitu na itakayokuwa inatumiwa kama nyumba kamili lakini muda ukifika ndio itakayoendelezwa na kuwa nyumba ya ndoto zako.
Hata hivyo ni watu wa chache na kwa sababu maalum hupendelea kuendeleza nyumba yake ya kawaida kwenda kuwa nyumba ya ndoto yake kwa sababu utofauti wa kipato kati ya nyakati za kujenga nyumba ya kawaida na nyumba ya ndoto huwa ni mkubwa sana kiasi kwamba hata ukubwa wa kiwanja na hadhi ya eneo husika kwa maana ya mtaa au mji huwa tofauti sana na wengi hupendelea maeneo yenye hadhi ya juu zaidi.
Architect Sebastian Moshi
Whatsapp/Call +255717452790
Leave a Reply
Want to join the discussion?Feel free to contribute!