GHARAMA ZA UJENZI WA KISASA NI TOFAUTI KABISA NA “VIJANA” WENGI WANAVYOFIKIRI
Kama eneo la ujenzi ambalo limekuwa ni changamoto sana kueleweka kwa usahihi ni eneo la gharama za ujenzi. Japo suala zima la uelewa sahihi wa gharama za ujenzi kwa ujumla limekuwa ni changamoto hata kwa watu wenye katika sekta ya ujenzi kutokana na utofauti mkubwa wa mambo mengi kuanzia ukubwa wa mradi, viwango ambavyo mradi unatakiwa kujengwa pamoja na aina ya jengo lenyewe lakini kwa vijana ambao hawana uzoefu na masuala ya ujenzi limekuwa ni tatizo zaidi. Watu wengi na hasa vijana wana mtazamo tofauti kabisa na gharama halisi za ujenzi kitu ambacho hupelekea kutoamini gharama hizo pale wanapotajiwa gharama za ujenzi. Watu wengi huchukulia mradi wa ujenzi kwa urahisi sana mpaka pale wanapokuja kujenga ndio hupata uelewa sahihi wa ni jinsi gani suala la kujenga sio suala rahisi kama wanavyodhani kama ilivyo kununua gari au hata kiwanja. Mtazamo huu umepelekea pia hata mivutano mikubwa kwenye huduma zinazoambatana na ujenzi kama vile huduma za michoro ya ramani kuonekana ni za gharama kubwa sana japo katika uhalisia ni ndogo ukilinganisha na thamani ya kile kinachokwenda kufanyika.
Ni kawaida kukuta kijana anakwambia anahitaji kujenga nyumba ya kiasi cha milioni saba za kitanzania au kufikiri labda nyumba inaweza kugharimu kiasi cha milioni kumi au ishirini. Ukweli ni kwamba kwa makadirio ya chini kabisa na kwa kujitahidi kuipunguza kabisa nyumba sio rahisi kukamilisha ujenzi wa nyumba ya vyumba vitatu kwa chini ya kiasi cha milioni 80 za kitanzania hata kama utajitajidi kuweka umakini kwenye gharama kiasi gani. Watu wengi ukiwaambia haya huwa hawaamini mpaka watakapojenga ndio wanagundua kwamba huo ni ukweli kwa sababu wakati mwingine wanaweza kupotoshwa na mtu ambaye wanaona tayari alishajenga bila kujua kwamba pengine alijenga kwa awamu na hajafanya mahesabu ya gharama zote kwa ujumla kujihakikishia kwamba ni kiasi gani cha fedha alitumia kwa mradi wote. Kiasi cha pesa kama milioni 10 za kitanzania zitaishia kujenga msingi wa nyumba peke yake, tena nyumba ya vyumba vitatu na sio zaidi hapo. Wakati mwingine pia unaweza kukutana na upotoshaji mtandaoni wa watu ambao wanajiita ni wataalamu lakini wasio na uzoefu wowote wakakudanganya kwamba kuna nyumba ya vyumba vitatu unaweza kuikamilisha kiasi cha shilingi milioni 50 za kitanzania kwa tamaa ya wao kupata kazi husika lakini kwa gharama ya kukupotosha wewe, hao pia ni watu wa kuwa nao makini sana.
Ikiwa unataka kufahamu wastani wa gharama ya nyumba husika unachopaswa kufanya ni kuchukua mita za mraba za eneo la sakafu ya nyumba unayotaka kujenga na kuzidisha kwa kiasi cha pesa za kitanzania kati ya laki 7 mpaka milioni 1 na gharama utakayopata ndio wastani wa gharama kwa ujumla, gharama hiyo ya jumla uliyopata inaweza kupungua kwa kadiri ya machaguo utakayofanya kwenye ujenzi lakini hatapungua kwa kiasi kikubwa sana kutokea kwenye wastani yaani kwa mfano haiwezi kupungua kufikia nusu ya wastani huo ulioupata. Ikiwa huna mita za mraba au huna kabisa ramani ya nyumba bado unaweza kutumia makisio ya mita za mraba kati ya 150 mpaka 200 kwa makadirio ya chini ya wastani wa ukubwa wa sakafu ya jengo la vyumba vitatu.
Architect Sebastian Moshi.
Whatsapp/Call +255717452790.
Leave a Reply
Want to join the discussion?Feel free to contribute!