KABLA YA KUNUNUA KIWANJA PATA USHAURI KUTOKA KWA MTAALAMU WA UJENZI

Imekuwa utamaduni wa kawaida kwamba mtu anapoamua kununua kiwanja hufanya hivyo kwa kuangalia upatikanaji wa kiwanja na gharama zake bila kufikiria kile ambacho anaenda kujanga kwenye eneo husika. Ni kweli kwamba mtu huweza kununua kiwanja kwa ajili ya kujenga baadaye hivyo akili yake kufikiria zaidi kuhusu kununua kiwanja husika bila kujali kama kinatimiza vigezo vya ule mradi wa ujenzi anaopanga kujenga hapo. Huu umekuwa ni utamaduni wa kawaida kwa sababu tumekuwa tunasukumwa na hisia zaidi kitu ambacho kinapelekea kutojali sana kuhusu mambo ya mbele na badala yake kuhakikisha kile tunachokilenga sasa hivi kwanza kinafanikiwa.

MRADI UNAOTAKA KUJENGA PAMOJA NA MAHITAJI YAKE MENGINE VINAPASWA KUENDANA NA UKUBWA PAMOJA NA UMBO LA KIWANJA HUSIKA

Hata hivyo umuhimu wa kujua unachotaka kufanya katika kiwanja husika na hivyo kushirikisha mtaalamu wa ujenzi akupe mtazamo wake kitaalamu kwa kulinganisha namna kiwanja kilivyo hasa ukubwa wake na kile unataka kufanya katika eneo hilo ni muhimu sana. Tumekuwa tunakutana na baadhi ya kesi ambazo unakuta mtu ameshanunua kiwanja na sasa anataka kujenga mradi fulani ndipo anauliza kama kiwanja husika kitatosha au kitafaa kuweka mahitaji yake yote anayotaka kuweka katika eneo husika. Jambo hili mara kdhaa utakuta linaleta mivutano kwa sababu mbalimbali, kwanza kabisa mamlaka husika huwa na vigezo na masharti yake juu ya namna ya matumizi ya eneo kwa kuzingatia kinachoenda kufanyika kwenye kiwanja husika ambayo huathiri mradi husika kadiri ya ukubwa au umbo la kiwanja hicho. Lakini pia ukiachana na vigezo na masharti ya mamlaka husika mahitaji yako pia ni muhimu ukayaainisha mapema kuona kama eneo husika litaweza kuyamudu kadiri ya ukubwa wa uhitaji wa kuhimili mahitaji husika. Hayo yote utaweza kuyafahamu kwa kumshirikisha mtaalamu wa ujenzi ambaye ana uzoefu mkubwa wa kucheza na vipimo vitu mbalimbali na kujua mpangilio utakavyoweza kukaa kwa uhakika na bila kuleta usumbufu wala mwingiliano unaoweza kusababisha mkwamo.

MAMLAKA ZINAZOHUSIKA NA UJENZI PIA HUWA NA VIGEZO VYAKE AMBAPO USIPOVITIMIZA UTAKWAMISHWA KUPEWA KIBALI CHA UJENZI

Watu wengi wamejikuta katika changamoto na viwanja vyao kutokana na aidha umbo au ukubwa wake na kukwama kwenye mahitaji mengi muhimu kama vile kuweza kuegesha magari anayohitaji, kupata eneo la kufanyia mambo muhimu ya kijamii kama vile ibada, au kushindwa kufikia vigezo vya mamlaka husika juu ya mpangilio sahihi wa mahitaji husika katika kiwanja husika, mambo ambayo unapaswa kuyafahamu mapema ili kufanya maamuzi sahihi.

Architect Sebastian Moshi

Whatsapp/Call +255717452790.

0 replies

Leave a Reply

Want to join the discussion?
Feel free to contribute!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *