NI BORA KUJIKUSANYA UKAJENGA NYUMBA YAKO TARATIBU KULIKO KUHARAKISHA NA KULIPUA
Binadamu kiasili tumeumbwa kuvutiwa na kutamani matokeo ya mwisho wa jambo lolote bila kujali mchakato wake ulivyoenda, ambapo mtazamo huu umekuwa ukiongezea nguvu na msemo wa kiingereza unaosema, “the end justifies the means” ikimaanisha mwisho wa kitu ndio huweza kuelezea mchakato wake, yaani ilimradi tu ufike mwisho kisha njia uliyopitia au mchakato utajieleza wenyewe baada ya kumaliza. Hata hivyo saikolojia hii ya kuangalia na kufurahia matokeo ya mwisho pekee na kupuuza mchakato mara nyingi huwa haituachi salama.
Ujenzi ni kati ya mambo ambayo mtu unapaswa kuweka umakini mkubwa sana na fikra sahihi zinazokuepusha na hisia kwa sababu ni miradi inayohusisha kiasi kikubwa cha fedha na hivyo hasara zake ni kubwa sana pia. Imekuwa kawaida kwa watu kuwa na kiasi fulani cha fedha ambacho wamekitenga kwa ajili ya ujenzi ambapo huingia kwenye ujenzi wakiamini kinaweza kumaliza mradi wote wa ujenzi wanaotaka kuujenga lakini wanapokuja kugundua kiasi hicho hakitoshelezi basi wamekuwa wakichagua kufuata njia rahisi kwa kutafuta namna watajenga kwa gharama nafuu kwa kulazimisha kiasi husika kutosha. Hii ni kwa sababu wanasukumwa zaidi na matokeo ya mwisho ambayo pia wanayahitaji kwa haraka, na hivyo kujikuta wakitafuta kukamilisha kazi kwa gharama nafuu sana. Kinachokuja kutokea ni jengo/nyumba husika kuduma kwa muda mfupi na kuanza kudhoofika na kujikuta wakibaki na nyumba mbovu. Cha ajabu ni kwamba baadaye wanakuja kupata tena fedha nzuri na kujutia kwa nini hawakuwa na subira na wangejenga nyumba nzuri ambayo ni imara ambayo ingedumu kwa miaka mingi zaidi badala ya kuharakisha na kujiingiza kwenye hasara. Kama umegundua kwamba kiasi ulichonacho hakitoshi kukamilisha ujenzi wa nyumba yako, badala ya kutafuta urahisi utakaokugharimu mbeleni ni bora ukajenga nyumba bora ambayo itaishia sehemu fulani kisha kujipanga upya na kutafuta pesa za kutosha kumalizia kilichobaki ambapo utafurahia nyumba yako na kujiepusha na majuto.
Mara nyingi sana kutafuta urahisi na kuwa na haraka sana kwa kitu ambacho hakiwezi kumalizika ndani ya muda ambao unatamani kimalizike ni rahisi kukupeleka kwenye hasara na majuto.
Architect Sebastian Moshi.
Whatsapp/Call +255717452790.
Ni kweli kabisa rafiki yangu Architect Sebastian
Na muhimu tunajenga nyumba ya kuishi miaka mingi ijayo. Hivyo hakuna haja ya kujenga bila viwango bora.
Rafiki yako,
Aliko Musa