ENEO LA BUSTANI NYUMBANI, NYUMBA YAKO SIO KARAKANA.

Katika suala zima la ujenzi, hasa ujenzi wa makazi watu wamekuwa wakiweka umakini mkubwa zaidi kwenye ujenzi wa jengo la nyumba na kuweka umakini kidogo sana kwenye mandhari inayoizunguka nyumba kitu kinachopelekea kukosekana kwa umakini wa kimpangilio.

Jambo muhimu sana la kuzingatia ni kwamba makazi ya kuishi ni eneo linalotakiwa kuwa na mandhari bora yenye kuvutia sana na inayokuwa na madhara chanya sana kwa mtu kiafya na kisaikilojia kwa sababu ndio eneo ambalo mtu anategemea kupata utulivu mkubwa kuliko eneo jingine lolote hasa ukizingatia kwamba ndilo eneo pia ambalo watu wanakaa kwa muda mwingi zaidi.

Kwa maana hii, sehemu kubwa ya eneo linaloizunguka nyumba linapaswa kuwa na mazingira asili yanayoendana au kuwa katika maelewano mazuri kiafya na kisaikolojia kwa watu kwa kutengeneza kijani kibichi eneo kubwa kisha eneo la vigae vigumu au sakafu eneo dogo kadiri inavyowezakana.

KAMA UNA ENEO KUBWA LA KUTOSHA TENGENEZA PARADISO NYUMBANI KWAKO NA UTAFURAHIA SANA MAKAZI YAKO

Ni muhimu sana kwamba makazi ya nyumbani yanahitaji eneo lenye vigae vigumu ardhini kwa ajili ya magari kuingia, kuingiza vitu mbalimbali ndani sambamba na eneo la maegesho ya idadi magari kadiri ya uhitaji na umuhimu wake lakini eneo hili linapaswa kuwekwa kiasi kinachohitajika pekee.

Ni mara nyingi sana utakuta watu wameweka karibu eneo lote la nyumba vigae vigumu au sakafu bila kuwepo kwa uhitaji au ulazima na kufanya mandhari ya nyumbani kupoteza mvuto bila sababu.

Hili ni kosa kubwa kwa sababu, kwanza nyumbani sio eneo kwa ajili ya karakana ya magari wala watu hawana uzito wa tani nyingi kiasi cha kuhitaji ardhi ngumu kukanyaga kama magari, badala yake watu wanahitaji ardhi nzuri ya kijana inayovutia na kuleta utulivu wa kiakili.

KUPANGILIO KWA USAHIHI KUTAKUFANYA UYAFURAHIA MAZINGIRA YAKO YA NJE KAMA UNAVYOFURAHIA YA NDANI AU ZAIDI

Ni muhimu sana kujua idadi ya magari ya nyumbani ambayo yatakuwa yanaegeshwa nyumbani na kuweka eneo la maegesho la kutosha idadi inayohitajika pamoja na eneo kiasi la nyongeza kwa ajili ya kuingia, kutoka, kugeuka na kushusha mzigo au shughuli nyingine muhimu ambayo itahitajika gari kufika.

Baada ya hapo maeneo yaliyobakia yote yanapaswa kupangiliwa bustani nzuri za miti, nyasi, maua au mikondo ya maji ambayo inasaidia kufanya mandhari ya nyumbani kuwa na mvuto wa asili unaoleta utulivu na hamasa kwa wakazi.

Architect Sebastian Moshi

Whatsapp/Call +255717452790.

2 replies

Leave a Reply

Want to join the discussion?
Feel free to contribute!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *