SAIKOLOJIA YA MALIPO NA UBORA WA KAZI KWENYE UJENZI.

Sisi binadamu ni viumbe wa kisaikolojia ambapo saikolojia ni ile tabia na mienendo ya binadamu inayosukumwa na hisia mbalimbali zilizopo ndani ya mwili katika kuendea au kufanya jambo fulani kwa kulipa uzito fulani ambao ndio unaoamua kiasi na viwango vya ufanyaji wake.

Imekuwa kawaida kwa baadhi ya watu kutaka kazi fulani ya usanifu na wakati mwingine hata ujenzi ianze kufanyika baada ya majadiliano na maelewano lakini bila malipo kwa hoja kwamba malipo yatakuja baadaye hivyo mtu aendelee tu na kazi bila wasiwasi.

Kitu kimoja ambacho watu wengi wamekuwa hawaelewi ni kwamba ule msukumo wa kufanya kazi nzuri ya viwango bora unatokana na imani ambayo mtaalamu husika ameiweka kwa mteja na ikiwa imani hiyo haipo hilo huathiri ubora wa kazi kwa kiasi kikubwa.

Kutokana na uzoefu wa muda mrefu kutoka kwenye kazi zilizopita pamoja na uhalisia wa namna mambo yanavyokwenda duniani watu wengi wamepoteza imani sana linapokuja suala la kifedha hivyo ni vigumu mtu kuamini kwamba kazi fulani ya ujenzi itafanyika kwa ushawishi wa maneno peke yake bila mtu kujitoa kwa sababu licha ya kwamba watu hubadilisha mawzo kila siku lakini pia kuna watu wengine huongea lakini wakiwa hawana uwezo au fedha za kufanya kazi husika.

Hivyo uhakika wa kazi ambao unajenga imani kwa mtaalamu ambayo inasaidia kuweka uzito unaostahili na kufanya kazi ya viwango vya juu inatokana mteja mwenyewe kuonyesha kwa vitendo kwamba kazi husika ni halisi na inakwenda kufanyika.

Hivyo malipo ya kazi ya mapema aidha kabla kazi haijaanza au hatua ya pili baada ya kazi kuanza ni muhimu sana ili kuhakikisha kwamba mtaalamu husika anapata msukumo na kuweka uwajibikaji wa viwango vya juu katika kazi husika baada ya kujenga imani thabiti iliyoletwa na kujitoa kwa mteja husika.

Architect Sebastian Moshi.

Whatsapp/Call +255717452790.

0 replies

Leave a Reply

Want to join the discussion?
Feel free to contribute!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *