KUJENGA NYUMBA NI KAMA KUFANYA SHEREHE YA HARUSI.
Moja kati ya changamoto kubwa katika kudili na wateja wanaotaka kujenga nyumba ni pamoja na kwenye suala zima la uhitaji wa kufahamu bei halisi. Kutokana na uhalisia wa maisha yetu, wateja wengi wa kujenga nyumba huwa kitu cha kwanza ambacho huwa wanahitaji ni kufahamu bei kamili ya ujenzi wa nyumba yake ya kuishi kabla ya kingine chochote.
Licha ya kwamba ni sahihi kabisa mtu kutaka kufahamu gharama ya mradi mzima ili kujua kama una uwezo wa kutosha kufanikisha ujenzi huo au utahitaji kujiongeza zaidi, lakini dhana ya uhalisia wa gharama za ujenzi haipo katika urahisi wan mana hiyo. Hakuna gharama kamili ya moja kwa moja ya ujenzi bali kuna viwango mbalimbali vya gharama za ujenzi kutokana na sababu mbalimbali. Kuna vit una hali zinazosababisha hilo kama vile ukubwa halisi wa jengo ambao unapatikana baada ya kukamilisha michoro ya ramani za ujenzi, kuna ubora na bei tofuati ya gharama za malighafi na ufundi unaotumika katika ujenzi wa mradi.
Gharama za ujenzi pia zinatofautiana kati ya mji au mkoa mmoja na mwingine. Lakini pia viwango vya ubora wa jengo pamoja na muda ambao jengo hilo litatumia mpaka kukamilika pia unaleta utofauti wa gharama husika za ujenzi.
Hivyo ninaposema kujenga nyumba ni kama kufanya sherehe ya harusi ninamaanisha kwamba sio rahisi sherehe mbili za harusi zikafanana na hakuna bei ya moja kwa moja ya kusema gharama ya sherehe ya harusi ni kiasi fulani. Hata hivyo, licha ya utofauti mkubwa unaoweza kuwepo lakini kuna makadirio ya chini ya gharama za ujenzi wa nyumba kadiri ya makisio na namna mtu anaweza kudhania sababu nyingine zote.
Tunajua kwamba gharama za sherehe ya harusi zinategemea machaguo mbalimbali yatakayokuwa yamefanyika kama vile gharama za usafiri, gharama za picha na video, gharama za ukumbi, gharama za vyakula n.k. Pia vyote hivi gharama zake zinatofautiana kulingana na ubora na eneo ambalo tukio hilo linaenda kufanyika. Kwenye ujenzi napo gharama zinatofautiana kadiri ya ubora wa vifaa na ufundi wa jengi husika.
Kitu kingine muhimu sana kinachoamua gharama za sherehe ya harusi ni wingi wa watu watakaohudhuria kwani utaathiri ukubwa wa ukumbi na wingi wa vyakula na vinywaji pamoja na usafiri wa watu hao kutoka eneo moja kwenda jingine. Hivyo hivyo na kwenye ujenzi ndivyo gharama za ujenzi zinatofautiana kulingana na ukubwa wa jengo unaosababishwa na wingi wa mahitaji ndani ya jengo.
Hivyo kufahamu gharama halisi za ujenzi kwa uhakika ni muhimu kwanza kuwa na michoro ya ramani ya ujenzi wa nyumba/jengo husika, kisha baada ya hapo kufanya mjadala mpana na wa kina sana juu ya mradi husika ili kufahamu kila kitu kwa undani na hasa machaguo ambayo yanaenda kufanyika na gharama zake.
Karibu sana.
Architect Sebastian Moshi.
Whatsapp/Call +255717452790.
Leave a Reply
Want to join the discussion?Feel free to contribute!