USANIFU MAJENGO NA UJENZI – 17 – UJENZI MAHAKAMANI
KITABU: FOUNTAINHEAD.
AUTHOR: AYN RAND.
1. Kesi mahakamani ya Hopton Stoddard dhidi ya Howard Roark inasomwa mwezi Februari/1931.
2. Steven Mallory, Austen Heller, Roger Enright, Kent Lansing na Mike wanakaa upande mmoja katika eneo moja. Watu ni wengi sana mahakamani na wengi ni watu wanaofahamiana.
3. Howard Roark amekaa peke yake bila kuwa na wakili, watu wachache wanaomuunga mkono wanakasirishwa na kukata tamaa kwamba wameshashindwa.
4. Mwanasheria anayemwakilisha Hopton Stoddard anaeleza kesi yake kuanza kusema, ni kweli kwamba Howard Roark alipewa kazi ya kujenga hekalu na Hopton Stoddard lakini kile alichojenga hakiwezi kuwa hekalu kwa namna yoyote ile wala kwa viwango vyovyote vile vinavyojulikana.
5. Shahidi wa kwanza upande wa Hopton Stoddard ni Ellsworth Toohey, hakimu wa mahakama anajaribu kuelezea kwa kina wasifu wa Ellsworth Toohey na maandiko yake kisha anamuuliza Ellsworth Toohey kama hekalu hilo lililofanywa na Howard Roark lina kiasi chochote cha thamani ya kuitwa hekalu kwa viwango vya Usanifu majengo vinavyokubalika. Ellsworth Toohey anamjibu hakimu kwamba halina hata kimoja.
6. Ellsworth Toohey anaendelea, anatoa historia ndefu ya mahekalu yaliyowahi kujengwa katika historia kwa maelfu ya miaka na kuzungumzia sifa zake na vipengele vyote ilivyozingatia. Ellsworth Toohey anaeleza mpaka tarehe yaliyojengwa na kukamilika mahekalu hayo mpaka makadirio ya gharama za ujenzi. Watu wanashangilia sana makelele yanakuwa mengi mpaka kusababisha kushindwa kusikilizana mahakamani na hakimu kutoa amri ya kunyamazisha watu.
7. Hakimu anamuuliza Howard Roark kama ana swali lolote, Howard Roark anajibu kwamba hana swali.
8. Shahidi wa pili upande wa mlalamikaji ni Peter Keating. Hakimu anamwambia Peter Keating ataje majengo yote aliyowahi kufanya na anayataja lakini anaacha kutaja mradi wa Cosmo-Slotnick. Hakimu anamuuliza mbona amesahau jengo muhimu kwake kuliko yote la Cosmo-Slotnick na kumuuliza si ni yeye amefanya Cosmo-Slotnick? Peter Keating anajibu kwa sauti ya chini, “ndio”.
9. Hakimu anamuuliza Peter Keating kwamba alisoma kwenye chuo cha “Stanton Institute of Technology” mwaka mmoja na Howard Roark, sasa ana nini cha kusema juu ya maisha ya Howard Roark chuoni? Peter Keating anajibu kwamba alifukuzwa. Na alifukuzwa kwa kushindwa kuendana na viwango vya juu vya kitaaluma vya chuo cha “Stanton Institute of Technology”. Kisheria statement hii haikubaliki na kama Howard Roark angekuwa na mwanasheria angeikata lakini Howard Roark mwenyewe alinyamaza.
10. Hakimu anamuuliza Peter Keating endapo Howard Roark aliwahi kuonyesha uwezo au kipaji chochote katika fani ya Usanifu Majengo wakati akiwa chuoni “Stanton Institute of Technology”. Peter Keating anajibu hapana kwa sauti ya chini. Hakimu anamwambia aongee kwa sauti kubwa inayosikika, Peter Keating anajibu hajawahi kuonyesha kipaji chochote.
11. Hakimu anamuuliza Peter Keating kwamba aliwahi kumwajiri Howard Roark katika ofisi yake lakini baadaye akalazimika kumfukuza, kwa nini alimfukuza? Keating anajibu kwa sababu hakuwa na uwezo.
12. Peter Keating anaendelea kumzungumzia Howard Roark kwa kina zaidi na kueleza misimamo yake na tabia zake dhidi ya wateja ambazo yeye anaziona sio sawa. Anaeleza kwamba Howard Roark ana tabia nyingi za ajabu na amejaribu kumshawishi kubadilika, amejitahidi sana kumbadilisha lakini imekuwa kama ni kumpigia mbuzi gitaa. Anasema kwamba Howard Roark amekuwa kama anaibudu taaluma ya Usanifu Majengo lakini yeye hafikiri kama ina utakatifu wowote bali ni biashara kama biashara nyingine tu.
13. Hakimu anamwambia Peter Keating azungumzie jengo la hekalu la Hopton Stoddard, Peter Keating anaelezea kwamba lina makosa mengi ya kisanifu na anajaribu kuyafafanua. Lakini anasema ni makosa kumpa mradi kama huo Howard Roark, anadai kwamba mradi wa namna hiyo alitakiwa apewe mtu mwenye ubinadamu na sio Howard Roark.
14. Ralston Holcombe anatoa ushahidi kwa kuanza kuzungumza kwa kirefu sana juu ya taaluma ya Usanifu Majengo na ujenzi. Kisha anasema jengo hilo la hekalu ni upuuzi mtupu. Ralston Holcombe anasema lakini yeye hawezi kumuonea huruma Hopton Stoddard kwani ni uzembe wake, kwa sababu inajulikana wazi kwamba kwa majengo ya mahekalu na makanisa mtindo wa Usanifu Majengo inayokubalika ni ya nyakati za Renaissance, kwa nini yeye hakusisitiza tangu mapema kwamba hekalu hilo liendane na mtindo wake uendane na mtindo wa Usanifu Majengo wa nyakati za Renaissance?
15. John Erik Snyte naye anatoa ushihidi kwa kueleza namna Howard Roark asivyo mwaminifu kwani alianzisha ofisi yake kwa kumwibia mteja.
16. Siku ya nne Dominique Francon anatoa ushahidi. Anaanza kwa kueleza kwamba yeye anafikiri kwamba Hopton Stoddard amefanya makosa makubwa na kesi hiyo ingekuwa vizuri zaidi kama sio ingedai marekebisho ya jengo hilo bali kubomolewa kabisa kwa jengo hilo. Hakimu anaonekana kufurahia huo wa Dominique Francon.
17. Hakimu anamwambia Dominique Francon aelezee sababu zake kwa nini anafikiri linapaswa kubomolewa, Dominique anamjibu sababu zimeshatolewa na wote waliotangulia. Anamuuliza kwa hiyo anakubaliana nao, anajibu anakubaliana ushahidi wao zaidi hata ya hao walioutoa.
18. Hakimu anamtaka Dominique atoe maelezo kidogo ya ziada namna gani anakubaliana nao. Dominique anasema Ellsworth Toohey ameeleza vizuri kwa hekalu hilo ni hatari kwetu sote, amefafanua vizuri kabisa na ninakubaliana naye, sasa unataka nieleze zaidi? Hakimu anasema kwa vyovyote vile elezea.
19. Dominique anajaribu kufafanua kwa mapema ili kujaribu kueleweka lakini maelezo yake ni kwamba mtazamo wa Howard Roark na mtazamo wa watu wengine ni tofauti na yeye alishaonya mapema. Hakimu anachanganyikiwa anashindwa kuelewa Dominique anatetea upande gani na kumuuliza, Dominique anamjibu kwamba yuko upande wa Hopton Stoddard na wala hamlaumu Ellsworth Toohey bali anamlaumu Howard Roark.
20. Dominique anaeleza kwa kirefu na kuhitimisha kwamba watu wote wamesema kweli na jengo hilo ni bora likabomolewa kabisa. Jengo hilo ni hatari kwao wote kama alivyosema Ellsworth Toohey. Dominique Francon anamaliza na kusema jengo hilo la hekalu linapaswa kubomolewa sio kwa ajili ya kuwalinda watu dhidi ya hekalu hilo bali kwa ajili ya kulilinda hekalu hilo dhidi ya watu.
21. Hakimu anamuuliza Howard Roark kama ana swali anasema hana swali. Anamtaka alete ushahidi mezani, anapeleka michoro ya jengo hilo la hekalu la Stoddard.
Architect Sebastian Moshi.
Whatsapp/Call +255717452790.
Leave a Reply
Want to join the discussion?Feel free to contribute!