USANIFU MAJENGO NA UJENZI – 28 KUSHINDA KESI YA UJENZI

KITABU: FOUNTAINHEAD.

AUTHOR: AYN RAND.

1. Bodi ya wakurugenzi inaweka kikao na Gail Wynand na kuhoji maamuzi yake kwenye kampuni yanayosababisha kuiweka kampuni kwenye migogoro. Wanamhoji Gail Wynand kwa nini anamtetea Howard Roark na kwa nini amewafukuza kazi wafanyakazi wanne wakubwa ndani ya kampuni.

2. Hata hivyo Gail Wynand ndio mmiliki na mwenye kura nyingi zaidi hivyo ndiye mwenye maamuzi ya mwisho. Wanajaribu kumshinikiza aache kumtetea Howard Roark na kurudisha wafanyakazi waliofukuzwa akiwemo Ellsworth Toohey. Gail Wynand anasema hataki kusikia jina la Ellsworth Toohey likitajwa. Haongei kitu kingine chochote baada ya hapo.

3. Kwenye mkutano huo Alvah Scarret na Mitchell Layton wanajaribu kumhimiza Gail Wynand kufanya makubaliano na wafanyakazi waliogoma ili aweze kuirudisha kampuni mahali pake. Gail Wynand anakaa kimya bila kujibu chochote.

4. Howard Roark anajaribu kumtembelea Gail Wynand ofisini kwake ili kuzungumza naye lakini anajulishwa Gail Wynand hawezi kuonana naye. Gail Wynand anamkwepa kabisa Howard Roark. Howard anamwandikia barua na kumwambia asiwe na wasiwasi kabisa.

5. Alvah Scarret anajaribu kumpa moyo Gail Wynand kwamba wanaweza kujijenga upya. Alvah Scarret anafanya kazi kwa bidii sana ili kuirudisha kampuni katika ufanisi wa hali ya juu.

6. Dominique anaenda kwa Howard Roark ambaye amekodi apartment katika majengo ya Monadnock huko Florida kwa ajili ya mapumziko. Kisha Dominique anapiga simu kuomba msaada kwamba amepoteza mkufu wa dhahabu wenye thamani ya dola za Marekani milioni tano alionunuliwa na Howard Roark. Dominique anajitambulisha kama Mrs. Wynand lakini yuko nyumbani kwa Howard Roark hivyo anaomba msaada wa kutokana na upotevu huo.

7. Taarifa hiyo ambayo Dominique ameitoa kwa makusudi na ambayo ina mashaka ya kutokuwa na ukweli unasambaa huko New York na kumsababishia aibu Gail Wynand.

8. Alvah Scarret anapata habari hiyo na kuchukia sana na kumshinikiza Gail Wynand ampe talaka mara moja, Alvah Scarret mwenyewe anashughulikia suala hilo. Alvah Scarret ambaye ni mfanyakazi Mzalendo sana kwa Gail Wynand na ambaye siku anampenda na kumpigania sana boss wake Gail Wynand anamwambia Wynand kwamba hakupenda kabisa yeye kumuoa Dominique kwani alijua tu kwamba atakuwa sababu ya anguko lake.

9. Alvah Scarret anamwahidi Gail Wynand kwamba atamshugulikia Dominique vilivyo. Alvah Scarret anahakikisha zinaandikwa makala nyingi za kumtetea Gail Wynand na zaidi zinaonyesha kwamba alipotoshwa na kuharibiwa na mwanamke aliyemuoa ambaye ni Dominique. Hii inasaidia watu kujenga tena imani kwenye gazeti la The Banner.

10. Dominique anarudi nyumbani kwa Gail Wynand na kukutana na mume wake. Gail Wynand anauliza kama kuna mapenzi yanaendelea kati yake na Howard Roark na kumwambia kwamba mapenzi hayo yalianza kipindi Howard Roark anafanya kazi kwenye mgodi wa mawe wa Guy Francon baba yake Dominique kama kibarua huko Connecticut.

11. Dominique anajitetea kwa Gail Wynand kwamba haikuwa ridhaa yake kwani Howard Roark alimbaka. Gail Wynand anamuuliza Dominique kama anataka kumchukulia Howard Roark hatua za kisheria juu ya jambo hilo. Dominique anamwambia hapana bali anataka kujitangaza kwenye gazeti la The Banner.

12. Guy Francon baba yake Dominique naye anasikia habari juu ya yaliyotokea kati ya binti yake na Gail Wynand. Guy Francon anampigia simu Dominique na kumwambia arudi nyumbani waende wakaishi pamoja kwenye jumba lake la kustaafu. Dominique anarudi nyumbani na baba yake anamwambia amlete nyumbani Howard Roark kumtambulisha ambaye anaonekana kumpenda sana. Dominique anafurahi lakini hawaongei sana.

13. Siku ya kesi ya Howard Roark inasomwa mahakamani, watu wengi sana wamehudhuria. Howard Roark mwenyewe yuko eneo la mshtakiwa na anasikiliza kwa makini sana.

14. Dominique amekaa eneo mashuhuda wakiwa pamoja na Steven Mallory, Austen Heller, Kent Lansing, Roger Enright, Mike na Guy Francon. Kwenye upande mwingine amekaa Ellsworth Toohey sambamba na Lois Cook, Gordon L. Prescott, Gus Webb, Lancelot Clokey, Ike, Jules Fougler, Sally Brent, Homer Slottern na Mitchell Layton. Mahakama imefurika sana watu wa kila aina wakiwepo wasanii mbalimbali, watu maarufu na watu wengine mbalimbali wakiwa kama mashuhuda.

15. Gail Wynand anakuja mahakamani peke yake kwa kuchelewa na kukaa nyuma. Anajaribu sana kukwepa kuangaliana uso kwa uso na Howard Roark. Kila wanapokutana Gail Wynand anatazama pembeni haraka.

16. Mahakama inaanza kwa mwendesha mashtaka kutangaza kesi na kutoa ufafanuzi wa kesi hiyo. Kisha mwendesha mashtaka anawataka mashuhuda wa tukio hilo kuanza kuzungumza yale waliyoshuhudia.

17. Polisi aliyemkamata Howard Roark kwa mara ya kwanza anazungumza kisha anazungumza mlinzi wa eneo hilo ambaye Dominique alimwondoa eneo la tukio kabla ya Howard Roark kulipua majengo hayo. Mwendesha mashtaka anamruka Dominique bila kumuhusisha kwenye kesi wala kuhitaji yeye kutoa ufafanuzi wowote.

18. Viongozi serikali wa mradi wa Cortlandt nao wanazungumza. Wanajaribu kutoa takwimu za mradi huo kuanzia gharama zake mpaka uwezo wake watu na shughuli zitakazofanyika.

19. Kesho yake Peter Keating anakuwa shahidi wa kwanza kuzungumza kwenye kesi hiyo. Mwendesha mashtaka anamtaka Peter Keating azungumza chini ya kiapo kama yeye ndiye aliyefanya kazi ya mradi wa ujenzi wa Cordlandt.

20. Peter Keating anajibu, hapana, hajafanya yeye. Mwendesha mashtaka anamuuliza ni nani amefanya anamjibu ni Howard Roark.

21. Mwendesha mashtaka anaendelea kumuuliza, alifanya kwa kuombwa na nani?, Peter Keating anajibu, yeye ndiye aliyemuomba afanye kazi hiyo. Mwendesha mashtaka akamuuliza kwa nini alimwita Howard Roark kufanya. Peter Keating akamjibu ni kwa sababu yeye hakuwa na uwezo wa kufanya mradi huo peke yake.

22. Mwendesha mashtaka akatoa karatasi ambayo walisainiana Howard Roark na Peter Keating na kumuuliza Peter Keating kama ule ndio mkataba waliosainiana na Howard Roark na Peter Keating akajibu ndio.

23. Peter Keating akaulizwa na hiyo ni sahihi ya Howard Roark akajibu ndio. Mwendesha mashtaka akamtaka Peter Keating asome mbele ya mahakama makubaliano yao kwenye mkataba huo na Howard Roark na Peter Keating akasoma makubaliano yote kwenye mkataba huo.

24. Katika kuzungumza kwake mbele ya mahakama Peter Keating anaonekana kutokuwa na uhakika na kukosa kujiamini, lakini zaidi anaonekana yote anayoongea ni kama amekariri. Karibu kila mtu ndani ya mahakama anayeshuhudia kesi hiyo anamuona Peter Keating kama amekaririshwa anayoongea na hilo linasababisha watu kukosa hamasa ya kumsikiliza.

25. Howard Roark anapewa nafasi ya kuongea ili kujitetea. Howard Roark anaanza kwa kuzungumza falsafa anayoisimamia ambayo ni kuhimiza katika upekee na ubinafsi wa watu (individualism).

26. Howard Roark anasema kwamba upamoja ni chanzo cha uovu na falsafa ya kuhimiza watu kujitoa kwa ajili ya wengine (altruism) imekuwa chanzo cha uharibifu na maanguko makubwa katika historia ya binadamu.

27. Howard Roark anasema kila binadamu ana upekee wake na unapaswa kuheshimiwa badala ya kuwaweka watu katika makundi kulazimisha mtazamo wa pamoja(collectivism). Anasema maendeleo makubwa ya binadamu na hatua ambazo watu wamepiga zimetokana na mtazamo wa ubinafsi na upekee wa watu. Hivyo juhudi za watu binafsi zinapaswa kuheshimiwa na suala la watu kutakiwa kujitoa kwa ajili ya wengine linapaswa kuhesabika kama uovu.

28. Howard Roark anasema hii dunia ina watu wa aina mbili, wale wanaounda au kuzalisha na wale ambao ni wategemezi(parasites). Anasema wanaounda ndio wajenzi wanaoleta thamani na maendeleo duniani na wale wategemezi ni waharibifu wanaopelekea anguko la mambo duniani siku zote.

29. Howard Roark anasema yeye anasimama kwenye misingi ambayo nchi ya Marekani imejengwa, ambapo ni nchi iliyosimama kwenye misingi bora zaidi duniani na imeweza kufanikisha mambo makubwa sana katika historia ya dunia. Nchi hiyo ya Marekani imejengwa katika msingi mkuu wa kuheshimu haki binafsi za mtu. Kwamba mtu atakuwa huru kuitafuta furaha yake mwenyewe na kufanikisha makubwa kiasi chochote anachotaka huku akilindwa na sheria ya haki ya kumiliki mali zake binafsi.

30. Howard Roark anasema ni kweli alilipua majengo hayo kwa sababu watu wategemezi walipora haki yake ya kuamua juu ya kazi aliyoifanya mwenyewe ifanyike namna gani. Anasema haki hiyo hakuna mtu mwenye mamlaka ya kuichukua kwake na kwa sababu kila kilielezwa kwenye mkataba watu hao walilenga kupora haki hiyo.

31. Howard Roark anamaliza utetezi na watu wanatawanyika mahakamani bila kuwa bayana juu ya maamuzi ya mwisho. Hata hivyo kesi inaamuliwa kwamba Howard Roark hana hatia.

32. Roger Enright ananunua mradi huo kutoka kwa serikali pamoja na kazi yote iliyofanyika mpaka hapo na kisha kumpa mkataba Howard Roark kuujenga mpya kwa ajili ya kuwapangishia watu wa kipato cha chini na sio kujitolea au kuwapa bure.

33. Gail Wynand anatoa talaka rasmi kwa Dominique baadaye mwezi Agosti.

34. Ellsworth Toohey anashinda kesi yake kwenye bodi ya wafanyakazi na Gail Wynand analazimika kumrudisha ofisini. Gail Wynand anaona hawezi kupangiwa namna ya kuendesha kampuni yake na kuwa radhi kuifunga kabisa ofisi hiyo kulipa kushindwa kuwa kwenye maamuzi ya kuamua mwenyewe. Hivyo baada ya Gail Wynand kumkaribisha tena ofisini Ellsworth Toohey, siku hiyo saa tatu kamili anafunga ofisi na kumwambia Ellsworth Toohey aondoke kwani ofisi hiyo haipo tena imefungwa.

35. Magazeti mengi mbalimbali yanamgombania Ellsworth Monkton Toohey kumwajiri kupata huduma yake. Ellsworth Toohey anachagua kufanya kazi katika gazeti la Courier ambalo lina sifa ya kipekee na heshima.

36. Gail Wynand anamwita Howard Roark ofisini kwake na kumwambia anataka asaini naye mkataba wa kujenga jengo refu zaidi duniani katika jiji la New York litakalokuwa ukumbusho wake kwa wakati huu. Howard Roark bila kusoma mkataba anakubali na kusaini mbele ya Gail Wynand kwamba atafanya kazi hiyo.

37. Gail Wynand anamwambia Howard Roark kwamba hatataka kuonana naye tena na mradi huo aufanye vyovyote anavyoona yeye ni sahihi. Kwa mambo mengine yote atadili na mtu wake wa kati na kwa jambo lolote huyo ndiye atakuwa anamfikishia taarifa. Afanye vyovyote vile kwa ajili yake yeye atakubaliana nalo.

38. Dominique ambaye kwa sasa ni mke wa Howard Roark na anajiita Mrs. Roark anatembelea eneo la ujenzi la jengo hilo refu zaidi duniani. Anafika na kuuliza alipo Howard Roark na kuambiwa yuko juu kabisa.

39. Dominique anapanda juu na kumkuta Howard Roark. Mahali hapo haoni kitu kingine zaidi ya mbingu, bahari na Howard Roark.

#MWISHO#

Architect Sebastian Moshi.

Whatsapp/Call +255717452790.

0 replies

Leave a Reply

Want to join the discussion?
Feel free to contribute!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *