AINA 7 ZA MICHORO YA JENGO UNAZOHITAJI.

Moja kati ya changamoto kubwa zinazojitokeza pale mteja anayehitaji huduma ya michoro ya ramani anapokutana na mtaalamu ni kushindwa kuelewana juu ya gharama za huduma hizo kutokana na kukosa uelewa wa ukubwa wa kazi husika kwa upande wa mteja. Kwanza kabisa uelewa wa namna kazi inavyofanyika na mchakato mzima inaopitia huwa hauko wazi kwa mteja, pia umuhimu wake na thamani ya kazi yenyewe sio jambo ambalo hueleweka kwa kila mtu kwa urahisi.

Sasa leo nataka nizungumzie aina saba za michoro ambazo ndio za lazima zinahitajika ili michoro ya ramani iwe imetimia. Aina hizi saba za michoro ndio matokeo ya mwisho ya kazi nzima ya huduma ya kitaalamu ya michoro kabla ya ujenzi kuanza maarufu kama kuchora ramani. Aina hizi saba za michoro ya ramani kwa upande wa usanifu majengo zinaweza kukupa picha ya uzito na ukubwa wa kazi husika. Hata hivyo hii ndio ile michoro mikubwa muhimu kwa upande wa usanifu majengo lakini kitaalamu kuna michoro mingine midogo midogo ambayo huongezeka kwa ajili ya kutoa ufafanuzi na uelewa kwa maeneo nyeti au yanayohitaji ufafanuzi zaidi hususan kwa miradi mikubwa au kitaalamu sana.

AINA 7 ZA MICHORO YA RAMANI YA USANIFU MAJENGO.

  1. Mchoro wa mpangilio wa majengo na vilivyomo katika kiwanja(site plan) – Hii huwa ni aina ya mchoro wa ramani ambayo inaonyesha mpangilio mzima wa kiwanja au eneo ambapo nyumba imejengwa. Mchoro huu huonyesha kuanzia eneo la kiwanja linavyoingika, eneo la maegesho ya magari, bustani, mpagilio wa mfumo wa maji taka, barabara na njia za kupita ndani ya kiwanja pamoja na majengo yote na miti iliyopo ndani ya kiwanja. Mchoro huu pia ndio ambao huonyesha hesabu ya matumizi ya eneo kwa ajili ya mamlaka husika kuangalia kama kiwanja kinatosheleza kwa mradi husika.
  2. Mchoro wa sakafu ya chini(floor plan) – Huu ni mchoro unaoonyesha mpangilio wa vyumba na vitu vingine vinavyohusika ndani sakafu husika ya ndani ya jengo. Wingi wa mchoro huu mara nyingi hutegemea na idadi ya sakafu za ndani ya jengo zisizokuwa na ufanano katika mipangilio yake.
  3. Michoro ya muonekano wa pande nne au zaidi za jengo(elevations) – Hii ni michoro inayoonyesha namna jengo linavyoonekana kutokea pande zote, upande wa mbele na nyuma na upande wa kulia na kushoto.Michoro hii husaidia kurahisi kuelewa mpangilio wa wima wa jengo na namna limetengeza uwiano wa vipengele vyake ambavyo ndivyo kwa pamoja huleta muonekano unaovutia wa jengo husika.
  4. Mchoro wa mkato wa ndani wa jengo kuanzia juu kwenye paa mpaka chini kwenye msingi(Cross-Section) – Huu ni mchoro au michoro ya jengo ambayo husaidia kuonyesha taarifa za ndani zaidi za kimpangilio na hasa maeneo yanayohitaji kueleweka kwa usahihi sana kama vile vipimo vya kwenye ngazi au lift. Mchoro wa section ni mchoro ambao pia huonyesha vipimo vya wima vya jengo kama vile urefu wa mlengo au dirisha, urefu wa paa, kina cha msingi wa jengo pamoja na mpangilio wa ngazi za jengo kuanzia chini kabisa kwenye msingi mpaka juu kabisa kwenye paa.
  5. Mchoro wa paa la jengo(Roof plan) – Huu ni ule mchoro unaoonyesha mpangilio wa paa namna litakavyojengwa na na vipengele vyake vyote kama vile migongo na mabonde pamoja na gata inayokusanya maji ya mvua na kuyapeleka sehemu iliyopangwa.
  6. Picha za muonekano wa jengo katika pembe mbalimbali – Hizi ni zile picha za muonekano wa jengo namna litakavyokuwa pale litakapokuwa limekamilika. Picha hizi kiufundi huwa sio za lazima kabisa kutokana na kwamba michoro mingine inakuwa imejitosheleza lakini zimekuwa zikisaidia sana katika kuhamasisha ujenzi wa jengo na kutoa mwelekeo(guidance) ya usahihi wa kule ambako jengo linaelekea. Picha za muonekano hupigwa katika pembe tofauti tofauti na zimekuwa zikiwavutia sana na kuwahamasisha wateja katika kukamilisha miradi yao ya ujenzi.
  7. Michoro ya mfumo wa majitaka wa jengo husika(Septic details drawings) – Hii ni michoro ambayo inaonyesha muundo na vipimo vya mfumo wa kuchuja na kuhifadhi majitaka kutoka kwenye jengo husika. Michoro hii ya mfumo wa majitaka huwa muhimu kwa sababu vipimo vyake hupaswa kuendana na ukubwa wa eneo la ujenzi na kuwa na mahusiano ya karibu na mpangilio wa nafasi nyingine katika kiwanja.

Hizo ndizo aina 7 za michoro ya ramani ya jengo kwa upande wa michoro ya usanifu wa jengo. Michoro hii ndio mara nyingi hutumika katika mijadala mbalimbali ya ujenzi na namna ya ufanikishaji wa ujenzi husika. Hata hivyo hiyo ndio michoro ya jengo ambayo huhitajika ukiondoa ile ya uhandisi mihimili ambayo huhitajika zaidi ikiwa jengo husika ni la ghorofa.

Ahsante sana

Architect Sebastian Moshi.

Whatsapp/Call +255717452790.

4 replies

Leave a Reply

Want to join the discussion?
Feel free to contribute!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *