GHARAMA ZA UFUNDI KATIKA UJENZI.

Moja kati ya maeneo ambayo watu wengi hupata changamoto sana kupata uhakika kama ni sahihi au sio sahihi ni eneo la gharama za ufundi katika ujenzi. Eneo hili limekuwa na mgogoro mkubwa kwa sababu kila upande hupata changamoto ya kupata uhakika wa usahihi wake. Hata hivyo mara nyingi eneo hili huishia kwenye makubalino zaidi kwa kila upande kuridhia kila kiasi ambacho kimekubalika na pande zote mbili.

– Changamoto kubwa inayokuja kutokea hapo baadaye ni kwenye suala la ubora kwani mara nyingi gharama za ufundi ni kati ya vitu muhimu sana ambavyo huamua ubora wa jengo husika. Lakini sasa kutokana na kwamba mara nyingi mapatano mengi hufanyika zaidi kwa hisia huwa ni rahisi sana kujikuta yanaishia kwenye matokeo ambayo aidha sio sahihi au sio yale yaliyokusudiwa.

– Hata hivyo suala la gharama za ufundi huwa ni changamoto kutokana na kwamba kila mradi una changamoto zake tofauti na hivyo kujikuta gharama zake zikitofautiana na kukosa uhakika lakini pia kila fundi au mkandarasi yuko na viwango tofauti vya ubora na hivyo hata gharama zao hutofautiana pia. Mwisho wa siku kwa baadhi ya watu ambao hutaka kuwa na msimamo katika gharama huamua kuweka asilimia fulani ya gharama za vifaa ndio huwa gharama za ufundi. Lakini pamoja na kuweka asilimia fulani za vifaa vya ujenzi kuwa ndio gharama za ufundi bado asilimia hizo hazifanani katika kampuni moja na nyingi wala mradi mmoja na mwingine.

– Sasa ni namna gani mtu unaweza kupata gharama sahihi ya ufundi? Japo gharama sahihi za ufundi za moja kwa moja sio rahisi kuzipata katika uhalisia kutokana na sababu nilizozieleza hapo juu lakini kwa ujenzi wa viwango sahihi usio wa mtaani huwa ni wastani au kuanzia 30% ya gharama ya vifaa vya ujenzi. Ikiwa unamtumia mkandarasi ambaye anafanya kazi kwa viwango vyenye ubora kiasi gharama za ufundi wa mradi kwa ujumla wake unaweza kuwa angalau wa kiasi hicho.

– Lakini hata hivyo gharama hiyo haiwezi kutumika namna hiyo kwa kipengele kimoja kimoja, gharama hiyo ni kwa mradi wote kwa pamoja. Nikizingumzia kipengele kimoja kimoja katika ujenzi namaanisha vipengele kama vile msingi wa jengo, ujenzi wa kuta, kupaua, kupiga ripu, kupiga rangi, kuweka sakafu ya vigae n.k., Hii ni kwa sababu gharama za vipegele hutofautiana sana kwani kuna vipengele ambavyo huchukua gharama kubwa zaidi kuliko hata gharama za vifaa vyake huku vipengele vingine vikichukua gharama kidogo sana hata chini ya asilimia 10 ya gharama za vifaa. Hivyo gharama hiyo ni wastani wa gharama yote ya jengo.

Karibu tuwasiliane.

Architect Sebastian Moshi.

Whatsapp/Call +255 717 452 790.

0 replies

Leave a Reply

Want to join the discussion?
Feel free to contribute!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *