GHARAMA ZA MIRADI YA UJENZI HAZILINGANI.

Katika maisha yetu ya kila siku moja kati ya vitu ambavyo wanasaikolojia wamekuwa wakitusisitiza sana ni kwamba ili tuwe na furaha ya kweli tunapaswa kuacha kujilinganisha na wengine. Hili jambo la sisi kujilinganisha na wengine limekuwa lina nguvu sana katika fikra zetu lakini japo linaweza kuwa linatuongezea hamasa ya kuweka bidii kubwa kwenye maisha lakini kwa sehemu kubwa limekuwa linakuja na gharama kubwa sana kwani linaathiri furaha yetu ya ndani na hata kutuletea msongo wa mawazo.

Kujilinganisha jambo ni jambo lililokuwa na manufaa kisaikolojia huko zama za zamani lakini kwa sasa sio jambo sahihi kufanya kwani linakuja na gharama kubwa. Hii ni kwa sababu kwa kufanya hivyo tunapoteza furaha na hata kuathiri afya zetu za akili na mwili pia. Kiuhalisia binadamu hatulingani kwani kila mtu ana historia yake tofauti kabisa, haiba yake tofauti kabisa na hata malengo na mategemeo tofauti. Pia tunatofautiana sana vipaji, imani na mitazamo hivyo kujaribu kujilinganisha na wengine badala ya kujikubali mwenyewe na kujiboresha ni kujitafutia matatizo yasiyo na suluhisho.

Sasa tunapokuja kwenye miradi ya ujenzi kuna ufanano mkubwa wa hali hii kama kwa binadamu na linaongezewa nguvu na tabia hii ya binadamu pia. Katika uhalisia gharama za miradi ya ujenzi hazilingani kutoka mradi mmoja na mwingine kwa sababu nyingi mbalimbali. Kwanza kabisa ni utofauti wa miradi yenyewe kwa ukubwa na mitindo ambapo hata kama nyumba zote ni za vyumba vitatu vya kulala au nyumba ya ghorofa moja yenye vyumba vinne bado ukubwa utakuwa tofauti. Lakini hata kwa miradi inayofanana kabisa kwa kila kitu ambayo inatumia ramani moja bado gharama zinaweza kutofautiana kwa sababu mbalimbali.

Kwanza kabisa gharama zinaweza kutofautiana kutokana na asili ya ardhi ya eneo(site) ambapo mradi husika unajengwa kuanzia muundo wake, aina ya udongo au miamba, au mwinuko au mteremko mkali unaoweza kuwepo. Baadhi ya maeneo mengine kama vile karibu na bahari yanaweza kuwa na ardhi ya mawe yale ya baharini yanayokwenda umbali mkubwa ardhi na kusababisha kazi kubw ana gharama kubwa kwenye kuchimba msingi wa jengo. Jambo lingine linalotokana na eneo ni umbai kutoka sehemu ambapo mahitaji ya vifaa na huduma nyingine za ujenzi zinakoweza kupatikana.

Jambo la mwisho ni machaguo ya mhusika mwenyewe au wahusika wenyewe, katika uhalisia binadamu tunatofautiana sana yale tunayoyapenda na ile tunayoyapa. Sasa ikiwa mtu anathamini zaidi mali zake na kutaka kuhakikisha ni za thamani kubwa basi atahakikisha ananunua vifaa vya thamani kubwa ili kuongeza thamani katika nyumba yake hiyo, na ikiwa mtu mwingine sio mtu wa kujali sana thamani katika mali zake sio rahisi kukuta akihangaika kutumia gharama kubwa kuhakikisha mali zake zinakuwa ni za thamani kubwa. Katika eneo hili napo gharama za ujenzi hutofautiana sana kati ya mradi mmoja na mwingine hata kama watu hao wameamua kutumia ramani moja inayofanana kwa kila kitu.

Hivyo sasa mtu unapokuwa unataka kufanya ujenzi na uko katika hatua ya kutafiti kujua gharama halisi za ujenzi ni vyema kuzingatia mambo mengi sana ili usije kupotoka juu ya gharama halisi za ujenzi. Kupotoshwa na kupotoka ni rahisi ikiwa mtu utaangalia mambo kwa juu na kujaribu kujilinganisha na wengine au kulinganisha mradi wako na mradi wa mtu mwingine usiyeujua kiundani wala kumjua mhusika kiundani na kufanya hitimisho kwamba gharama hizo zitakuwa sawa na za kwako pia. Ni muhimu sana kuzingatia utofauti huo uliopo ili kubaki katika uhalisia.

Karibu sana.

Architect Sebastian Moshi.

Whatsapp/Call +255 754 584 270.

0 replies

Leave a Reply

Want to join the discussion?
Feel free to contribute!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *