KUONGEZA THAMANI YA JENGO KATIKA HATUA YA UJENZI.
Changamoto kubwa katika fani ya ujenzi katika eneo la ubora na thamani ipo zaidi kwenye miradi midogo midogo kwa sababu ndio eneo ambalo miradi hii haifuati taratibu mbalimbali za kitaalamu zilizowekwa kwa sababu mbalimbali. Sababu kuu ya watu wengi ni gharama lakini sababu nyingine ya ndani zaidi ni kukosekana kwa uelewa wa hatari na madhara yanayokwenda kutokea ukilinganisha na gharama inayokimbiwa. Katika eneo hili la miradi midogo ambayo mingi ni ya watu binafsi na inajengwa kwa gharama binafsi za watu mteja akishakamilisha kupata michoro ya ramani za ujenzi huendelea na ujenzi bila kuendelea kushirikisha utaalamu kwenye hatua za wakati wa ujenzi.
Jambo hili ni sawa na mtoto kuzaliwa na kuanza kutunzwa bila kupelekwa kliniki kwa ajili ya kuangalia maendeleo ya mtoto. Mtoto anaezaliwa kisha kuendelea na malezi na asipelekwe tena kabisa kliniki wala kupata ushauri mwingine wowote wa malezi kiafya ni wazi kwamba mtoto huyo anaandaliwa kudumaa au hata kufariki kabla ya kufikisha umri wa miaka mitano. Kwenye ujenzi mfano huu hauna utofauti mkubwa, michoro ya ramani ya ujenzi inapokamilika kisha ujenzi kuanza bila kushirikisha utaalamu wa ujenzi kutoka kwenye taaluma husika wakati ujenzi unaendelea ni kujiandaa na mradi uliofanyika chini ya kiwango na thamani ya mradi husika kuwa chini kwa sababu mbalimbali.
Lakini watu wengi hufanya makosa ya kukamilisha ramani kwa mtaalamu kisha kuondoka nayo kwenda kuifanya bila ufuatiliaji wa yule mtaalamu husika na hapo ndipo mambo hufanyika chini ya kiwango wakati mwingine bila hata wao wenyewe kujua kwa sababu hawana uelewa mpana wa usahihi wa utaalamu husika. Hapo ndipo mtoto anapopata kwashiakor, pepopunda, utapiamlo na matatizo mengine mengi ya kiafya. Jengo linapopata kwashiakor watu wengi wataona hayo matatizo lakini hawatasema chochote kwa sababu sio kazi yao kusema na wala hiyo haiwahusu hivyo inaweza isiwe bayana lakini watu wenye wameona na wanalisemea kimoyomoyo.
Hivyo sasa ili kuhakikisha kwamba thamani ya jengo inakuwa juu sawa sawa na vile ilivyotegemewa mwanzoni wakati wa kufanya michoro unapaswa kuhakikisha kwamba timu yote ya wataalamu inahusika katika kutoa miongozo na kusimamia utekelezaji katika hatua ya ujenzi kuhakikisha kwamba kile kinachotegemewa kinatimizwa. Hili litasaidia kuhakikisha kwamba hata matatizo mengi katika ujenzi ambayo huja na hasara kubwa na ndogo wakati wa ujenzi yanatatuliwa.
Architect Sebastian Moshi.
Whatsapp/Call +255 717 452 790.
Leave a Reply
Want to join the discussion?Feel free to contribute!