KWENYE UJENZI UNAWEZA KUTUMIA MALIPO KUHAKIKISHA UBORA WA KAZI.

Kumekuwepo na changamoto kubwa sana kwenye suala la ufanyaji kazi na hasa kufanya kazi katika viwango bora na kwa usahihi. Changamoto za kufanya kazi isiyo katika viwango bora(poor workmanship) inachangiwa na sababu mbalimbali kama vile kushindwa kuweka vipaumbele kwa usahihi, malipo duni, kukosekana usimamizi na ufuatiliaji makini n.k., Lakini hata hivyo pamoja na changamoto zote hizo bado kuna njia nzuri ya kuhakikisha kwamba wahusika wanafanya kazi katika viwango vinavyotarajiwa. Na njia yenyewe ni mbinu ya kuwa na nguvu ya kuwadhibiti waweke umakini mkubwa sana kwenye kazi kwa hiari yao wenyewe na wao wenyewe ndio wanaokazana kuwajibishana kuhakikisha kazi inakuwa katika viwango bora kabisa.

Jambo hili linafanyika kupitia malipo kwa kuwapa masharti kwamba wakishamaliza kila hatua ya kazi, kazi yenyewe itakaguliwa na mtaalamu maalum wa viwango vya ubora akiangalia maeneo yote yanayopaswa kuchunguzwa kisha kuidhinisha au kukataa wao kulipwa kwa kazi husika. Mbinu hii huwa na nguvu sana kwa sababu msukumo mkubwa sana wa kazi unatokana na matumaini ya watu kulipwa baada ya kumaliza kazi yao, sehemu kubwa ya matumaini ya wahusika huwekwa kwenye malipo baada ya kukamilisha hatua hiyo ya ujenzi hivyo unapoweka masharti katika eneo hilo ni wazi kwamba kila kitu kitafanyika kwa ubora sana ili wasije kupata usumbufu kwenye kulipwa au wakati mwingine kukosa kabisa malipo yenyewe.

Kinachotakiwa kufanyika ni kila hatua kugawa kiasi cha malipo ya hatua husika katika mafungu kadhaa kadiri ya ukubwa na mgawanyiko wa hatua yenyewe kisha kuweka masharti kwamba malipo yatafanyika kwa utaratibu huo uliowekwa na kila hatua itakaguliwa kwa umakini sana kwa kufuata vigezo vilivyowekwa nak ama kazi haijafikia kiwango kinachotakiwa hakutakuwa na malipo. Kwa kufanya hivyo utashangaa jinsi ubora wa kazi umekwenda juu kutokana wahusika kuweka umakini mkubwa kwenye kazi zao. Kwa kufanya hivyo pia wale mafundi wasimamizi wa kazi hawawezi kuchukua watu wenye uwezo mdogo ili kuwalipa vibaya kwa sababu watajua tangu mwanzoni kwamba watakuja kuwakwamisha kwenye malipo hivyo wataingia gharama kwa kufanya maamuzi sahihi ya kuchukua watu sahihi ili kuhakikisha kazi inafanyika kwa viwango vinavyopaswa.

Karibu sana.

Architect Sebastian Moshi.

Whatsapp/Call +255 717 452 790.

0 replies

Leave a Reply

Want to join the discussion?
Feel free to contribute!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *