CHANGAMOTO YA KUKOSEKANA KWA MSANIFU MAJENGO KWENYE MRADI WA UJENZI.

Kama tulivyojadili mara nyingi sana katika makala zilizopita kwamba kuna mapungufu mengi sana hujitokeza katika miradi ya ujenzi kwa sababu ya kukosekana kwa wataalamu husika wa ujenzi huo. Ikiwa mtaalamu kamili hatatumika kuanzia hatua ya michoro mpaka mwisho basi jengo litakuwa na mapungufu makubwa sana kuanzia ya kimatumizi mpaka kimuonekano. Na ikiwa mtaalamu atahusika katika hatua ya michoro lakini akakosekana kwenye hatua ya utekelezaji wa ujenzi mapungufu hayo yatapungua lakini bado yataendelea kuwepo ambayo yatasababisha jengo kutokea katika viwango sahihi kwa sababu anakuwa amekosekana mtu wa kufanya maamuzi sahihi na hivyo baadhi ya maamuzi yanaishia kuwa sio saihihi.

Leo tunajadili kwa kifupi changamoto zinazoweza kujitokeza kwa kukosekana kwa mtaalamu wa usanifu majengo katika hatua ya utekelezaji wa ujenzi. Katika hali ya kawaida mpangilio wa jengo kimuonekano na kimatumizi ni kazi ya msanifu wa jengo, au kwa kifupi tunaweza kusema kazi yote ya kulitengeneza jengo ukiondoa mifumo ya mihimili na huduma za ndani ya jengo ni kazi ya msanifu wa jengo. Hivyo msanifu wa jengo ndiye mtu mwenye kushughulika na karibu kila kitu kinachohusiana na jengo. Hivyo sasa msanifu wa jengo anapokosekana kinachotokea ni baadhi ya vipengele vinavyosaidia mzunguko sahihi ndani ya jengo na mpangilio sahihi unaoleta muonekano maridadi na unaoendana na saikolojia ya macho kupuuzwa au kubadilishwa kwa namna ambayo italeta usumbufu kwa mtumiaji au mtazamaji wa jengo.

Mara nyingi ukitembelea mradi wowote ambao msanifu wa jengo hakuwepo wakati wa utekelezaji wa ujenzi wenyewe utakuta kuna maamuzi yalifanyika tofauti na ilivyokuwa inaelekezwa kwenye mchoro kwa sababu mbalimbali lakini maamuzi hayo hayakuwa sahihi na yamesababisha usumbufu au uharibifu fulani wa kiufundi, kimatumizi au kimuonekano katika jengo hilo. Ni kitu ambacho kinaweza kukusangaza lakini naweza kukuhakikishia kwamba ni karibu miradi yote suala hilo hujitokeza, hata ikiwa msimamizi wa mradi huo “site foreman” ni mzoefu kiasi gani. Hii ni kwa sababu aidha yeye ndiye atafanya maamuzi au atashinikizwa na mteja wafanye maamuzi hayo na kwa sababu utakuta haoni chochote kinachoharibika kwa sababu ya maamuzi hayo basi atajikuta ameshafanya maamuzi hayo.

Twende kwenye eneo lolote la ujenzi ambalo mradi wa ujenzi unaendelea bila usimamizi na nitakuonyesha makosa yanayoendelea ambayo yataleta usumbufu kwenye jengo hilo aidha wa kimatumizi au wa kimuonekano.

Karibu sana.

Architect Sebastian Moshi.

Whatsapp/Call +255 717 452 790.

0 replies

Leave a Reply

Want to join the discussion?
Feel free to contribute!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *