MCHAKATO WA KUPATA KIBALI CHA UJENZI.
Juzi nimepigiwa simu na binamu yangu mmoja ambaye alikuwa anajulisha kwamba anataka uchukua kibali cha ujenzi ili aweze kuanza kujenzi wa nyumba yake katika eneo analoishi bila kukutana na bugdha wala usumbufu wa aina yoyote kutoka kwenye mamlaka husika. Binamu yangu alinipigia akaniamba, “Seba nataka nichukue kibali cha ujenzi, hivi nahitajika nini na nini”, mimi nikamwambia kwamba anahitaji kuwa na seti nzima ya michoro ambayo imepigwa mihuri pamoja na hati ya kiwanja aende navyo halmashauri ya manispaa husika ambapo ataenda kujaza fomu za kibali cha ujenzi na zikishapita michakato mingine kama vile kufanya malipo itafuata. Akaniambia, “kwa hiyo sasa nikishajaza hizo fomu na kufanya malipo ndio wataniandikia hicho kibali cha ujenzi?”, nilicheka kidogo.
Hapo ndipo nilikumbuka kwamba watu wengi hawaelewei kwa nini mtu anapaswa kuchukua kibali cha ujenzi ili kufanya ujenzi na mchakato wa kukipata ukoje. Kiuhalisia ni kwamba mtu unachukua kibali ujenzi sio kwa sababu tu unapaswa kuchukua bali kibali cha ujenzi ni uthibitisho kwamba mradi wako umetimiza vigezo vyote muhimu vinavyotakiwa kutimizwa ili kukidhi viwango vilivyowekwa na mamlaka husika ambavyo vinalenga kuhakikisha kwamba kazi zote zinafanyika kitaalamu na kwa viwango sahihi. Hivyo kibali cha ujenzi ni mchakato unaolenga kuhakiki kama kazi husika ya ujenzi inayoenda kuanza imekidhi vigezo vilivyowekwa na halmashauri husika.
Hivyo basi michoro ya ramani ya jengo au nyumba inayoenda kujengwa inapopelekwa katika halmashauri husika huwa inakwenda kupitishwa kwenye idara mbalimbali za halmashauri ya mji/jiji/manispaa husika kufanyiwa ukaguzi katika kila idara kuhakikisha kwamba imekidhi vigezo vya idara husika. Idara za halmashauri ya mji, manispaa au jiji ambapo michoro hiyo inapitishwa ni kama vile idara ya ujenzi, idara ya mipango miji, idara ya afya, idara ya mazingira n.k. Ikiwa michoro hiyo itaonekana ina hitilafu fulani au haijakidhi vigezo au kuwaridhisha wataalamu wa idara husika basi inapaswa kurudishwa na kwenda kufanyiwa marekebisho husika ndipo kurudishwa tena manispaa kukamilisha mchakato wa kupata kibali cha ujenzi.
Zoezi hilo huweza kuchukua angalau wa siku kadhaa au wiki kutegemea na wahusika wanafanya kazi kwa haraka kiasi gani. Baada ya zoezi hilo kukamilika faili la michoro husika linawekwa kwenye orodha ya mafaili ambayo yataingia kwenye kikao cha jopo ya wataalamu katika halmashauri husika ambao ndio watafanya maamuzi ya mwisho kupitisha mafaili hayo na hivyo kutoa idhini rasmi ya vibali husika vya ujenzi kuandikwa kisha kusainiwa tayari kwa kukabidhi wahusika. Hilo ndio zoezi zima la kupata kibali cha ujenzi kutoka kwenye halmashauri ya mji/jiji/manispaa husika, ambapo unaweza kuona kwamba sio zoezi la siku moja wala sio jambo ambalo linakwenda kiurahisi rahisi tu kama mtu anavyochukua leseni ya biashara.
Karibu sana.
Architect Sebastian Moshi.
Whatsapp/Call +255 717 452 790.
Leave a Reply
Want to join the discussion?Feel free to contribute!