UJENZI NI UTAALAMU NA UZOEFU.

Moja kati ya changamoto ambayo huwakuta wataalamu waliomaliza chuo siku za karibuni na kuingia kwenye kazi za ujenzi ni pamoja na kuwa na uwezo mdogo kwenye kazi za ufundi wa ujenzi. Suala la wataalamu wa ujenzi kuwa na uwezo mdogo katika shughuli za ujenzi haliwaathiri vijana waliotoka chuoni peke yake bali hata wataalamu wakongwe ambao hawajatumia muda wa kutosha kuwekeza katika maeneo ya ujenzi kujifunza kwa kina masuala ya ufundi wamekuwa wahanga sana wa jambo hili. Wapo watu wengi hata baada ya kufanya kazi miaka mingi bado wamekuwa na uoga wanapokuwa maeneo ya ujenzi kwamba wanaweza kupata aibu kutoka kwa mafundi ujenzi ambao wanafahamu mambo mengi kwa kina kuwazidi.

Tatizo ni kwamba inapaswa mtu hata baada ya kumaliza chuo na kupewa shahada anatakiwa kwenda kwenye mradi wa ujenzi na kujifunza kuanzia mwanzoni ili kujenga uwezo mkubwa katika mambo ya ufundi na sio tu utaalamu pekee kwenye ujenzi ili aweze kufanya maamuzi muhimu kwa usahihi akiwa kama msimamizi. Lakini kutokana na kuogopa kuonekana hajui licha ya kuwa na elimu kubwa wengi wameamua kutokiri udhaifu na hivyo kuendelea kubaki hawajui kwa miaka mingi sana. Wanachoshindwa kuelewa ni kwamba utaalamu na uzoefu ni vitu viwili tofauti kabisa na vyote vinapatikana kwa namna tofauti na hakuna kimoja kilichojitosheleza wala ambacho kimebeba mwenzake.

Wataalamu wanapaswa kujua kwamba kukosa uzoefu baada ya kumaliza shule ni jambo la kawaida kabisa wala sio la aibu kwa sababu utaalamu na uzoefu katika ufundi ni vitu viwili tofauti. Katika utaalamu unakuwa umejifunza mambo kwa nadharia zaidi na hivyo unapofika wakati wa kufanya ndipo unakutana na uhalisia ambao unatofautiana kwa kiasi na yale uliyojifunza kwenye nadharia. Kutokuwa na uzoefu bado hakukuondolei utaalamu wako wala haimaanishi utaalamu wako hauna maana bali utaalamu wako ni wa muhimu sana na unahitajika sana kwenye miradi ya ujenzi hivyo hivyo pamoja na kwamba unakosa uzoefu katika ufundi.

Hivyo weka aibu na fedheha pembeni na weka bidii kwenye kukusanya uzoefu katika ufundi mpaka ujenge uwezo mkubwa kuliko wale uliowakuta kwenye fani. Na kwa kuwa wewe tayari ni mtaalamu basi suala la uzoefu ni jambo rahisi sana kulifanikisha kwa haraka na kwa viwango kama utakuwa na juhudi. Unapokuwa na vyote viwili utaalamu na uzoefu utafanikisha makubwa sana kwenye fani ya ujenzi.

Karibu sana.

Architect Sebastian Moshi.

Whatsapp/Call +255 717 452 790.

0 replies

Leave a Reply

Want to join the discussion?
Feel free to contribute!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *