GHARAMA YA UJENZI ULIOPEWA NI MAKADIRIO TU.
Unaweza kufurahia au kuumizwa na gharama ya ujenzi uliopewa kwa kuiangalia kwa sababu umeamini kwamba hiyo ndio gharama inayokwenda kumaliza kazi yako. Nachopenda kukushauri ni kwamba hutakiwi kufurahia wala kuumizwa na gharama ya ujenzi unayopewa na fundi au mkandarasi kwa ajili ya kukujengea jengo lako kwa sababu kwa sehemu kubwa hiyo sio gharama halisi. Na japo wakati mwingine gharama hiyo huenda ikawa ni kubwa kuliko gharama itakayomaliza jengo lako lakini mara nyingi zaidi huwa inakuwa ndogo kuliko gharama itakayomaliza jengo lako.
Kwa kuwa taarifa tunazopokea huwa zinaathiri sana hisia zetu basi watu wengi wakipokea taarifa ya makadirio ya gharama za ujenzi wa nyumba zao huwa na hisia tofauti kadiri ya uzoefu na uelewa. Lakini kwa bahati mbaya au nzuri gharama za ujenzi sio kitu ambacho kinaweza kupatikana kwa uhakika kiasi hicho isipokuwa makadirio pekee. Utakuta mtu aliyekupatia gharama zake za ujenzi wa jengo lako akikuomba kazi hiyo unajikuta unamchukia na kumuona ni mwenye tamaa kutokana na gharama alizokupa ambazo umeziona ni kubwa sana lakini unapofanya ujenzi huo na kufika mwishoni unakuta kumbe mtu yule alikuwa sahihi kabisa na pengine hata alikupa gharama za chini.
Wakati mwingine ni unapoanza ujenzi ukiwa umepewa gharama za makadirio na mkandarasi au fundi anayekuomba kazi na unaona kwamba gharama zake ni nzuri na kumpa kazi lakini mradi unapofikia katikati ndio unagundua kwamba kumbe aina za vifaa alivyochagua ni vya bei ndogo na hauko tayari kuvitumia kwenye nyumba yako. Badala yake basi unakuja kuamua kununua vifaa vingine hasa kwa upande wa eneo la umaliziaji ambavyo ni vyenye thamani ya juu zaidi na ubora hivyo kujikuta gharama ya ujenzi wako imeongezeka sana tofauti na ulivyofurahia mwanzo hata kutoa kazi kwa mhusika. Hivyo ni muhimu sana kuzingatia kwamba suala la gharama za ujenzi haziko katika msimamo mmoja na mwishoni ndipo utakuja kupata picha kamili ya uhalisia wa kile ulichokuwa unafanya, mwanzoni utaishia kujidanganya pekee na kutoa hukumu isiyo ya haki.
Karibu sana.
Architect Sebastian Moshi.
Whatsapp/Call +255 717 452 790.
Leave a Reply
Want to join the discussion?Feel free to contribute!