MALIPO YA MAFUNDI NA VIBARUA KWENYE MRADI WA UJENZI NI KWA KAZI AU KWA SIKU?
Katika kuhakikisha kwamba miradi ya ujenzi inafanyika kwa ubora na kwa gharama nafuu zaidi kumekuwa na mbinu mbalimbali za kushughulika nayo katika utekelezaji ikiwemo usimamizi na udhibiti wa ufundi na mafundi. Kumekuwa na utofautiano kwamba ni njia ipi sahihi ya kuwalipa mafundi ambayo inafanya kazi vizuri zaidi na inayoweza kusaidia kwa uhakika kupunguza gharama na kuhakikisha ubora wa jengo kati ya kulipa mafundi kwa kazi waliyofanya kwa siku au kulipa kwa kuuza kazi kama kazi. Katika uhalisia njia zote zina faida na hasara kutegemea na namna ya usimamizi wa kampuni husika na kile wanachokitegemea au kukilinda.
Hata hivyo njia ya kulipa mafundi na vibarua katika mradi wa ujenzi kwa siku inaweza kuwa ni ngumu kidogo kwa sababu inahitaji usimamizi mkali sana na ufuatiliaji mkali kuhakikisha kwamba kazi inafanyika kwa kasi licha ya mafundi kujua kwamba siku ikiishi kiwango chao cha malipo ni kile kile. Njia huenda ikawa inapunguza gharama zaidi ikiwa kazi kupitia usimamizi makini kazi itafanyika kwa kasi na kumalizika ndani ya muda mfupi na kwa ubora uliokubalika lakini hilo mara nyingi huwa ni changamoto sana kuliko mtu unavyoweza kulifikiria.
Hivyo njia ya kuuza kazi kwa mafundi na vibarua huku ukiwasimamia kuhakikisha kwamba wanazingatia viwango sahihi vya ubora uliowekwa inapunguza ulazima wa kufuatilia sana kazi kwa kina na kuhangaika sana na watu. Unaweza kuweka msimamizi mkuu wa ufundi ambaye atalipwa kwa siku, kwa wiki au kwa mwezi wa kusimamia ubora wa kazi na kufuatilia mafundi na vibarua wote kuhakikisha wanafanya kazi bora na kwa viwango vilivyowekwa. Lakini wale watekelezaji wa kazi wanapewa kazi kwa malipo kwa kiasi cha kazi unachokubaliana nao. Uzuri wa njia hii ni kwamba kila mtu atajisukuma kufanya kazi amalize haraka na kwa ubora uliokubalika ili kuokoa muda na gharama ambazo zinaendelea kumwangukia yeye binafsi kwa sababu amechukua mradi kwa kazi na sio kwa muda.
Karibu sana.
Architect Sebastian Moshi.
Whatsapp/Call +255 717 452 790.
Leave a Reply
Want to join the discussion?Feel free to contribute!