MCHUNGUZE SANA FUNDI WA UJENZI WA BEI RAHISI, HUENDA ANAKUIBIA VIFAA.

Ndugu mdau wa ujenzi watu wengi wamekuwa wakitafuta sana namna watafanikisha mambo yao yanayohitaji fedha kwa gharama nafuu kadiri inavyowezekana, na kweli hilo ni jambo jema na muhimu sana hasa kwa rasilimali yenye uhaba kwa wengi kama rasilimali fedha huku vipaumbele vyake vikiwa ni vingi sana. Lakini bado ni muhimu sana wakati unafanya hivyo kuongeza umakini sana katika kufanikisha kwani watu wengi au kwa makala hii niseme mafundi wengi nao ni wajanja na wana akili nyingi sana katika kufanikisha kile anachokitaka.

Mafundi wengi au hata wakandarasi kabisa wanafahamu vizuri tabia za wateja walio wengi kwamba wanavutiwa na wajenzi wenye gharama nafuu za vifaa na hivyo hukimbilia huko, hivyo ili yeye kufanikisha malengo yake hudai kiasi kidogo cha malipo ya ufundi wa kazi hiyo huku akijua atafanya kila linalowezekana kufidia gharama zake kwenye vifaa nya ujenzi. Sawa utasema kwamba wewe ni mjanja zaidi kwa sababu vifaa utanunua mwenyewe na kuhakikisha unalipia vitu vyote peke yako hakuna pesa inayopitia kwa fundi au mtu mwingine yoyote. Kumbe hujui kwamba hata hapo bado unajidanganya.

Najua unafahamu kwamba huyo unayejihusisha naye ni mtaalamu wako na unamwamini katika kazi hiyo ya ufundi ndio maana umemchukua na ndiye unayemsikiliza kwa mambo yote ya kitaalamu anayokwambia. Kwa maana hiyo aidha anajua unaponunulia vifaa au yeye ndiye atakwambia ukanunue sehemu fulani kwa sababu katika duka hilo ndipo kuna vifaa vyenye ubora au ambavyo ndivyo vinavyomfaa yeye ili ufundi wake uwe wa viwango bora. Kwa sababu huyo ni mtaalamu wako huwezi kumkatalia vinginevyo kazi inaweza kuharibika na akakulaumu wewe mwenyewe kwamba hukumsikiliza na kununua pale alipokuelekeza kwenye vifaa vinavyomfaa au vyenye ubora ndio maana kazi ikaharibika.

Hivyo kwa sehemu kubwa utamsikiliza bila hata wewe kujua kumbe kule dukani tayari ana mkataba na mwenye duka tena pengine wa muda mrefu jinsi anavyofaidika kupitia wewe kwa aidha kuuziwa kwa bei kubwa au kuibiwa sehemu ya vifaa ambavyo havitafikishwa katika eneo lako la ujenzi. Kuhusu ukaguzi kwa kesi ya vifaa ambavyo havijafikishwa katika eneo la ujenzi huenda yeye mwenyewe ndiye anahakiki au mlinzi au mtu yeyote anayejua anahakiki alishaongea naye tayari na kumpanga bila ya wewe kufahamu chochote. Na ukumbuke kwamba watu wote hawa anawahonga hivyo sio rahisi kukujali wewe kama watakavyojali maslahi yao wanayokwenda kuyapata kwa fundi huyo. Hata wenye maduka wanafaidika zaidi kupitia mafundi wanaowaletea biashara kila siku na mara kwa mara kwa miaka na miaka kuliko wewe ambaye hawategemei ununue tena baada ya hapo.

Hivyo unapokuwa umepata fundi ambaye unaona umempata kwa bei rahisi na ukafikiri umenufaika sana kabla hujaanza kushangilia kwanza chunguza kwa undani kuhusu urahisi wake kwani huenda ni wa bei mbaya kuliko yule uliyemkimbia ukidhani ni wa bei kubwa sana. Kwa sababu uchakachuaji wa vifaa vya ujenzi ndio chanzo kikubwa cha ubovu wa majengo mengi na hata nyufa nyingi kwenye majengo huchangiwa sana na suala zima la uchakachuaji wa vifaa ambao hufanywa na mafundi wasio waaminifu ambao huja kujukikana wakati makosa yalishafanyika zamani na pengine hata asijulikane kabisa. Mara nyingi rahisi ndio ghali ambayo inachelewa kujulikana ughali wake na binadamu wana akili nyingi na mipango mingi sana vichwani mwao kuliko unavyoweza kutegemea.’

Architect Sebastian Moshi.

Whatsapp/Call +255 717 452 790.

0 replies

Leave a Reply

Want to join the discussion?
Feel free to contribute!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *