KUJUA KAMA GHARAMA YA UJENZI NI SAHIHI LINGANISHA BEI YA MKANDARASI NA MKADIRIAJI MAJENZI WAKO.

Miezi michache iliyopita tulifanya kazi ya mteja wetu mmoja ambaye tulitokea kuelewana sana mwanzoni kiasi cha kutembeleana nyumbani kujadili mradi wake wa ujenzi na hata kuhudhuria matukio ya kifamilia. Kwa kweli mteja huyu ni kati ya wateja waungwana sana, wenye utu na ambao hawana ule ubinafsi wa kujiangalia wenyewe pekee bali wanajali hata kuhusu wengine. Hivyo mteja huyo akataka kutupa kazi ya ujenzi kwa namna ambayo itafanyika kwa ubora sana lakini bila kutuumiza sisi. Hivyo tuliweza kutengeneza orodha ya gharama ya vifaa na ufundi vitakavyotumika katika ujenzi huo.

Baada ya kuwasilisha kwake aliangalia ripoti ya gharama zile kwa kushirikiana na watu wake wa karibu na baada yah apo waliona kwamba hizo ni gharama kubwa sana kiasi kwamba walipata hofu na kupoteza matumaini na sisi. Hivyo waliahirisha kutupa kazi ile na badala yake wakatafuta mtu mwingine ambaye atasimamia ujenzi huo huku wao wakipeleka vifaa katika eneo la ujenzi. Mwisho walitutaka sisi tuwe tunatembelea ujenzi huo kuhakikisha kwamba jengo linajengwa kwa viwango bora na sahihi vilivyopangwa ambapo tutakuwa tunalipwa kwa kila siku tunayotembelea na kutoa ushauri wa kitaalamu hatua kwa hatua.

Tulikubaliana hivyo na kazi ile ikaanza ambapo usimamizi na ushauri wa kitaalamu kwa hatua ya ujenzi ilianzia tangu wakati wa kuliseti jengo katika sehemu yake maarufu kama, “building setting out”. Baada ya msingi kukamilika mteja yule alinifuata na kuniambia kweli nilikuwa sahihi kwani katika gharama za ujenzi nilizompa kwa hatua ya msingi makadirio ya gharama yamekuwa kama tulivyokuwa tumempatia hivyo kumbe gharama zile zilikuwa sahihi. Tulikubaliana na kushukuru kwamba nilikuwa nimempatia gharama sahihi na wala hakukuwa na lengo lolote la kutaka kujinufaisha sana kwa kumpa gharama kubwa kupita kiasi. Tumeendelea na kazi yake na ameendelea kushukuru sana kwa mchango ambao tumeuweka katika kuongeza sana thamani ya jengo lake kwa usimamizi wa wakati huu wa ujenzi.

Sasa ni nini kinachopelekea watu kuona gharama na kubwa na baadaye kugundua haikuwa sahihi? Jibu ni rahisi ambalo ni kutumia hisia katika kuhukumu kabla kujiridhisha kuhusu uhalisia wake. Ni kweli kwamba ni vigumu kufahamu gharama halisi ikiwa hujui hali halisi ya gharama za vifaa na ufundi katika ujenzi hivyo kibinadamu utaishia kutumia hisia kuhukumu. Sasa ili iwe rahisi kufahamu kama gharama unazopewa na mkandarasi ni zinakufaa au hazikufai unapaswa kutafuta mtaalamu husika wa masuala ya ukadiriaji majenzi anayejulikana kama mkadiriaji majenzi au jina la kitaalamu Quantity Surveyor(QS) akufanyie makadirio ya gharama ambayo utalinganisha na mahesabu hayo ya mkandarasi na hilo litakusaidia kujua kama mtu huyo amekupa bei sahihi kwako au bei ambayo sio sahihi kwako. Kama bei ni sahihi kwako unafanya naye kazi lakini kama bei sio sahihi kwako unaachana naye.

Kwa miradi ya ujenzi ambayo tumekuwa tukifanya kwa namna hiyo imekuwa ni rahisi sana kuelewana na mteja naye mteja kufurahi na kuridhika kwa sababu anajua bei hiyo hajalanguliwa na kwamba ni bei sahihi kwake. Lakini isipokuwa tu kama mteja ana uzoefu wa kujenga mara kwa mara ndio anaweza kuelewa pale unapomletea makadirio ya gharama zake, kwa wateja wengine ambao hawana uzoefu na gharama za ujenzi huwa na mitazamo tofauti na wengi mitazamo hasi.

Karibu sana.

Architect Sebastian Moshi.

Whatsapp/Call +255 717 452 790.

0 replies

Leave a Reply

Want to join the discussion?
Feel free to contribute!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *